Breaking News

Your Ad Spot

Jul 10, 2016

TANZANIA NA INDIA ZASAINI LEO MIKATABA YA MIRADI YA MAENDELEO

Na Immaculate Makilika- MAELEZO
Serikali ya India na Tanzania zimesaini mikataba ya miradi ya maendeleo katika sekta za maji, kilimo, viwanda, teknolojia ya habari na mawasiliano na afya katika kuimarisha mahusiano ya nchi hizo mbili ili kusaidia wananchi wake.

Mikataba hiyo imesainiwa leo, wakati Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi alipokuakifanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mikataba wa kwanza uliosainiwa inahusisha mradi wa kusambaza maji katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

Aidha, mkataba wa pili unahusisha mradi wa kusambaza maji Zanzibar ambao unatarajiwa kugharimu dola  za kimarekani milioni 92 ambapo mradi huo unatarajiwa kufikia miji 17 nchini na mkataba mwingine utahusisha mafunzo ya ufundi yatakayosaidia kuzalisha wataalamu mbalimbali.

“Lengo letu ni kusaidiana  na kuimarisha mahusianao yetu katika kukuza uchumi na kutengeneza fursa mpya za ajira kwa wananchi wetu” alisema Waziri Modi.

Waziri Modi aliongeza kuwa Serikali ya India itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa biashara na hatimaye kukuza uchumi wa nchi hizo.

Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alisema Serikali India imekua na ushirikiano mzuri na Tanzania hasa katika masuala ya maendeleo ambapo imeweza kuwekeza nchini kiasi shilingi za Kimarekani dola bilioni 2.4 na kuzalisha  ajira 54,176.

Baadhi ya misaada iliyotolewa na Serikali ya India ni pamoja na  mashine ya vipimo vya ugonjwa wa kansa katika hospitali ya Bugando, itakayosaidia wakazi wa kanda ya ziwa na nchi nzima kwa ujumla pamoja na kuongeza na kuimarisha ushirikiano kati ya Shirika la viwanda vidogo vigodo la India kushirikiana na Tanzania katika kukuza viwanda vidogo na vya kati nchini.

Katika masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano, Serikali hiyo imeahidi kuleta wataalamu wao nchini Tanzania kwa lengo la kutengeneza program mbalimbali ili kuisaidia Tanzania katika masuala ya ulinzi wa mitandao pamoja na kutengeneza namna bora za ukusanyaji wa mapato ya nchi.

Katika masuala ya viwanda, Serikali ya India imeahidi kuanzisha viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu  zitakazotibu  magonjwa mbalimbali ikiwemo malaria, figo na kisukari, ikiwa ni pamoja na kutengeneza vifaa tiba vitakavyotumika katika hospitali mbalimbali nchini kwa lengo la kupunguza gharama ya kununua vifaa hivyo nje ya nchi.

Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa nchi ya India ina uhitaji mkubwa wa mazao ya kilimo hasa jamii ya kunde hivyo akawataka wakulima kutumia fursa hiyo kuzalisha mazao hayo kwa wingi.

“India inauhitaji wa tani 200 za mazao jamii ya kunde, wakulima mnatakiwa kuzalisha mazao hayo kwa wingi kwa vile tayari kuna soko la uhakika, na tutahakikisha madalali hawatakuwepo ili mkulima asikandamizwe” alisema Rais Magufuli.

Katika sekta ya uwekezaji nchini, India ni nchi ya tatu kwa uwekezaji Tanzania ikifuatiwa na Uingereza pamoja na China.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages