Morocco imesema kuwa imefanikiwa kuzima shambulio la kemikali
lililokuwa limepangwa kufanywa na mtandao mmoja wa kigaidi unaohusishwa
na kundi la kitakfiri la Daesh.
Abdelhak Khiame, Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi nchini humo,
leo Jumapili amesema kuwa, vyombo vya usalama vya nchi hiyo vimekamata
makopo yaliyokuwa na kemikali ya sumu aina ya salfa, wakati wa
operesheni yao kwenye ngome za magaidi hao katika miji mbalimbali.
Amesema, magaidi hao wanaoaminika kuwa na mafungamano na Daesh
hawakupokea mafunzo kutoka kambi za kundi hilo nchini Iraq ama Syria,
lakini wamekuwa wakipokea mafunzo na ufadhili kutoka kwa Daesh kupitia
njia zisizo za moja kwa moja. Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa
Morocco amesema silaha walizozikamata wakati wa operesheni hiyo zinatoka
Libya. Miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa katika msako huo ni kijana
mmoja wa miaka 16 ambaye alikuwa amefundishwa namna ya kuripua magari
kwa bomu.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi za Morocco, raia zaidi ya 1,300 wa nchi
hiyo ya magharibi mwa Afrika wamejiunga na Daesh kufikia sasa na kwamba
246 kati yao wamekwishauawa nchini Syria na wengine 40 nchini Iraq.
Imearifiwa kuwa 156 kati ya magaidi hao ambao walikuwa wameenda Syria na
Iraq, wamefanikiwa kurejea nchini humo kwa lengo la kufanya mashambulio
mbalimbali.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269