Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tanzania (TAMWA) kimesema wanawake waliogombea nafasi
mbalimbali kwenye Uchaguzi Mkuu 2015 walikosa nafasi ya kutosha
kuzungumza kwenye vyombo vya habari. Alisema utafiti mdogo walioufanya
katika vyombo vya habari kadhaa ulibaini kuwa ni asilimia 11 tu ya
wanawake wagombea ndio walipata nafasi ya kuandikwa katika magazeti
wakati wa uchaguzi huo.
Takwimu hizo zilitolewa jana
katika semina ya wadau wa vyombo vya habari pamoja na baadhi ya wagombea
na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Edda Sanga alipokuwa akifungua semina
hiyo ambayo pia ilishirikisha wahariri kutoka vyombo anuai vya habari
nchini Tanzania.
Alisema katika utafiti huo
uliofanywa kwa miezi miwili yaani Septemba na Oktoba 2016 kwenye
magazeti sita ulibaini kati ya vyanzo vya habari 2577 vilivyotumika
kwenye habari za Uchaguzi Mkuu, wanaume waliotumika kama vyanzo walikuwa
2256 ikiwa ni sawa na asilimia 88 huku wanawake 303 kama vyanzo hii
ikiwa ni asilimia 11 tu.
Mkurugenzi huyo Mtendaji wa TAMWA
alisema utafiti pia uliainisha kuwa wanaume waliongoza katika makundi
yote ya mada za habari hata zile ambazo hazikuwa zikihusiana na uchaguzi
huo. Aliongeza kuwa katika utafiti huo ilikuwa ni nadra sana kupata
habari ambazo zipo katika kurasa za mbele huku vyanzo vyake vikiwa
vimetokana na wanawake. Habari za wanawake zilianza kujitokeza kuanzia
kurasa za nne na kuendelea.
“…Kwa mujibu wa matokeo ya
ufuatiliaji wa habari za magazeti, wanawake kwa ujumla waliogombea na
wasiogombea kote nchini walikabiliwa na unyanyasaji kama vile kufanyiwa
ghasia, na vitisho wakati wa kampeni na siku ya uchaguzi. Pia wanaume
walificha kadi za kupigia kura za wanawake zao, wanaume waliwalazimisha
wake zao kuwapigia kura wagombea ambao wanawataka hata kama mwanamke
hamtaki, utumiaji wa lugha ya matusi dhidi ya wagombea wanawake na
wakati wa kampeni kuna baadhi ya wagombea wanawake walikamatwa na
kutishiwa kwa tuhuma za kutotii amri ya Jeshi la Polisi,” alisema Sanga
katika taarifa yake akifungua semina hiyo.
Wanahabari waliminya sauti za wanawake Uchaguzi Mkuu – Utafiti
Kwa upande wao wanawake
waliogombea wakizungumza katika semina hiyo walisema vyombo vya habari
kiujumla havikutoa nafasi sawa kwa wagombea hasa wanawake na vingi
vilikimbilia kutoa habari za wagombea wenye majina na maarufu kwa
wanajamii. Bi. Stella Jairos ambaye aligombea Ubunge Vitimaalum Chama
Cha Mapinduzi (CCM) Dodoma alisema wanawake walemavu mbali na kukosa
fursa kwenye vyombo vya habari walikabiliwa na changamoto mbalimbali
zilizofifisha mafanikio katika kinyang’anyiro cha uchaguzi huo.
Naye Loyce Kibona aliyegombea
upande wa vyama vya upinzani katika uchaguzi huo alisema licha ya vyombo
vya habari kuwa ni changamoto kwao kupata nafasi ya kusikika bado hali
ya kujiamini kwa wanawake na kukatishana tamaa kunaendelewa kukwamisha
mafanikio ya kundi hilo hivyo kuwataka wanawake kuungana mkono.
Imeandaliwa: www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269