Breaking News

Your Ad Spot

Oct 6, 2014

ZITTO KABWE AZIDI KUNG'ARA BARANI AFRIKA

Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, akizungumza na mmoja wa wakulima wa kahawa wilayani Kigoma Vijijini katika mojawapo ya ziara zake za kuhamasisha kilimo na kuhimiza wakulima kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. 
.............................................................................................................................................................................
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ameibuka mwanasiasa wa kwanza barani Afrika kutwaa Tuzo ya Mtetezi wa Haki ya Hifadhi ya Jamii, imefahamika.
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki na Umoja wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya Nchi za Afrika Mashariki na Kati (ECASSA), Zitto anatarajiwa kukabidhiwa tuzo yake hiyo katika sherehe rasmi iliyopangwa kufanyika Oktoba 30 na 31 mwaka huu katika mji wa Livingstone nchini Zambia.
 
“Tuzo hii imetolewa kwako kwa kuzingatia mchango wako mkubwa unaoutoa kuhakikisha sehemu kubwa ya Watanzania ambao walikuwa hawanufaiki na mifuko hii wanafaidika nayo.
 
“ECASSA, mahususi kabisa, imevutiwa sana na jitihada zako za kuhakikisha kwamba wasanii wananufaika na mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na wakulima kupitia chama chao cha ushirika cha Rumako kilichopo Kigoma Vijijini,” ilisema sehemu ya barua ya umoja huo kwa Zitto ambayo gazeti hili imefanikiwa kupata nakala yake.
 
RUMAKO ni Ushirika wa Msingi wa Vijiji vya Mkabogo, Rusaba na Matyazo wilayani Kigoma Vijijini ambako zaidi ya wakulima wake 750 wameingia kuwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
 
Kwa takribani miaka minne sasa, Zitto amekuwa akipigania wakulima wa Tanzania kupewa uanachama wa wa mifuko hiyo ili kuwakwamua kiuchumi na pia kuwawezesha kupata huduma ya hifadhi kama ilivyo kwa wafanyakazi katika sekta rasmi wanaopata huduma hizo.
 
Baada ya wakulima hao wa Kigoma, kumekuwepo na wimbi la vyama vingi vya wakulima katika maeneo mbalimbali nchini kutaka kuingia katika mifuko hiyo na ECASSA inaamini kwamba Zitto ana mchango mkubwa katika hilo.
 
Akizungumzia tuzo hiyo, Zitto alisema, " nimeipokea tuzo hii kwa unyenyekevu mkubwa. Naamini kuwa siku za usoni haki ya Hifadhi ya jamii kwa wananchi itakuwa ni haki ya kikatiba. Nchi masikini zinapaswa kuongeza uwekaji akiba ili ziweze kuendelea kwa kasi.
 
Bila akiba uwekezaji unakuwa mdogo na hatimaye uchumi haukui. Hifadhi ya jamii ni moja ya njia mwafaka kabisa ya kukuza uwekaji akiba katika nchi kwani wanachama wanafaidika na mafao ya muda mrefu kama pensheni na yale ya muda mfupi kama Bima ya Afya na mikopo kupitia saccos".
 
Azimio la kutolewa kwa tuzo hiyo lilitokana na Mkutano Mkuu wa Sita wa ECASSA uliofanyika jijini Kampala, Uganda miaka miwili iliyopita, ambapo wakuu wa mifuko hiyo walikubaliana iwepo ili kuchochea wanasiasa kuhamasisha wananchi kuelewa umuhimu wa Hifadhi ya Jamii.
  
ECASSA ni umoja unaounganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii takribani 20 katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Zambia

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages