.

KIONGOZI WA WAASI WA ZAMANI WA CONGO ATOWEKA KAMBINI

Nov 14, 2016

Ostkongo Goma Rebellenf├╝hrer Makenga (Simone Schlindwein)
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imeimarisha doria zake mipakani baada ya kiongozi wa kijeshi wa zamani wa kundi la waasi la M23 kutoweka kwenye kambi iliowakusanya wapiganaji wa zamani katika nchi jirani ya Uganda.
Julien Paluku gavana wa jimbo la Kivu Kaskazini nchini Congo amesema maafisa wa serikali wa Uganda hawajuwi mahala alipo Sultani Makenga ambaye alikuwa kiongozi wa kijeshi wa kundi la waasi la M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Paluku ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters hapo Jumamosi kwamba wamekuwa na mawasiliano na idara ya ujasusi ya Uganda ambao wamethibitisha kwamba kanali huyo wa zamani huenda ametoroka tokea Ijumaa na majasusi wa Uganda wanashindwa kujuwa mahala alipo.
Afisa wa kitengo cha kisiasa wa kundi la M23 amekataa kuzumgumzia juu ya kadhia hiyo kwa kusema kwamba masuala kuhusu Makenga waulizwe maafisa wa Uganda. Msemaji wa jeshi la Uganda amesema hajuwi iwapo Makenga ametoweka lakini atafuatilia kujuwa mahala alipo.
Milio ya risasi yahanikiza Bunagama
Afisa wa forodha wa Congo katika mji wa Bunagama amesema milio ya risasi ilisikika wakati wa usiku katika milima inayouzunguka mji huo ambacho ni kituo muhimu cha kuvuka mpaka kuingia Uganda na ilikuwa ngome ya kundi la M23.Milio ya risasi iliendelea kusikika hadi Jumamosi asubuhi.
Afisa huyo amesema hawajuwi milio hiyo ya risasi ilikuwa ikitokea wapi na hawajui nini kinachotokea kutokana na kwamba jeshi haliwaambii kitu chochote.Afisa huyo aliyekataa kutajwa jina kutokana na kutoruhusiwa kuzungumza na vyombo vya habari amesema harakati za kijeshi zimeongezeka katika mji huo wa Bunagana halikadhalika uwepo wa kijeshi wa wanajeshi wa Uganda upande wa pili wa mpaka katika mji wa Kisoro.
Paluku amesema hakuna uthibitisho kwamba Makenga amerudi Congo lakini kumekuwepo na repoti ya kuwepo kwa vikosi visivyojulikana katika Mbuga ya taifa ya Sarambwe inayopakana na mpaka.Gavana huyo amesema "Kuna hali kubwa ya tahadhari.Vikosi vyetu viko katika doria ya mapambano ili kwamba jambo hilo ikiwa ni la kweli waweze kumdhibiti Makenga na washirika wake anaoandamana nao."
Hadi kushindwa kwake hapo mwaka 2013 kundi la M23 lilikuwa na nguvu kubwa kabisa miongoni mwa makundi kadhaa ya wapiganaji ambayo yalikuwa yakiendelea kudhibiti maeneo makubwa yenye utajiri wa madini ya mashariki mwa Congo licha ya kumalizika kwa vita vya mwaka 1998-2003.
Uvumi kuungana upya wapiganaji wa M23
Eneo hilo linaendelea kuwa hatari kutokana na mgawanyiko wa kikabila na kisiasa.Wakati ilipofikia kilele cha umashuhuri wake kundi hilo la M23 liliuteka mji mkuu wa Kivu ya Kaskazini wa Goma lakini kufuatia kushindwa kwake na majeshi ya Umoja wa Mataifa na yale ya Congo wapiganaji wake wengi walikimbilia Uganda na Rwanda. Tokea wakati huo wamekuwa wakiishi katika makambi yanayosimamiwa na wanajeshi wakisubiri misamaha walioahidiwa chini ya makubaliano ya amani.
Hao mwaka 2014 Uganda ilisema ilikuwa ikiwahifadhi wapiganaji wa zamani wa kundi hilo 1,430. Hata hivyo wengi wao tayari wameondoka kwenye makambi hayo na uvumi umekuwa ukizidi kuhanikiza kwamba waasi hao wanajiandaa kuungana tena.
Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamesema kundi hilo linalotuhumiwa kwa uhalifu wa kivita na mashirika ya kutetea haki za binaadamu linaungwa mkono na Rwanda madai ambayo serikali ya nchi hiyo imekuwa ikiyakanusha mara kwa mara. DW

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª