.

TSAVANGIRAI AMTEMBELEA JK IKULU

Mar 31, 2011

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo na
 Waziri Mkuu Zimbabwe Morgan Tsvangirai,  Ikulu jijini
Dar es Salaam leo asubuhi (Freddy Maro).

MBUNGE WA MCHINGA AIPIGA TAFU UHURU QUEENS

Mbunge wa Jimbo la Mchinga Mheshimiwa Said Mtanda , jana amefanya mambo yazidi kuwa mazuri kwa timu ya netiboli ya  Uhuru Queens kwa kuipatia sh. 100,000 taslim, kwa ajili ya kusaidia matumizi ya wachezaji wa timu hiyo inayoshiriki michuano ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF). Pichani, mbunge huyo akimkabidhi fedha hizo, kwa  mchezaji wa timu ya Uhuru Queens Salome Mwasamale, katika chumba cha habari cha Uhuru Publications Ltd, mtaa wa Lumumba mjini Dar es Salaam. Michuano hiyo inaendelea katika viwanja vya TTC Chang'ombe  ambapo Uhuru Queens inaongoza katika kundi C la mashindano hayo ikiwa na pointi sita hadi sasa. Wanaoshuhudia makabidhiano hayo kutoka kushoto ni Mdau wa timu hiyo, Laurencia Masota, Meneja wa timu Jane Mihanji na Mhariri wa gazeti la Burudani Rashid Zahoro.

DK.BILAL ATOA POLE TETEMEKO LA TSUNAMI LILILOTOKEA JAPAN

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Mohamed Gharib Bilal, akisalimiana na Balozi wa Japan Nchini Tanzania Mhe. Hiroshi Nakagawa wakati alipokwenda kwenye Ofisi ya Ubalozi wa Japan Upanga jijini Dar es Salaam leo kwa ajili ya kusaini kitabu cha pole kwa  maafa ya tetemeko na Tsunami, nchini Japan hivi karibuni 
Akisaini kitabu hicho. (Picha zote na Maelezo na Amor Nasor -VPO)

NAIBU WAZIRI MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA ATEMBELEA ZANTEL

OFISA Mkuu wa Teknolojia katika Kampuni ya Zantel, Moncef Mettiji wa pili (kulia) akimuonyesha moja ya mitambo ya mawasiliano ya kampuni hiyo, Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, Charles Kitwanga alipotembelea kampuni hiyo Dar es Salaam, leo. Kuliani ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Zantel, Ali Bin Jarsh.

BAADA YA KUZOA TIZO KIBAO TANZANIA KILI MUSIC AWARDS 20% ALONGA

*Asema hapendi sifa bila ushahidi
*Anajiita 20% kwa sababu ya akili na maisha anayoishi
 *Asema anaandika nyimbo zake katika fikra za Ki-hip hopAbbas Hamisi  20% akipiga gita ndani ya
 studio ya Combinations Sound.
 MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya, Abbas Hamisi, maarufu kwa jina la 20%, mwishoni mwa wiki iliyopita aling’ara baada ya kushinda tuzo tano za muziki za Kilimanjaro katika sherehe zilizofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Abbas aliibuka mshindi katika tuzo ya msanii bora wa kiume, mwimbaji bora wa kiume, mwandishi bora wa nyimbo wa mwaka, wimbo bora wa mwaka na wimbo bora wa Afro-pop.

Hata hivyo, Abbas hakuwepo ukumbini kupokea tuzo zake. Zilipokelewa na mtayarishaji wake wa muziki, John Shariza ‘Man Water’ kutoka Kampuni ya Combination Sound.

Je, kwa nini Abbas hakuwepo kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee siku hiyo? Aliupokeaje ushindi huo? Ni kwa nini anajiita 20%? Nini kinafuata katika maisha yake na kazi zake? Makala hii ya ana kwa ana ya mtandao wa Bongo Celebrity inaelezea.

SWALI: Mambo vipi 20%?
JIBU: Ee bwana mimi Mungu ananisaidia, sijui wewe bradha.
SWALI: Yuko nasi pia. Kwanza hongera sana kwa ushindi wako wa mwishoni mwa wiki iliyopita. Tuzo tano kwa mkupuo sio mchezo. Hongera sana
JIBU: Ni kweli kabisa Bradha. Hata mimi namshukuru sana Mungu kwa kuniwezesha kuibuka mshindi namna ile.
SWALI: Labda swali la kwanza, ambalo watu wengi wangependa kujua ni ilikuwaje ukakosa kuhudhuria shughuli ya utoaji wa tuzo zile? Nini kilitokea?
JIBU: Kwa kweli hata mimi mwenyewe nilisikitika kutokuwepo pale. Ilitokea tu kwa bahati mbaya nilikuwa na onyesho lingine la kijamii mjini Tabora, ambalo nilishalitengea nafasi muda mrefu sana uliopita. Kwa hiyo ilinibidi kwenda kule kwa sababu kama unavyojua, katika onyesho huwezi kutuma mwakilishi kama ambavyo unaweza kufanya au nilivyofanya katika tuzo za Kili.
SWALI: Hilo linaeleweka na naamini mashabiki wako watakuelewa. Sasa zile taarifa kwamba umeshinda ulizipataje na ulizipokea namna gani?
JIBU: Taarifa za ushindi ule nilizipata kupitia luninga kwa sababu nilikuwa sehemu fulani nikifuatilia kila kitu kupitia ITV kabla ya kwenda kwenye onyesho letu. Pale nilipokuwa nilifuatilia mpaka niliposhinda tuzo ya nne ndio jamaa wakanifuata kwamba sasa twende kwenye onyesho. Taarifa za tuzo ya tano nilizipata nikiwa tayari nipo kwenye onyesho pale uwanjani Tabora. Kwa kweli nilifurahi sana kupata ushindi ule.
SWALI: Sasa kuna baadhi ya mashabiki wamekuwa wakijiuliza huyu 20% ni nani? Hawa ni wale, ambao walikuwa hawajawahi kufuatilia kwa karibu muziki wako au kazi zako za kiusanii. Labda kwa faida ya mashabiki hao, ambao hawakufahamu, wale ambao ndio ilikuwa mara ya kwanza kusikia jina lako, je jina lako kamili ni nani na kwa nini uliamua kujiita 20%?
JIBU: Jina langu kamili ni Abbas Hamis. Ni mzaliwa wa mkoa wa Pwani. Ni mtoto wa pili katika watoto wa kiume wa mzee wangu.
Hili jina la 20% nililipata kutokana tu na jinsi mimi mwenyewe nilivyokuwa najiona.Hata wewe mwenyewe kama utabahatika kusimama na mimi, utajua mimi kweli ni 20% kutokana na kimo na maumbile.
Halafu pili mimi najitambua kama 20% kimatendo kwa sababu tofauti na labda watu wengine mashuhuri au matajiri duniani, ambao wanaishi kwa kutegemea utajiri waliorithi au akili nyingi walizopewa na Mungu na mambo kama hayo, mimi natumia akili yangu ndogo kuishi na kufanya mambo yangu, kitu ambacho mimi nakiona ni 20%, yaani kulinganisha akili yangu na labda za wale manabii wa hapo zamani.
SWALI: Sasa nikisikiliza nyimbo zako tangu umeanza, nyimbo kama vile ‘Maisha ya Bongo’ ukielezea jinsi watu wanavyochomwa moto, vijana hawana mwelekeo; yaani suluba zinazowakuta vijana wa Uswazi, ulikuwa kwenye mahadhi ya hip hop zaidi kwa (mtazamo wangu). Ingawa bado unazungumzia mambo yale yale (heko kwa hilo), kwanini umebadilisha mtindo kidogo? Au ulikuwa unajitambulisha tu?
JIBU: Ni kweli kwamba kuna mabadiliko kidogo hususani katika midundo.Kwa jumla mimi natumia mitindo mbalimbali.Utaona kwa mfano wimbo kama ‘Maisha ya Bongo’ upo kwenye mtindo wa reggae zaidi wakati wimbo kama ‘Money Money’ upo katika mahadhi ya Pop zaidi.
Na mimi mwenyewe jambo moja, ambalo labda watu wengi hawajui ni kwamba, ni mtunzi mzuri wa nyimbo za mitindo tofauti tofauti kama vile reggae, hip hop, zouk nk.Kwa hiyo kinachotokea hivi sasa ni kwamba naziandika nyimbo zangu katika fikra za ki-hip hop na kisha kuziimba katika mahadhi tofauti tofauti.
SWALI: Hivi karibuni kumekuwa na hoja kwamba mwelekeo wa Bongo Fleva kwa ujumla umekuwa kama haueleweki. Lakini inaonekana wewe sasa hivi (hata kabla ya kuchukua tuzo) ndio ‘alama’ ya muziki wa Tanzania. Wengine wanaufananisha uwepo wako katika muziki wa kizazi kipya na kama vile alivyo Chameleon kule Uganda. Je, unachukuliaje maoni kama hayo? Je ni jukumu ambalo uko tayari kulibeba au inakuwaje?
JIBU: Nianze kwa kusema nashukuru kusikia sifa kama hizo kwa sababu najua Chameleon ni msanii anayeheshimika vyema kule kwao. Lakini kiukweli mimi katika maisha yangu nilivyo ni kwamba sipendi sifa ndogo na pia sipendi sifa bila ushahidi.Mimi ninachopenda kuona ni kwamba watu wote au wasanii wote waliopo katika hii tasnia ya Bongo Fleva wawe wanaumiza vichwa.
Binafsi nathamini sana suala la kuumiza kichwa katika tungo na kazi zangu. Kwa hiyo kama kuna, ambao wananiona mimi kama ‘mfano wao wa kuigwa’, basi la muhimu ni kufuata nyayo kwa kuumiza vichwa katika tungo zao na kazi zao kwa ujumla kabla hata hawajaingia studio. Binafsi namshukuru Mungu kwamba mpaka hivi sasa sijawahi kutengeneza wimbo ambao ukaishia studio tu.Namshukuru sana Mungu kwa hilo.
SWALI: Sasa hebu tuongelee kidogo kuhusu wimbo wako wa ‘Malumbano’, ambao ni miongoni mwa nyimbo zako zilizotokea kupendwa zaidi, ni wimbo wa mapenzi. Bahati mbaya au nzuri, Tanzania sasa hivi wasanii wengi wanapenda kuimba nyimbo za mapenzi. Unadhani ni kwa nini wimbo ule, ingawa uko katika maudhui, ambayo tunaweza kusema yameshazoeleka kupita kiasi, wenyewe umetokea kubamba zaidi?
JIBU: Kikubwa zaidi katika nyimbo ya ‘Malumbano’ ni kwamba nimeongelea mazingira ambayo tunaweza kuita ni mapenzi.Lakini ‘Ya nini malumbano’ ni neon, ambalo linajibeba lenyewe,halimaanishi mapenzi peke yake.
Maudhui ya wimbo huu yanaweza kutumika katika maeneo mengi, mfano hata barabarani, ukiwa barabarani na gari yako mbovu na ukaona inataka kuzimika, ni vyema ukaliweka pembeni.Kwa busara unalisogeza pembeni na kupisha wengine.Hakuna haja ya malumbano.
Mfano mwingine unaweza kuwa na taaluma yako nzuri, unaingia kazini na unakuta eneo limetawaliwa na chuki na maneno maneno. Katika mazingira kama hayo, mimi sioni kama kuna haja ya kuendelea kulumbana.Basi unaweza tu kujiweka pembeni kwani taaluma yako inabakia kichwani mwako.Mifano ipo mingi sana kuonyesha jinsi gani haina haja ya Malumbano ambayo ndio maudhui makubwa ya wimbo ule.
SWALI:Sasa hebu tuongelee kidogo masuala ya ubunifu kwamba unapokuwa studio yule mtayarishaji wako anakupa uhuru wa kufanya unachotaka au kuna mtu/watu wanaokupa muongozo zaidi. Unapoingia studio huwa inakuwaje?
JIBU: Mimi binafsi huwa napenda sana kufanya kazi na prodyuza, ambaye ananipa pia muda wa kuzungumza na kuchangia katika uboreshaji wa kazi nzima kwa sababu mimi ninapotunga wimbo huwa natunga pia kila kitu, mfano mapigo, kiitikio, mpangilio wa ala na viginevyo.
Kwa hiyo huwa napenda kupata prodyuza, ambaye pia ananisikiliza. Nashukuru Mungu kwamba watayarishaji wangu wa muziki ninaofanyanao kazi, tunashirikiana vizuri kabisa katika kuhakikisha kwamba kitu kinachotoka ni katika kiwango cha kueleweka na kukubalika.
SWALI:Taarifa nilizonazo zinasema kwamba watu waliposikia umeshinda tuzo kibao, kuna sehemu inasemekana watu walishangalia kama tunavyoshangilia mpira. Unajisikia vipi ukisikia vitu kama hivi?
JIBU: Kwa kweli inatia moyo na kuleta raha sana kuona jinsi gani watu wanakubali kazi zangu. Na nasikia kelele hizo hazikuwa pale ukumbini tu bali sehemu zingine nyingi nchini Tanzania.Hiyo ni kumaanisha kwamba watu wengi walipenda ushindi ule utokee na walijitolea na kujituma katika kunipigia kura. Haishangazi kuona kwamba jina langu lilipokuwa linatajwa tu katika kategori fulani fulani, tayari watu walikuwa wanalipuka kwa kushangilia.
Napenda kuwashukuru sana mashabiki wangu na watanzania wote kwa kuniwezesha kuibuka na ushindi huo.
SWALI: Sasa nini kinafuata baada ya hapa.Unaendelea na ziara zako,unajiandaa kufyatua albamu nyingine au mambo gani yanaendelea?
JIBU: Kusema kweli hapa nahitaji kuingia ofisini kumalizia filamu yangu moja ninayofanya na ndugu yangu Afande Sele. Inaitwa Haki Iko Wapi? Baada ya hapo nitaendelea na kazi zangu zingine na pengine kama kutakuwa na ‘Kili Music Awards Tour’-maana mpaka hivi sasa bado sijapokea au kusikia chochote kuhusiana na kitu kama hicho. Zaidi ni kuendelea na kazi tu kama kawaida.
SWALI: Labda kwa kumalizia tu,una ushauri gani kwa vijana wanamuziki wenzako au wengine wanaoota kufikia mafanikio kama haya yaliyojidhihirisha kupitia Tuzo za Muziki za Kili?
JIBU: Ninachopenda kuwaambia neno la kwanza ni waandike sana.Na neno la pili waandike sana na hata neno la tatu pia waandike sana.
SWALI: Asante sana kwa muda wako 20%. Kila la kheri katika kazi zako.
JIBU: Asante sana Bradha.

YANGA YAILAMBA AZAM FC 2-1

Beki wa Yanga, Shadrack Nsajigwa (kushoto) akijaribu kumthibiti  mshambuliaji wa Azam FC, Mrisho Ngassa, timu hizo zilipomenyana leo, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Yanga ilibuka na ushindi wa mabao 2-1. (Picha kutoka Blogu ya Dina Ismail).

MBUNGE WA MCHINGA ASAINI KITABU MAAFA YA TSUNAMI JAPAN

Mar 29, 2011

MBUNGE wa Mchinga, Saidi Mtanda akitia saini kitabu cha maombolezo ya maafa ya tetemeko la Tsunami yaliyotokea Japan, mapema mwezi huu,leo kwenye Ubalozi wa nchi hiyo mjini Dar es Salaam, Kushoto ni, Balozi Mdogo wa Japan, Shuichiro Kawaguchi. 
Mheshimiwa Mtanda akimpa pole balozi huyo mdogo, baada ya kusaini kitabu. Kushoto ni Katibu Msaidizi wa Ubalozi huo, Shigeru Nemoto 
Mheshimiwa Mtanda akiagana na Balozi huyo 
Mteshimiwa Mtanda akizungumza neno la mwisho, na Ofisa Mipango katika ubalozi huo Tatsujiro Suzuka. Kushoto ni Balozi mdogo na katikati ni Nemoto..

RAIS KIKWETE AKAGUA AKIBA YA CHAKULA; ATEMBELEA WIZARA YA SOPHIA SIMBA

Mar 28, 2011

RAIS Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akikagua akiba ya chakula katika ghala linalohifahdi akiba ya chakula ya Taifa( National food Reserve Agency) lililopo chang’ombe jijini dare s Salaam leo asubuhi.Wapili kushoto ni Mtendaji Mkuu wa wakala wa taifa wa hifadhi ya Chakula Bwana Charles Walwa, na watatu kushoto ni Waziri wa kilimo chakula na Ushirika Profesa Jumanne Maghembe(picha na Freddy Maro)
Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii jinsia na Watoto wakati wa ziara yake ya kikazi wizarani hapo leo mchana.Wapili kulia ni Waziri wa wizara hiyo Bi.Sophia Simba(picha na freddy Maro)

TUWAENZI WAHANGA WA BIASHARA YA UTUMWA-BAN KI MOON

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, kushoto wake ni Naibu wake, Dkt. Asha-Rose Migiro na kulia  Bw. Joseph Deiss, Rais wa Baraza Kuu la 65 la Umoja wa Mataifa, wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kuwakumbuka wahanga wa utumwa na biashara ya utumwa, maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila  March 25 yalifanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Na Mwandishi Maalum
Mwishoni mwa wiki, Umoja wa Mataifa uliadhimisha siku ya Kimataifa ya kuwakumbuka wahanga wa utumwa na biashara ya  utumwa.
Maadhimisho  hayo ambayo ujumbe wake kwa  mwaka huu ulikuwa “ the  living legacy of 30 million untold stories” hufanyika kila  March 25 yaliambatana na  makongamano, maonesho ya dhana zilizotumika kusafirishia watumwa, ngoma za kiafrika  na  vyakula vya asili ya afrika.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki Moon,  pamoja na mambo mengine amesisitiza haja na umuhimu wa kuendelea kufundishwa kwa  historia ya utumwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Ban Ki Moon  anasema kwa kufundisha na kujifunza historia ya utumwa na biashara ya utumwa pamoja na  madhara makubwa yaliyotokana na  biashara hiyo,  itakuwa ni njia moja wapo ya kuwaenzi wahanga wa utumwa. Lakini pia kujifunza nini kilipelekea kuanzishwa kwa biashara hiyo.
Akasema kuwa  UNESCO imefanya kazi kubwa ya  kukusanya na kuhifadhi kumbukumbu na matukio ya kutisha  na  utumwa na biashara ya utumwa. Lakini anakiri kuwa bado kuna mengi ya kujifuza  kuhusu mamilioni ya waafrika walioathirika na biashara hiyo. kwamba kazi hiyo inatakiwa kuendelea mashuleni na katika maeneo mengine.
Katibu Mkuu wa UM, katika mazungumzo yake, amesisitiza kuwa biashara hiyo ya utumwa ilikuwa ni moja ya biashara mbaya sana iliyokandamiza na kuudhalilisha utu na hadhi ya mtu mweusi na kwamba  madonda   biashara hiyo bado yapo hadi leo hii.
“ kwa kuadhimisha siku hii ya kimataifa,  ni sehemu ya kuwakumbuka wahanga wa utumbwa,  tunatambua utu wao, heshima yao, kudhalilishwa kwao na mateso waliyoyapata” anasisitiza Ban Ki Moon
Na kuongeza kuwa maadhimisho haya pia yanalenga kutambua mchango wa wale wote waliojitolea  mhanga licha ya hatari kubwa iliyowakabilia kuipinga na hatimaye kumaliza biashara ya utumwa. 
 “ Hili hasa ndio kusudio la maadhimisho ya siku hii ya kimataifa ya watu wa asili ya afrika. Na ndio maana  mchakato wa ujenzi wa mnara wa kumbumbu ya biashara ya utumwa  unaendelea   kama njia moja wapo ya kuendelea kuwaenzi wahanga hao.” Anaeleza zaidi
Kwa Mujibu wa Katibu Mkuu,  maadhimisho hayo   pia yalikuwa yanalenga kutambua  mchango  na  juhudi za wanaharakati ambao hadi leo hii wanaendelea na kazi ya kupigania na  kupinga  aina mbalimbali za ukandamizaji na ukiukwaji wa haki za binadamu.
 Aidha  Ban ki Moona, anasema  kuwa ingawa  miaka 400 imepita tangu kukomeshwa kwa biashara ya utumwa, kumeibuka  aina mpya ya utumwa, anautaja utumwa huo kuwa ni ndoa za umri mdogo, usafirishaji haramu wa watoto, uuzwaji wa wanawake, na utumwa wa madeni unaowalazimu baadhi ya sehemu ya jamii kufanya kazi kwa muda mrefu kulipia madeni ya familia zao.
 “Ni vema tukautambua ukweli wa biadhara ya utumwa,   hebu basi  na tuwakumbuke wahanga  hao.  lakini lazima  pia tukumbuke na aina mpya  ya utumwa unaoendelea katika jamii zetu na  tukusanye nguvu za kuukabili  utumwa huu mpya” anasisitiza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

UONGOZI WA VODACOM WAMTEMBELEA JK IKULU

Mar 27, 2011

Rais Jakaya Kikwete, akisalimiana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya simu za mkononi, ‘Vodacom Group’ ,  Pieter Uys, wakati wa ujumbe wa kampuni hiyo ulipofika Ikulu Dar es Salaam juzi kwa ajili ya mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali ya kuongeza uwekezaji nchini. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Dietlof Mare. Picha na Mpigapicha Wetu 
Rais Jakaya Kikwete, akimkaribisha  Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya simu za mkononi, ‘Vodacom Group’ ,  Pieter Uys, wakati wa ujumbe wa kampuni hiyo ulipofika Ikulu Dar es Salaam juzi kwa ajili ya mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali ya kuongeza uwekezaji nchini, (kushoto) ni Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Dietlof Mare. Kulia ni Mkurugenzi wa Mahusiano wa kampuni hiyo, Mwamvita Makamba. Picha na Mpigapicha Wetu

KANGOYE AONGOZA MAANDAMANO KUUNGA MKONO HOTUBA YA JK

MKUU wa wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, Christopher Kangoye,
akipokea maandamano ya zaidi ya sungusungu  na wananchi 2,000, katika
maandamano ya kumuunga mkono Rais Jakaya Kikwete na kulaani
maandamano yanayofanywa na viongozi wa Chadema.
 
SERIKALII wilayani Kwimba imesema kwamba, itawakamata na kuwafikisha kwenye mkono wa sheria wanasiasa watakaotumia majukwa kuitukana, kufanya uchochezi na kuhatarisha amani.

Akihutubia maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano wa kupinga maandamano ya uchochezi, hivi karibuni mjini Ngudu, Mkuu wa wilaya ya Kwimba Christopher Kangoye   alisema wanasiasa ‘uchwara’ wasiifanye Kwimba uwanja wa kupangia vurugu na uchochezi. Kangoye  ambaye ni Mtemi wa jeshi la jadi la wilaya hiyo (Sungusungu) alisema hayo baada ya kupokea heshima na salamu za askari zaidi ya 2,000 wa jeshi hilo , waliodai kwamba wamechoshwa maandamaono na mikutano ya uchochezi ya wanasiasa.

“Tutawakamata wanasiasa wanaodai wanakuja kufanya mikutano kwa nia nzuri kisha wanatumia fursa hiyo kufanya uchochezi, kumtukana Rais na Serikali, Kwimba siyo uwanja wa kupangia uchochezi,” alisema Mkuu huyo wa wilaya.

Alieleza kwamba nchi yetu imejengwa kwa misingi imara ya demokrasia, amani, mshikamano na umoja wa kitaifa ambao unapaswa kulindwa kwa nguvu yote na kila mmoja, hivyo kuruhusu kundi la watu waivuruge ni kuuza amani ya watanzania.

Alisema maelfu ya sungusungu hao, wananchi, viongozi wa vyama vya siasa, Vitongoji, Vijiji, Kata na wilaya waliohudhuria kwenye mkutano huo wa kupinga siasa za uchochezi zinazoweza kuvunja amani ya nchi, ni ishara kwamba wana Kwimba wanataka amani siyo mambo ya Tunisa au Libya .

Sungusungu hao wakiongozwa na Mteni wa Tarafa ya Ibindo Shimbi Mogani, wakiimba nyimbo za kusisitiza amani kwa lugha ya kisukuma, walisema uchaguzi umekwisha wana Kwimba wanachapa kazi na kusomesha watoto kuondoa umaskini na ujinga, waachiwe amani waliyozoea.

Waliimba “Obebe Slaa nelechama lyako mle bayojase.” Yaani wewe Dk Slaa na chama chako ni wachonganishi na kuwaasa wananchi wasiwape nafasi ya kuchochea vurugu na pia kumtaka Mtemi wao (Kangoye) achukue hatua kama serikali wilayani mwake wanapotokea wachochezi.

Awali mkutanao huo ulitanguliwa na maombi ya sala kuiombea nchi iwe na amani na kuepuka vurugu kama za Misri, Tunisia na Libta, kabla ya jeshi hilo kutoa heshina na nasaha hizo.

Waliotoa maombi hayo ni Sheikh Mkuu wa wilaya ya Kwimba Sad Seif (BAKWATA) na Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa wilayani humo, Mchungaji Samuel Makima (AICT Kwimba) ambao walisema kuwa  
uchaguzi ulisha isha viongozi wakapatikana hivyo wajibu wa kila moja ni kutii mamlaka ya serikali.

20% ATAMBA KILI TANZANIA MUSIC AWARDS AZOA TUZO 5 KWA MPIGO

DMI WAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI


                           Baadhi ya wafanyakazi wa DMI na mgeni rasmi
(walioko upande wa kulia) wakitazama bidhaa za nguo
kwenye maonyesho yaliyoambana na maadhimisho hayo,
kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha St. Joseph,
 Mbezi Luguluni, Dar es Salaam.
 MPANGO wa kuweka fedha kidogo kila wiki, umewezesha vikundi vya maendeleo ya wanawake vilivyoko chini ya Shirika la Mabinti wa Maria Imakulata (DMI) mjini Dar es Salaam na mkoa wa wani, kufikisha akiba ya sh. milioni 668.4,hadi sasa.

Hayo yalisemwa jana na Sista Lily wa DMI, katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanywa na Wanawake wa vikundi hivyo, kwenye Viwanja vya Chou Kikuu cha St. Joseph, Mbezi Luguluni, Dar es Salaam, ambapo pia yaliambana na shughuli mbalimbali ikiwemo maonyesho ya kazi za mikono na nguo.

Alisema, mwaka 2004 kilianza kikundi kimoja, kikiwa na wanachama 15, na akiba ya sh. 200,500 na sasa kuna vikundi 350 vyenye wanawake 5575 ambapo kutokana na kuweka akiba kidogo kila wiki sasa vikundi hivyo vimefikisha kiasi cha sh. 666,465,000.

Sista Lily alisema mafanikio hayo yametokana na wanawake hao, kushika kwa makini mafundisho waliyokuwa wakipewa na Masista wa DMI, yenye lengo la kuleta chachu ya maendeleo ya wanawake kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Alisema, wanavikundi wote wamekuwa wakipewa semina na elimu bora ya uendeshaji na utunzaji fedha za mikopo ili ziweze kuzaa faida, kwa njia za kuzalisha mali katika sekta mbalimbali ikiwemo ufumaji, kilimo, biashara za maduka na biashara ndogo ndogo.

Sista Lily alisema, mbali na kuwafundisha stadi za biashara, pia hufunzwa namna na kutunza mazingira, afya zao na elimu ya mawasiliano.

Kuhusu malengo ya baadaye, Sista Lily alisema, sasa wanalenga kuanzisha muunganiko wa vikundi kitaifa ili kuleta chachu zaidi ya kimaendeleo na pia wana mpango wa kufanya kazi na asasi za kiraia.
Alisema katika mipango ya mwaka huu, zaidi ya wanawake 2000 hadi 3000 watanzisha miradi mbalimbali ya biashara, kuanzishwa mabwawa ya kisasa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji katika vijiji vitano ili kuwa na shamba la kisasa katika jamii husika.

Akizungumza katika sherehe hizo, mgeni rasmi, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya wanawake, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Judy Kizenga, aliipongeza DMI kwa ubunifu wake, wa kuleta mipango inayowalenga wanawake na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Mkurugenzi huyo ambaye aliwakilisha Waziri wa wizara hiyo, alisema, wanawake na wananchi kwa jumla, wanazingatia mafundisho ya dini wakiwa na hali bora kuliko wakiwa masikini, hivyo Shirika la DMI limefikiria jambo la msingi kuhakikisha kwamba pamoja na kuwafundisha uumini wa dini lakini wanawake wanakuwa na hali bora kimaisha.

Maadhimosho ya Siku ya Wanawake Duniani, hufanyika Machi 8 ya kila mwaka, lakini DMI hawakuweza kufanya kutokana na kuwa katika majukumu mengine, ikiwemo kuhudhuria yale ya kitaifa yaliyofanyika Kibaha mkoa wa Pwani.

STARS YAILAZA AFRIKA YA KATI 2-1

Mar 26, 2011


Timu ya Taifa, Taifa, Stars imefanikiwa kuifunga Afrika ya Kati mabao 2-1, katika Mechi ya awali kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani, iliyopigwa leo jioni kwenye Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Nitakufunga kesho..., inaelekea ndivyo Kocha wa Stars Jan Poulsen alivyokuwa akimwambia kocha wa Afrika ya Kati, wakati wakiwaambia waandishi wa habari maandalizi ya mechi hiyo jana, kwenye ofisi za TFF mjini Dar es Salaam.

JK APOKEA UJUMBE KUTOKA KWA EL BASHIR WA SUDAN

Mar 25, 2011

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akipokea ujumbe maalumu wa Rais Omar El Bashir wa Sudan kutoka mjumbe maalum ambaye pia ni Waziri wa mambo ya Nje  wa Sudan Ali Ahmed Karti aliouwasilisha ikulu jijini Dar es Salaam leo asubuhi.(picha na Freddy Maro).

NMB YAIPA VIFAA STARS

Mkuu wa kitengo cha Masoko na Mawsiliano wa Benki ya NMB, Imani Kajula, akikabidhi vifaa vya michezo kwa Mkurugenzi wa ufundi wa TFF, Sunday Kayuni kwa ajili ya Timu ya Taifa Taifa Stars leo. Kushoto ni Katibu Mkuu wa TFF,  Angetile Osseah

RAIS KIKWETE ATINGA WIZARANI KWA PROF. MWANDOSYA

Mar 24, 2011

Rais Jakaya Kikwete akisalimia wafanyakazi baada ya kuwasili Ofisi za Wzara ya Maji, Ubungo, Dar es Salaam, leo asubuhi.
Rais Kikwete akiwa na Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya lwenye ofisi za wizara hiyo

WAZIRI SAMIA AKUTANA NA BALOZI WA NORWAY

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano Bi. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi wa Norway Nchini Tanzania Bi. Ingunn Klepsvik kuhusu Masuala ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, mchakato wa Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na changamoto za Muungano. Mazungumzo hayo yanefanyika leo Ofisini kwake Mtaa wa Luthuli Mjini Dar es Salaam.(Picha na Ali Meja)

SERENGETI BEER YAIPA STARS MILIONI 100 KWA AJILI YA MECHI YAKE NA AFRIKA YA KATI: VIJANA NAO WAONDOKA LEO KWENDA CAMEROUN

KAMPUNI ya Bia ya Serengeti (SBL), imetoa sh. milioni 100, kusaidia timu ya Taifa, Taifa Stars katika mechi ya timu hiyo na Afrika ya Kati, kesho kwenye Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam. Pichani, Meneja wa bia ya Serengeti Allan Chonjo, akimkabidhi mfano wa hundi ya fedha hizo Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Angetile Oseah, katika Ofisi za TFF mjini Dar es Salaam, leo. Mbele ni Kocha mkuu wa Stars Jean Poelsen na wachezaji wa timu hiyo, Nahodha, Shadrach Nsajigwa na Mshambuliaji, Athumani Machupa.

WACHEZAJI wa timu ya Taifa ya Vijana, wakiwa katika basi katika Ofisi za Shirikisho la soka Tanzania (TFF), kwa ajili ya kwenda Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, jana, tayari kwa safari ya kwenda  Cameroun, kwenye mechi yao na timu ya vijana ya nchi hiyo.

'SIFA ZA KIJINGA'

Bango hili lipo kandoni mwa Barabara ya Morogoro, eneo la Kimara

MSIBA FIVE STARS: TIZO MGUNDA AZIKWA MKURANGA LEO

Mar 23, 2011

JENEZA lenye mwili  wa aliyekuwa msanii wa Five Stars,Tizo Mgunda likiwa tayari kwa ajili ya kuswaliwa mwili huo, nyumbani kwao, Tandika , Dar es Salaam, leo kabla  kuzikwa katika makaburi ya Mkamba, Mkuranga, mkoani Pwani. Mgunda alifariki juzi na wenzake 12, katika ajali ya basi dogo mkoani Morogoro.

SEMINA YA TCRA KIBAHA; NI KWA AJILI YA WATUMIAJI WA HUDUMA ZA MAWASILIANO


SHEIKH wa Wilaya ya Kibaha mkoa wa Pwani, kutoka Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Sheikh Husein Madenge, akijiandikisha katika daftari la mahudhurio, katika semina ya watumiaji huduma za mawasiliano, iliyofanyika leo katika Hoteli ya Njuweni mjini Kibaha. Kushoto ni Karani wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanhzania (TCRA) inayoratibu semina hiyo, Rebecca Mawolle.
Katibu Tawala wa mkoa wa Pwani, Bernard Nzyungu akifungua semina hiyo, kwenye hoteli ya Njuweni, Kibaha mkoa wa Pwani.
OFISA Mwandamizi masuala ya watumia huduma za mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA), Thadeo Ringo, akimkabidhi zawadi ya simu aina ya Nokia, mmoja wa wshiriki wa semina ya watumiaji wa huduma za mawasiliano, Selina Wilson, baada ya kujibu swali vizuri, katika semina hiyo, iliyofanyika leo katika hoteli ya Njuweni, Kibaha mkoa wa Pwani.
Wakati Selina akiruka na Nokia, mwingine akajipatia Nokia 'Blackbarry'
washiriki

Washiriki
Yussuf Said Mfinanga, almaarufu, Mzee Njuweni (kushoto), akimsalimia Sheikh wa wilaya ya Kibaha mjini nje ya ukumbi wa semina hiyo.

DK SHEIN AKABIDHIWA CHETI CHA KUSHINDA URAIS KATIKA UCHAGUZI MKUU ULIOPITA

RAIS  wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Sheni,akipokea hati ya uthibitisho ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar , na Cheti cha ushiriki  mgombea urais huo, katika uchaguzi mkuu uliopita, kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi  Zanzibar, Said Bakari Jecha. Ikulu mjini Zanzibar, leo.(Picha na Ikuklu, Zanzibar).

JK AZURU WIZARA YA UJENZI LEO

Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na baadhi ya wafanyakazi wa wizara ya Uchukuzi muda mfupi baada ya kuwasili katika makao makuu ya wizara hiyo jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi ambapo alizungumza na uongozi pamoja na wafanyakazi .
Rais Kikwete akiwaaga wafanyakazi hao baada ya kuzungumza na viongozi kwenye wizara hiyo

PROF MWANDOSYA ATEMBELEA TBL MWANZA

Waziri wa Majii, Profesa Mark Mwandosya (kulia) Meneja wa Kiwanda cha TBL Mwanza, Richmond Raymond (kushoto) pamoja na Meneja Ubora wa Bidhaa wa kiwanda hicho, Caroline Nhonoli (katikati) alipotembelea hivi karibuni kiwanda hicho kuona uzalishaji wa bia na juhudi mbalimbali za utunzaji na udhibiti wa matumizi ya maji ambayo ni muhimu kwa maisha ya kila siku ya Watu. Ziara hiyo ilikuwa ni moja ya shamrashamra za maadhimisho ya Wiki ya Maji iliyofikia kilele juzi jijini Mwanza.5289
Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya (kulia) akitembelea Kiwanda cha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) cha Mwanza, alipofanya ziara hivi karibuni katika kiwanda hicho kuona uzalishaji wa bia na juhudi mbalimbali za utunzaji na udhibiti wa matumizi ya maji ambayo ni muhimu kwa maisha ya kila siku ya Watu. Ziara hiyo ilikuwa ni moja ya shamrashamra za maadhimisho ya Wiki ya Maji iliyofikia kilele juzi jijini Mwanza.
Meneja wa Kiwanda cha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) Mwanza, Richmond Raymond (mbele kushoto) akimuongoza Waziri wa Majii, Profesa Mark Mwandosya kutembelea mradi wa maji alipofanya ziara hivi karibuni kiwandani hapo, kujionea utendaji wa kiwanda hicho pamoja na mradi huo wa maji unaowahudumia bure wananchi wanaoishi karibu na kiwanda hicho. Ziara hiyo ilikuwa ni moja ya shamrashamra za maadhimisho ya Wiki ya Maji iliyofikia kilele juzi jijini Mwanza..(Picha zote na Mpigapicha maalum)

MAJERUHI WA FIVE STARS TAARAB WAFIKA DAR

Mar 22, 2011

Baadhi ya majeruhi wa Kundi la Muziki wa Taarab la Five Stars, wakiwa eneo la Equator Grill, Mtoni kwa Azizi Ally, Temeke Dar es Salaam, leo mchana baada ya kufikishwa wakitokea hospitali kuu ya mkoa wa Morogoro. Equator Grill ndiyo ngome kuu ya kundi hilo. (Picha kutoka Isaamichuzi Blog)
============================
Kutoka Morogoro
Picha ya chini ni Mwanamuziki maarufu na mkongwe wa muziki wa taarab, Mwanahawa Ali wa kundio hilo,  akiwa katika hospitali ya mkoa wa Morogoro leo asubuhi baada ya kupatiwa matibabu kutokana na majeraha aliyopata katika ajali ya gari walilokuwa wakisafiria na wasanii wenzake wa Kundi la muziki wa taarab la Five Stars, eneo la Doma, Mikumu nje kidogo ya mji wa Morogoro ambapo wanamuziki 13 waliokuwa katika gari hilo wamekufa papo hapo. (Picha kwa hisani ya mdau wa Morogoro).


JK ATEMBELEA WIZARA YA UTUMISHI WA UMMA

Msafara wa Rais Jakaya Kikwete ukiingia katika eneo la Ofisi ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, leo 
Rais Kikwete akimsalimia Katibu Mkuu wa wizara hiyo, George Yambesi. Katikati ni Waziri wa wizara hiyo, Hawa Ghasia na Kaimu Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadick 
Rais Kikwete akimhoji jambo na kutaka ufafanuzi wa kina kwa Waziri Ghasia (aliyesimama) , wakati akipokea taarifa kutoka kwa waziri huyo. Kushoto ni Yembesi. 
Wafanyakazi wa wizara hiyo wakimsalimia kwa hamu, Rais Kikwete kabla ya kuondoka wizarani hapo.

MSIBA WA KUFARIKI KWA AJALI WASANII WA FIVE STARS; SERIKALI YATOA TAMKO

ยช