Rais Hassan Sheikh Mohamoud wa Somalia
ameitaka jamii ya kimataifa kutuma misaada ya dharura katika maeneo
yanayokabiliwa na ukame na baa la njaa nchini humo.
Rais huyo amewataka Wasomali waishio nje ya nchi kuwajali ndugu
zao wanaokabiliwa na njaa na kiu kutokana na ukame unaoitafuna nchi
hiyo ya Pembe ya Afrika.
Rais wa Somalia amesema msimu wa masika umepita pasina kushuhudiwa
mvua zozote nchini humo, hivyo maeneo mengi yanakabiliwa na ukame.
Ameitaka jamii ya kimataifa kuingilia kati na kutuma misaada ya dharura
katika maeneo hayo kabla hali haijawa mbaya zaidi.
Mwanzoni mwa mwaka huu, wataalamu walionya kwamba mwaka huu wa 2016
utashuhudia ukame katika baadhi ya nchi za Afrika hususan eneo la Pembe
ya Afrika. Taathira hasi za El-Nino sambamba na ukame na mafuriko
katika nchi za Somalia na Ethiopia zimeyaweka hatarini maisha ya watu
wengi wa nchi hizo.
Ofisi ya Uratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa mwezi
Septemba mwaka huu ilisema kuwa, uhaba wa maji katika nchi za Somalia na
Ethiopia umesababisha karibu watoto milioni tatu kukumbwa na hatari ya
utapiamlo, huku karibu raia milioni tano wa Somalia wakihitaji misaada
ya chakula.
Mbali na majanga hayo ya kimaumbile, Somalia inakabiliwa na harakati
za kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab ambalo limekuwa
likitekeleza mashambulizi ya kigaidi kila leo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269