Ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa
rais nchini Marekani umezusha wimbi na wasiwasi mkubwa na hali ya
kutokuwa na imani kuhusu siasa za kigeni za kiongozi huyo mkabala wa
nchi za Afrika.
Mkurugenzi wa Kituo cha Habari cha Cape Town nchini Afrika
Kusini, Rayan Cummings anaamini kuwa, kushika madaraka kwa Trump huko
Marekani kunazua maswali mengi kuhusu mabadiliko ya siasa za nje za nchi
hiyo katika masuala ya kupambana na ugaidi, biashara, misaada ya
kifedha na makubaliano ya kimataifa ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Japokuwa katika kampeni zake za uchaguzi Donald Trump hakugusia moja
kwa moja suala la uhusiano wa siku zijazo kati ya Marekani na nchi za
bara la Afrika, lakini swali linajitokeza kwamba, je, sisitizo lake la
kupambana na ugaidi lina maana ya kushirikiana na nchi kama Nigeria na
Kenya kwa ajili ya kuyaangamiza makundi ya Boko Haram na al Shabab?
Rayan Cummings anaamini kuwa, iwapo tutayazingatia matamshi ya Trump
katika kampeni za uchaguzi kuwa ndiyo dira ya sera na siasa za serikali
yake, basi ni wazi kuwa rais mteule wa Marekani anaamini sana suala la
kutumia mabavu na nguvu za kijeshi.
Kwa sasa Marekani imetuma majeshi katika nchi za Afrika kama wale
waliotumwa Uganda kwa kile kinachosemekana ni kuisaidia serikali ya
Kampala kupambana na waasi wa kundi la Lord's Resistance Army (LRA).
Maafisa wa serikali ya Marekani wanaunga mkono suala la kutuma majeshi
ya nchi hiyo barani Afrika; hata hivyo askari hao wanatumiwa kama wenzo
wa kuingilia masuala ya ndani ya nchi za bara hilo. Suala hilo
linaonekana wazi kwa kutilia maanani kwamba, nchi zinazolengwa zaidi
barani Afrika ni zile zenye utajiri mkubwa wa maliasili kama almasi,
dhahabu, urani na kadhalika.
Kwa sasa wengi wanauliza kwamba, Donald Trump ambaye katika kampeni
zake za uchaguzi alijikita zaidi katika matatizo ya ndani ya wananchi wa
Marekani ataendeleza siasa na sera hizo baada ya kuapishwa rasmi na
kushika hatamu za uongozi au la? Wachambuzi wa mambo wanasema, sisitizo
la Trump na kujiepusha na siasa za kuingilia masuala ya ndani ya nchi
kama Iraq na Syria lina maana ya Marekani kujitenga na masuala mengi ya
kimataifa katika kipindi cha miaka minne ijayo. Wanasisitiza kuwa, iwapo
hali itakuwa hivyo kutajitokeza mgongano wa kustaajabisha kati ya siasa
za rais mteule wa Marekani na wanadharia wa siasa za kigeni mjini
Washington hasa juu ya suala la kutuma majeshi ya nchi hiyo katika nchi
zenye utajiri na maliasili nyingi kama zile za Afrika.
Wakati huo huo misimamo mikali ya Trump kuhusu majukumu ya Marekani
mkabala wa mkataba wa hali ya hewa wa Paris, inatia wasiwasi. Trump
amekuwa akipinga vikali mkataba huo. Katika upande wa pili wasomi
wanasema kuwa, bara la Afrika ndilo linalopatwa na madhara makubwa zaidi
yanayosababishwa na mabadiliko ya hali hewa kuliko maeneo mengine ya
dunia. Mkataba wa Paris unasisitiza kuwa, nchi za Afrika zinapaswa
kupata misaada ya kifedha kutoka kwa Marekani na nchi nyingine
zilizostawi ili kufidia madhara yanayosababishwa na nchi hizo kwa
mazingira ya dunia.
Donald Trump anaamini kuwa, mikataba ya kibiashara na uwekezaji wa
moja kwa moja wa Wamarekani barani Afrika unasababisha kukosa ajira na
kazi raia wengi wa Marekani. Hapa linakuja swali kwamba, vipi kiongozi
mwenye mitazamo kama hiyo ataruhusu wamiliki wa viwanda, wafanyabiashara
na matajiri wa Marekani kuwekeza barani Afrika na kutayarisha kazi na
ajira kwa Waafrika maskini? Kwa msingi huo inatabiriwa kuwa, katika
kipindi cha utawala wa Trump kutashuhudiwa kupungua sana kwa misaada ya
kifedha ya Marekani kwa nchi za Afrika.
Viongozi wa nchi za Afrika pia wana wasiwasi kwamba, katika kipindi
cha utawala wa Trump, yumkini Marekani ukakiuka au kutengua Mkataba
wa Biashara kati ya Mataifa ya Afrika na Amerika wa AGOA. Kwa mujibu wa
mkataba huo nchi 39 za Afrika zinaweza kupeleka bidhaa zao za kilimo na
kuziuza Marekani bila ya kulipa ushuru, ingawa baadhi ya viongozi wa
Afrika kwa upande wao wamekuwa wakilalamika kuwa mkataba wa biashara
huru wa AGOA unaifaidisha zaidi Marekani.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269