Breaking News

Your Ad Spot

Mar 6, 2010

LIGI KUU YA SOKA TANZANIA BARA

Dakika 6 za nyongeza zainyoonyesha mambo Simba
*Yaishinda JKT Ruvu 3-1
MABAO mawili yaliyofungwa katika dakika sita za nyongeza, leo yameiwezesha Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3 -1 dhidi ya timu ya JKT Ruvu Stars ya mkoani Pwani, katika mechi ya mzunguko wa pili wa michuano ya soka ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya mashabiki..
      Ushindi huo umeiwezesha Simba kukusanya pointi 53, baada ya kushuka dimabni mara 19, imeshinda mechi 17 na kutoka sare mechi mbili, hatua ambayo sasa inaifanya timu hiyo kubakiza pointi mbili ili itangazwa bingwa mpya wa michuano hiyo ya ligi msimu huu.
      Dalili za Wekundu hao wa Msimbazi kama inavyojulikana na mashabiki wake, zilianza tangu dakika za awali za pambano hilo, ambapo katika dakika ya kwanza tu almanusura Mussa Hassan' Mgosi' aipatie bao la kuongoza. Baada ya kuunasa mpira na kuachia mkwaju mkali ambao ulitoka nje ya lango la JKT.
      Bao la kwanza la Simba lilipatikana dakika ya 26 kupitia kwa kiungo mkabaji, Mohammed Banka, ambaye alifanikiwa kuukwamisha kimiani mpira huo baada ya kupiga mkwaju mkali wa adhabu akiwa nje ya eneo la hatari la JKT na moja kwa moja kwenda kimiani.
      Kuingia kwa bao hilo kulionekana kuamsha ari kwa vijana wa JKT, ambao walianza kuonana vyema na kupeleka mashambulizi mfululizo langoni kwa Simba. Hali hiyo ilifanya JKT kupata adhabu ya penalti ambayo ilitolewa na mwamuzi wa kati Israeli Nkongo, baada ya kipa Juma Kaseja wa Simba, kumwangusha mshambuliaji, Hussein Bunu wa JKT akiwa mbioni kuzifumania nyavu zake.
    JKT ilipata bao lake kusawazisha kupitia kwa nahodha wake, Haruna Adolf, ambaye alipiga shuti hilo lililokwenda kimiani katika dakika ya 40. Hivyo hadi timu hizo zikienda mapumziko, timu hizo zilikuwa zimetwishana nguvu kwa kufungana bao 1 - 1.
    Simba ambayo inanolewa na kocha raia wa Zambia, Patrick Phiri ilikianza kipindi cha pili kwa kasi kama ilivyokua kwenye kipindi cha kwanza, hatua ambayo iliifanya ipate penalti katika dakika ya 63 ambayo ilitolewa na Nkongo kutoka mkoani Dar es Salaam, baada ya mlinzi mmoja wa JKT kumwangusha Nico Nyagawa katika eneo la hatari.
   Lakini hata hivyo, Mgosi ambaye alionekana kuwa mwiba mkali wa walinzi wa timu ya JKT alijikuta akipiga mkwaju mkali ambao ulipita juu ya lango la wapinzani wake, baada ya kurudia penalti ya kwanza ambayo awali aliipata na mwamuzi kumwamuru arudie kutokana na kupigwa kimakosa.
   Alikuwa Mgosi katika dakika za lala Salama ambaye aliwainua vitini mashabiki wa Simba, alipoifungia timu yake bao la pili kwa shuti baada ya kuunasa mpira na kuukwamisha kimiani kwa shuti lililomwacha kipa wa JKT, Jackson Chove akichupa bila ya mafanikio.
    Bao la ushindi lilihitimishwa na mshambuliaji hatari, Uhuru Selemani, ambaye aliunasa mpiora akiwa upande wa Kaskazini Mashariki na kuambaambaa nao hadi upande wa Kaskani Magharibi na kisha kuachia mkwaju mkali ambao ulimpita kipa wa JKT, Chove na kutinga wavuni.
   Chupuchupu mechi hiyo iingie dosari, baada ya kupulizwa kwa filimbi ya mwisho na mwamuzi Nkongo, kwani wachezaji wa JKT walionekana kumzonga mwamuzi huyo, na kubwa walionekana wakipinga kitendao cha mwamuzi wa mezani wa mechi hiyo, Hamis Chang'walu kuonyesha bango na kuongeza dakia sita zaidi.
    Hata hivyo askari Polisi waliokweko uwanjani hapo waliweza kuwatuliza na kuwaondosha waamuz hao uwanjani hapo, bila ya kupatwa na rabasha zozote zile.
    Simba: Juma Kaseja, Haruna Shmate, Juma Jabu, Juma Said 'Nyosso', Joseph Owino, Mohammed Banka, Nico Nyagawa/ Uhuru Seleman, Mussa Hassan'Mgosi', Ulimboka Mwakingwe/ Mohammed Kijuso na Ramadhan Chombo'Redondo'..
   JKT Ruvu: Shaban Dihile/ Jackson Chove, Kessy Mapande/ Manyuki Ally, Damas Makwaya, Stanley Nkomola, Shaibu Nayopa, Kisimba Luambano, Yahaya Khan, Mwinyi Kazimoto, Hussein Bunu, Abadallah Bunu na Haruna Adolf.

Wachezaji wa Simba wakishangilia baada ya mechi
Kipa wa Simba Juma Kaseja (kushoto) akiungama na wenzake kushangilia timu yake ilipomaliza mchezo ikiwa mshindi kwa mabao 3-1

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages