Breaking News

Your Ad Spot

Mar 22, 2016

‘MABASI YAENDAYO KASI KUANZA NDANI YA WIKI HII’

JILWAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mabasi yaendayo kasi (DART) yataanza kufanyiwa majaribio ndani wiki moja kuanzia sasa ili madereva waanze kuzoea njia na taa za kuongozea magari.
“Wataanza na mabasi kati ya 30 – 50 ambayo yatapita kwenye njia zote za mradi huo. Zoezi hilo litafanyika ili watumiaji wengine wakiwemo waendesha daladala, bodaboda na watembea kwa miguu waweze kutambua kuwa njia ya mabasi yaendayo kasi si ya kwao, hivyo waanze kuzoea,” alisema.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Machi 22, 2016) wakati alipofanya ziara ya ghafla katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri iliyokuwa na lengo la kuangalia mfumo wa majiko ya gesi sokoni hapo na kukagua ujenzi wa ukuta unaotenganisha soko hilo na mabasi yaendayo kasi.
Waziri Mkuu ambaye ametembelea soko hilo kuanzia saa 5:10 hadi saa 5:54, alitoa jibu hilo wakati akijibu maombi ya mfanyabiashara mmoja, Bw. Sharifu Ramadhani ambaye alisema wanatumia fedha nyingi kwa ajili ya usafiri kwa vile mabasi mengi yanaishia Mnazi Mmoja. “Mabasi yanaishia Mnazi Mmoja na huku ni mbali kwa hiyo tunalazimika kutembea kwa miguu kwa sababu kukodi taxi ni gharama kubwa,” alisema.
Akifafanua kuhusu hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa mradi huo, Waziri Mkuu alisema: “Hivi sasa wanakamilisha ufungaji wa mitambo ya kukatia tiketi ambapo abiria atakuwa na kadi kama za benki ambayo anaijaza fedha halafu anapita kwenye mashine, kiasi cha nauli kinakatwa halafu anaingia kwenye basi, hakutakuwa na muda wa kukata tiketi.”
Alisema tatizo la usafiri kwa wafanyabiasha wa feri litakwisha hivi karibuni baada ya mabasi hayo kuanza.
IMETOLEWA NA: OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
  1. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, MACHI 22, 2016.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages