.

KAMANDA SIRRO: VITENDO VYA UBAKAJI NA ULAWITI VYAONGEZEKA JIJINI DAR ES SALAAM

Dec 31, 2016

1
Kamishna wa Kanda Maalum  ya Polisi mkoa wa Dar es salaam CP Saimon Sirro amesema matukio ya Ubakaji na Ulawiti yameongezeka kwa kiwango kikubwa katika mwaka wa 2016 ukilinganisha na mwaka 2015 kutokana na matukio yaliyolipotiwa kiwa kipindi cha mwaka mzima.

Amesema hii inatokana na kuanzishwa kwa Dawati la Jinsia na pia wananchi kupata uelewa na kuripoti matukio hayo kila yanapotokea hii ndiyo sababu kubwa inayofanya kuongezeka kwa matukio hayo katika mkoa wa Dar es salaam.

Kamishna Saimon Sirro akizungumza katika Kituo Kikuu cha Polisi Kati jijini Dar es salaam ametoa  taarifa hiyo wakati  akielezea takwimu za matukio mbalimbali yaliyotokea kwa mwaka 2016.

Kamishna wa Kanda Maalum  ya Polisi mkoa wa Dar es salaam CP Saimon Sirro amesema  mwaka 2015 vitendo vya ubakaji vilivyoripotiwa vilikuwa 972 wakati mwaka  2016 vitendo vya kubaka vilivyoripotiwa vilikuwa 1030 ambapo ongezeko lilikuwa ni asilimia 58 ukilinganisha na matukio hayo kwa mwaka 2015.

Akitoa takwimu za vitendo vya kulawiti kwa mwaka 2015 amesema vitendo vya ulawiti vilivyoripotiwa ni 3010 ambapo  mwaka 2016 vitendo hivyo viliripotiwa kwa matukio 383 sawa na asilimia 73.

Amewataka wananchi kuacha matendo maovu kwani hayatawafikisha popote zaidi ya kuishia katika mikono ya sheria na kutupwa jela.

VIONGOZI WA CLUB YA WAANDISHI SHINYANGA WAKUTANA NA DC KAHAMA, KUHUSU MWANDISHI ALIYEFIKISHWA MAHAKAMANI

UONGOZI wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Shinyanga (SPC), na baadhi ya waandishi wa habari wilayani Kahama, wakiwa Ofisini kwa Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu kupata muafaka kufuatia kukamatwa na kufikishwa mahakamani mwandishi wa habari wa kujitegemea Paul Kayanda.

MAJALIWA ACHANGISHA FEDHA ZA UJENZI WA SEKONDARI MPYA RUANGWA, CCM LINDI WAMPA TUZO KUTAMBUA MCHANGO WAKE

 Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea cheti maalum cha kutambua mchango wake katika kukijenga na kukiimarisha Chama cha Mapinduzi wilayani Ruangwa kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Lindi, Ali Mtopa katika mkutano wa hadahara aliouhutubia mjini Ruangwa Desemba 30, 2016.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha Cheti Maalum  cha kutambua mchango wake katika kukijenga na kukiimarisha Chama cha Mapinduzi wilayani Ruangwa alichokabidhiwa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Lindi, Ali Topa   (kulia) katika mkutano wa hadhara aliouutubia mjini Ruangwa Desemba 30, 2016. Kushoto ni Katibu wa CCM wa wilaya ya Ruangwam Issa Njinjo.
 Wananchi wa Ruangwa wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia mkutano wa hadhara mjini Ruangwa, Desemba 30, 2016. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya Shilingi milioni sita kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya Pacco GEMS Limited, Bw. Mahendra Bardiya katika harambee  ya kuchangia ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari wilayani Ruangwa ambapo jumla ya shilingi milioni 138.26 zilichangwa. Harambee hiyo ilifanyika sambamba na  mkutano wa hadhara uliohutubia wa Waziri Mkuu mjini Ruangwa, Desemba 30, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya Shilingi milioni sita kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya Pacco GEMS Limited, Mahendra Bardiya katika harambee  ya kuchangia ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari wilayani Ruangwa ambapo jumla ya shilingi milioni 138.26 zilichangwa. Harambee hiyo ilifanyika sambamba na  mkutano wa hadhara uliohutubia wa Waziri Mkuu mjini Ruangwa, Desemba 30, 2016. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

WAKAZI WA MJI WA LINDI WAFANYA USAFI LEO KUITIKA MWITO WA RAIS DK. MAGUFULI


Wakazi wa mji wa Lindi wakifanya usafi wa mazingira katika mitaa na barabara  zinazozunguka hospitali ya mkoa huo Desemba 31, 2016. Walifanya hivyo kuitikia agizo la  Rais John Pombe Mgufuli la kuwataka watanzania kutumia muda wa asubuhi kila Jumamosi kufanya usafi wa mazingira. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

BONDIA WA AUSTRALIA AWAPIGA JEKI MABONDIA WA TANZANAIA

Mwakilishi wa Kimweri Promotion Nchini Tanzania Yusuph Mnyeto kushoto akimkabidhi vifaa vya ndondi kwa kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D' baada ya kupokelewa na kukabidhiwa kwa wadau mbalimbali nchini vifaa hivyo vimetolewa na Bondia Mtanzania anaefanya shughuli zake nchini Ausralia.
PICHA ZAIDI/>BOFYA HAPA

HAKUNA UHABA WA DAWA YA KAPUTI HOSPITALI YA BOMBO

Na Frank Mvungi- MAELEZO
Serikali Iimesema hakuna uhaba wa dawa ya usingizi katika Hospitali ya Rufaa Bombo mkoani Tanga kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini kuwa hali hiyo inachochea kuzorota kwa huduma za upasuaji.

Akifafanua suala hilo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga  Dkt. Asha Mahita amesema kuwa taarifa kuwa huduma za upasuaji katika hosipitali hiyo zimesimama si za kweli na ukweli ni kwamba huduma zinaendelea kama kawaida.

“Huduma za upasuaji katika Hosipitali yetu zinaendelea kama kawaida na hakuna tatizo kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari” Alisisitiza Dkt. Mahita.

Akifafanua zaidi Dkt. Mahita alisema kuna mgonjwa mmoja tu ambaye upasuaji wake ulisogezwa mbele kutokana na sababu za kitabibu na si kwa sababu ya kukosekana kwa dawa ya usingizi.

Aliongeza kuwa sababu zinazoweza kusababisha kuahirishwa kwa upasuaji wa mgonjwa aliye kwenye ratiba ni pamoja na uwepo wa wagonjwa wengi wa dharura hali inayoweza kuchangia nguvu kubwa kuelekezwa katika kuhudumia wagonjwa hao wakiwemo wahanga wa ajali.

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kuwahudumia wananchi na kuhakikisha kuna dawa za kutosha na vifaa tiba katika hospitali na vituo vya kutolea huduma hapa nchini.

RAIS WA ZANZIBAR DK. SHEIN ATOA SALAM ZA MWAKA MPYA WA 2017

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alipokuwa akitoa salamu za mwaka mpya wa 2017 kwa Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, ambapo ameuombea kuwa mwaka wa mafanikio na Amani. Salamu hizo alizotoa leo Desemba 31, 2016, katika  ukumbi wa Ikulu Mjini Unguja,(Picha na Ikulu.)

DONDOO ZA MAGAZETI YA LEO DESEMBA 31, 2016-TBC1

TANGAZO LA KIFO CHA MZEE OMULANGIRA CORNEL KAGOMBORA

kashaBw. Venanti Kagombora wa Bunju Dar es Salaam anasikitika kutangaza kifo cha baba yake mzazi Omulangira Cornel Kagombora, kilichotokea leo katika Hospitali ya Serikali ya Mkoa, mjini Bukoba. Habari ziwafikie watoto wake Verdiana Kagombora na Prosper Kagombora wa TEXAS Marekani, mkwe wa marehemu Bw. Justin Lambert wa Dar es Salaam na Father Mushuga wa Ibalaizibu Bukoba. Mazishi yafanyika Jumapili, tarehe 1 Januari, 2017 nyumbani kwake Katika kijiji cha Bulembo kitongoji cha Katoma Kamachumu, Kagera.

BURUNDI YATISHIA KUISHTAKI AU NA KUONDOA ASKARI WAKE SOMALIA


Burundi imetishia kuushataki Umoja wa Afrika-AU na wakati huohuo kutishia  kuwaondoa askari wake waliopo katika nchini ya Somalia ambao wanaohudumu chini ya mwavuli wa Kikosi cha Kulinda amani cha Umoja wa Afrika- Amisom.

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi amesema askari wa nchi hiyo wanaohudumu katika kikosi cha Amisom hawajalipwa mishahara na marupurupu yao kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa na ndipo serikali yake inataka kuwaondoa nchini Somalia, mbali na kuishtaki AU..Inaendelea>BOFYA HAPA

MAGAZETI YA LEO DESE 31, 2016WATU 13,626 WALIKAMATWA NA POLISI MA KUFIKISHWA MAHAKAMANI DAR KWA TUHUMA ZA UJAMBAZI NADAWA ZA KULEVYA

KIKOSI cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imekamata jumla ya watuhumiwa 13,626 na kuwafikisha mahakamani kwa tuhuma mbalimbali, ikiwemo dawa za kulevya na ujambazi wa kutumia silaha kwa kipindi cha mwaka mmoja wa 2016.

Aidha, hali ya uhalifu wa kutumia silaha katika jiji la Dar es Salaam umepungua, ukilinganisha na mwaka uliopita wa 2015 na matukio yanayoongezeka kwa wingi ni ya ubakaji na ulawiti.

Akitoa tathmini ya mwaka mmoja, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema jana kuwa matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha yamepungua kutoka 204 mwaka jana hadi 127 mwaka huu.

Idadi hiyo ni pungufu ya matukio 77, sawa na asilimia 37.7 huku matukio ya kutumia nguvu yamepungua kutoka 1,181 mwaka jana hadi 874 sawa na asilimia 26.

Kamishna Sirro alifafanua kuwa matukio ya mauaji, yamepungua kwa asilimia 11 ukilinganisha na mwaka jana, ambapo kulikuwa na jumla ya matukio 327 wakati kwa mwaka huu ni matukio 291 pungufu ya matukio 36.Alisema matukio ya ubakaji, yameongezeka kutoka 972 mwaka jana hadi 1030 mwaka huu, sawa na asilimia sita wakati matukio ya ulawiti yameongezeka kutoka 310 mwaka jana hadi 383 mwaka huu sawa na asilimia 23.5.

‘’Kwa matukio ya ubakaji yaliyoongezeka ni 58 na ulawiti matukio yaliyoongezeka ni 73. Lakini wizi wa watoto umepungua kutoka 26 mwaka jana hadi matukio 19 mwaka huu sawa na asilimia 27,’’ aliongeza.

Kwa mujibu wa Sirro, matukio ya uvunjaji yamepungua kwa asilimia 5.7 ambapo kwa mwaka jana kulikuwa na matukio 5,677 na mwaka huu matukio 5,355 sawa na upungufu wa matukio 322.Kwa upande wa wizi wa magari, umepungua kwa asilimia 18.1 kutoka matukio 392 hadi 321 mwaka huu huku wizi wa pikipiki ukipungua kutoka pikipiki 2,644 mwaka jana hadi 2,191 ambapo matukio 453 yamepungua sawa na asilimia 17.1.

Wizi wa mifugo umepungua kutoka 197 mwaka jana hadi 163 mwaka huu sawa na asilimia 17.3 ikiwa ni pungufu ya matukio 34.

“Sababu za kuongezeka au kupungua kwa matukio hayo kumetokana na juhudi za polisi wa kuzuia na kupambana na uhalifu kwa kufanya doria pamoja na misako mbalimbali iliyosaidia kukamatwa kwa wahalifu wa makosa mbalimbali pamoja na raia wema ambao wametoa taarifa za siri ili kugundua makosa hayo,’’ alieleza Sirro.

Akielezea watuhumiwa hao, Sirro alisema kuwa kati yao 52 walikutwa na silaha za kivita 67 na risasi 1,076, na watuhumiwa 126 walikutwa na dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 75 na gramu 254.

Pia alisema kuwa watuhumiwa 7,625 walikutwa na bangi kilo 2,843 na gramu 78 huku watuhumiwa 269 walikutwa na cocaine kilo tatu na gramu 255 na heroine kilo moja na gramu 654.

‘’Watuhumiwa 5,627 walikutwa na pombe haramu ya gongo lita 8,547 na mitambo 34 na tuliwafikisha mahakamani. Pia tumekamata wahamiaji haramu 105 kutoka mataifa mbalimbali ambao hawana kibali cha kuingia na kuishi nchini,’’ alisema Sirro.

Katika hatua nyingine, Sirro alisema kuwa jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watu wanne wakiwa na gari moja aina ya Noah lenye namba za usajili T 188 CZN rangi nyeupe ambalo liliibwa mkoani Kilimanjaro.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Erasto Edward (36), mkazi wa Kawawa Moshi, Wilson Kapori (37) mkazi wa Njia Panda Himo mkoani Kilimanjaro, Hussein Issah (32) mkazi wa Chanika na David Marwa mkazi wa Pugu Kajiungeni.


Watuhumiwa hao walikamatwa Desemba 21 mwaka huu, saa 5 asubuhi katika misako maeneo ya Tabata Bima. Watuhumiwa walitumia ufunguo bandia kuiba gari hiyo.

690 MBARONI KWA UHALIFU WA MTANDAO,WAMO MATAPELI,WEZI NA WAPORAJI WA SIMU ZA MKONONI


SERIKALI kupitia kitengo maalum cha uchunguzi wa jinai ya kimtandao, imefanikiwa kukamata watuhumiwa 690 kwa tuhuma za kufanya uhalifu wa mtandao.
Watuhumiwa hao ni matapeli, wezi, waporaji wa simu za mkononi na wengineo wanaotumia mfumo wa intaneti kuibia watu wasiokuwa na hatia.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Projestus Rwegasira alisema juzi jioni kuwa ofisi yake imekuwa ikikabiliana kikamilifu na wahalifu hao.
Alisitiza kwamba wahusika wote wa vitendo hivyo, watakamatwa. Meja Jenerali Rwegasira alikuwa akizungumza katika mahojiano katika kipindi cha Tunatekeleza, kinachorushwa na Televisheni ya Taifa(TBC). Kwamba wizara yake kwa kushirikiana na vyombo vya serikali, inaandaa mashtaka dhidi ya watuhumiwa waliokamatwa na watafikishwa mahakamani.
“Tunafanya kila juhudi kuzuia vitendo vya uhalifu wa kimtandao, tayari tumekamata baadhi ya watuhumiwa na watakabiliana na mkono wa sheria mahakamani,” alisema.
Alisema serikali imeunda kitengo maalumu chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, kukabiliana na udanganyifu na uhalifu wa kimtandao nchini na kimekuwa kikifanya kazi nzuri.
Rwegasira alisema, “Ningependa kuutangazia umma kuwa huru kutoa taarifa ya vitendo kama hivyo polisi mara wanapoona, tuna uwezo wa kufuatilia simu zilizoibwa na kuwakamata watuhumiwa”.
Mwezi Januari mwaka huu, Mkuu wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Veronica Sudayi alisema tangu kupitishwa kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao na Miamala ya Kielektroniki ya 2015 mwezi Septemba 2015, kiwango cha wizi na udanganyifu nchini, kimepungua kwa asilimia 60.
Sudayi alisema hayo wakati akizungumza na wafanyakazi na wanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kuhusu Sheria hiyo ya Makosa ya Mtandao. Kuhusu amani na usalama, katibu mkuu huyo alisema serikali imejiandaa vya kutosha kulinda watu na mali zao na kujipanga vya kutosha.
Alisema jeshi la polisi liliweza kukabiliana na changamoto za kiusalama katika mikoa ya Tanga na Mwanza baada ya watu wasiokuwa na hatia kuuawa na majambazi. Alisema katika tukio la Tanga, watuhumiwa 28 walikamatwa na wengine nane walikamatwa kuhusiana na tukio la Mwanza.

MAABARA YA KISASA YAZINDULIWA MASHARIKI YA KATI NA SHIRIKA LA NDEGE LA ETIHAD

Dec 30, 2016

SHIRIKA la Ndege la Etihad kupitia Kitengo chake cha Uhandisi (Etihad Airways Engineering) kwa kushirikiana na Lental Textiles AG wamezindua maabara ya kipekee ya kwanza Mashariki ya Kati kwa ajili ya wateja wa kanda hiyo walio sekta ya anga na waendeshaji mashirika ya uzalishaji na ubunifu.

Maabara hiyo ambayo ipo ndani ya kituo cha uhandisi cha Shirika la Ndege la Etihad karibu kabisa na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abu Dhabi itakuwa inatoa huduma mbalimbali ikiwemo vipimo vya kuwaka kwa moto, joto na moshi.

Aidha, maabara hiyo itaenda sambamba na hadhi ya ubora wa Kimataifa ISO 17025 na vipimo vyote vitafanyika kwa mujibu wa Kanuni za Anga za imataifa FAR/CS25.853.

Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi cha Shirika la Ndege la Etihad Jeff Wilkinson alisema, “Tunatoa huduma zilizotukuka kwenye matengenezo ya ndege na ufumbuzi wa kiuhandisi katika soko la anga duniani na kwa ajili ya aina zote za ndege za kibiashara.

“Kupitia ushirikiano wetu huu na Lantal, itakuwa rahisi sasa na haraka kwa kwa wateja wa sekta ya anga katika Ukanda kupata huduma bora za vipimo katika kituo chetu cha Abu Dhabi,” alisema.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Lantal, Dkt. Urs Rickenbacher alisema, “Maabara yetu ya Lantal kwa ajili ya vipimo nchini Uswisi inajulikana vema kwa huduma zake bora na haraka. 

"Kwa sasa tunalo soko kubwa barani Ulaya na sasa maabara yetu hapa Abu Dhabi tukishirikiana na Kitengo cha Uhandisi cha Shirika la Ndege la Etihad (Etihad Aiways Engineering) litatuwezesha kutoa huduma kwa ukaribu zaidi na wateja wetu wa Mashariki ya Kati”, alisema.

MAONI YA WATEJA NI MUHIMU KWA UKUAJI WA BIASHARA YAKO

Na Jumia Travel Tanzania
KUJA kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia hususani mtandao wa intaneti kumebadilisha kwa kiasi kikubwa mienendo ya matangazo ya utoaji wa huduma mbalimbali duniani na hii ni kutokana na uwezo wake wa kuwaruhusu wateja kutoa ushuhuda, kukosoa au kutoa maoni juu ya walichohudumiwa na kujionea.

Tofauti na kipindi cha nyuma kidogo ambapo wataalamu wa masoko walikuwa wanatumia zaidi njia za luninga na redio kuwafikia wateja wao, siku hizi mfumo wa intaneti unapewa kipaumbele zaidi kutokana na namna unavyofikia watu wengi zaidi ndani ya muda mfupi, kwa haraka na gharama kidogo.

Matangazo ya luninga na redio yanaweza kuwa hayana ushawishi mkubwa ukilinganisha na mtandao wa intaneti kwani hivi sasa makampuni yanaweza kuwasilisha bidhaa na huduma zao na kupokea majibu kujua kwamba zinakubalika au la. 


Hali hiyo ni dhahiri kutokana na makampuni mengi kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika teknolojia na rasilimali watu katika kusimamia tovuti na kurasa zao rasmi za mitandao ya kijamii kama vile facebook, twitter, instagram na mingineyo/Inaendea>>BOFYA HAPA

WAPINZANI DRC WASEMA MAZUNGUMZO YALEGALEGA

Wapinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanasema mazungumzo ya namna Rais Joseph Kabila (pichani) atakavyoondoka madarakani yanalegalega na yamkini yakasambaratika.

Kwa mujibu wa Félix Tshisekedi mmoja kati ya vinara wa upinzani, pande husika katika mazungumzo hayo zinakaribia kusambaratika kuliko kupata suluhisho.

Jana mazungumzo baina ya serikali na vyama vya upinzani chini ya upatanishi wa Kanisa Katoliki yamefanyika mjini Kinshasa. Jana Alhamisi makasisi wapatanishi walikutana na Rais Kabila pamoja na kiongozi mkongwe wa upinzani Etienne Tshisekedi/KUSOMA ZAIDI>BOFYA HAPA 

FRANCIS CHEKA AFUNGIWA MIAKA MIWILI

SERIKALI KUANDAA TAMASHA MBALIMBALI JUU YA ELIMU YA KURIDHIA MKATABA WA MATUMIZI YA DAWA ZA KUONGEZA NGUVU MICHEZONI

Na. Lilian Lundo
MAELEZO.
Dar es Salaam
30.12.2016

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa  na Michezo pamoja na  Tume ya Taifa ya UNESCO wamekusudia kuandaa tamasha na matembezi mbalimbali ili kutoa elimu kwa jamii kuhusu udhibiti wa matumizi ya dawa na mbinu za kuongeza nguvu michezoni.

Hayo yamebainishwa leo Jijini Dar es Salaam na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo,  Dkt. Moshi Kimizi namna ambavyo Serikali imekusudia kuanzisha kampeni hizo ili kuionyesha jamii athari mbalimbali za kisaikolojia na kiafya kwa wachezaji na hasa vijana.

Aliongeza kuwa mwezi Juni mwaka huu, Bunge la Tanzania liliridhia mkataba wa kimataifa wa udhibiti wa matumizi ya dawa na mbinu za kuongeza nguvu katika michezo, hatua iliyolenga kulinda na kuimarisha afya za wanamichezo nchini.

“Kwa kuridhia mkataba huu na kuutekeleza itainufaisha nchi kuweza kuhudhuria mafunzo, mikutano na vikao vya kimataifa na kushiriki katika makongamano yenye maamuzi mbalimbali yanayohusu suala hili” alisema Dkt. Kimizi.

Kwa mujibu wa Kimizi alisema kupitia mkataba huo, wanamichezo, walimu wa michezo na wadau wa michezo wataweza kuelimishwa kuhusu athali za matumizi ya dawa au mbinu za kuongeza nguvu michezoni pamoja na aina ya vyakula au vinywaji ambavyo vina asili ya kuongeza nguvu mwilini.

Kwa upande wake Afisa Michezo, Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Rashidi Mijuza alisema  kuwa, wanamichezo wengi hujikuta wakiwekewa dawa za kuongeza  nguvu na walimu wao katika chakula au vinywaji bila kujua ili tu waweze kushinda.

Kwa mujibu wa Mijuza alisema Serikali imekusudia kutoa elimu kwa wanamichezo na walimu ili kuondokana na visingizio vya kutojua au udanganyifu ambao umekuwa ukifanyika kwa wanamichezo pindi wanapokuwa katika mashindano mbalimbali.

“Kwa Tanzania kuridhia mkataba huo, nchi itanufaika na mambo mbalimbali katika sekta ya michezo ikiwa ni pamoja na Tanzania kushiriki na kuandaa mashindano mbalimbali ya kimataifa, kupata misaada ya wataalamu, fedha na mafunzo kwa ajili ya utekelezaji wa makubaliano” alisema Mijuza

EWURA YAIDHINISHA ONGEZEKO LA ASILIMIA 8.5 YA BEI YA UMEME

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeidhinisha asilimia 8.5 ya ongezeko la bei ya huduma za umeme ili kukidhi gharama za uzalishaji wa umeme.


Ongezeko hilo limetangazwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Felix Ngamlagosi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maombi ya kurekebisha bei za umeme ambapo marekebisho hayo yanatarajiwa kuanza kutekelezwa kuanzia Januari Mosi mwaka 2017.

Ngamlagosi amesema kuwa TANESCO iliomba kuidhinishiwa ongezeko la bei ya huduma hizo ili kuliwezesha shirika hilo kupata fedha za kulipia gharama za uendeshaji, kupata fedha za uwekezaji katika miundombinu pamoja na kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia asilimia 75 ya wananchi wote ifikapo mwaka 2025.

”Baada ya TANESCO kuwasilisha taarifa zinazohitajika kwa ajili ya kukamilisha maombi yao, EWURA ilifanya mikutano ya taftishi, matangazo kwa umma pamoja na kushirikisha wadau mbalimbali kutoa maoni juu ya ongezeko hilo ambapo baada ya uchambuzi wa maoni hayo tulilidhia kuongeza asilimia 8.5 tu ya ongezeko la bei hizo ,” alisema Ngamlagosi.

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) ambalo linanunua umeme wa jumla kupeleka Zanzibar limeongezewa asilimia 5.7 ya bei ya umeme badala ya asilimia 19.1 iliyoombwa na TANESCO.

Amefafanua kuwa kulingana na marekebisho yaliyofanyika, jumla ya mapato yanayohitajika kwa mwaka 2017 ni shilingi bilioni 1,608.47 ambayo ndiyo iliyopelekea ongezeko la bei la wastani wa asilimia 8.5 hivyo gharama za umeme zimeongezeka kutoka shilingi 242.34 kwa uniti moja hadi shilingi  263.02 kwa uniti moja.

Aidha, Mkurugenzi huyo ametoa maagizo kwa TANESCO yakiwemo ya kuanzisha tozo ya mwezi ya shilingi 5,520 kwa wateja wa kundi linalohusisha viwanda vidogo, mabango na minara ya mawasiliano, kuboresha huduma kwa wateja pamoja na kuacha kuwaunganisha wateja wadogo kwenye kundi la wateja wakubwa na badala yake kuwaonganishe moja kwa moja katika kundi la wateja wadogo.

Amewataka wananchi kuelewa kuwa kundi linalojumuisha wateja wa majumbani ambao matumizi yao ya umeme hayazidi uniti 75 kwa mwezi hawataathirika na ongezeko hilo la bei.

CCM KASULU YATOA ADHABU KWA MBUNGE NA MADIWANI WAKE KWA TUHUMA ZA KUCHOCHEA MGOGORO WA KUMPINGA MWENYEKITI WA HALMASHAURI YA MJI WA KASULU

Na Rhoda Ezekiel- Kigoma
KAMATI ya Usalama na maadili na kamati ya siasa ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, imetoa adhabu kwa Mbunge wa Viti maalum wa Mkoa wa huo, Josephin Ngezabuke na madiwani sita wa Halmashauri ya mji wa Kasulu kwa tuhuma za kuchochea mgogoro wa madiwani kupinga uongozi  wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu..

Akizungumza na Waandishi wa Habari jana Katibu Mwenezi wa Wilaya ya Kasulu Masoud Kitowe alisema kumekuwa na mgogoro Mkubwa uliodumu kwa miezi mitano wa Baadhi ya madiwani wa Act na CCM waliomuandikia barua Mkurugenzi ya kudai Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Kasulu aondolewe hafai na Chama Cha mapinduzi hakikupatiwa barua hiyo ambayo ingeweza kuwasaidia kujua chanzo cha tatizo nini.

Alisema katika mgogoro huo madiwani wa CCM walio shiriki ni watano na kati ya hao mmoja ambaye ni Seleman diwani wa kata ya Kumnyika amepewa adhabu ya kalipio ambayo ataitumikia kwa miezi 18 kwa kosa na kushiriki kuandika barua ya kumkataa mwenyekiti wa Halmashauri hiyo wakati jambo hilo bado halijajadiliwa katika Kikao cha Chama kwamujibu sisi kama chama tulipo pata taarifa kutoka kwa Mkurugenzi tuliwaita madiwani walio husika na kupewa onyo.

Aidha kitowe alisema madiwani wanne waliojiorodhesha kwenye barua ya kushiriki kumpinga Mwenyekiti huyo kamati ya siasa pia imetoa adhabu ambayo kwa Mujibu wa Sheria za Chama cha mapinduzi hairuhusiwi kuitangaza hazarani nao watatumikia adhabu hiyo kwa miezi 12.

Alisema Madiwani hao walipo hojiwa walikili mgogoro huo una chochewa na baadhi ya watu ambao ni Diwani wa Kata ya Murusi Steward Zinduse ambae alikuwa akigombea nafasi ya Mwenyekiyi wa halmashauri akashindwa pamoja na Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Kigoma Josephini Ngezabuke nao pia wamepewa adhabu ambayo hairuhusiwi kutangazwa kwa mujibu wa sheria na barua walishapewa zinazo elezea adhabu zao.

Hata hivyo Kitowe alitaja sababu zinazo pelekea Mbunge huyo kumkataa Mwenyekiti wa halmashuri ni kwamba aliwahi kumuomba meya wa kasulu ashiriki vikao vya halmashauri ya Mji wa Kasulu baada ya kukataliwa kwakuwa ni mjumbe wa Baraza la madiwani kakonko alijenga chuki na Mwenyekiti huyo ,jambo la pili alimuomba mea amuite Everina diwani wa viti maalumu kwa madai avuliwe madaraka ya udiwani viti maalumu kutokana na migogoro ya kifamilia kati yake na diwani huyo wa viti maalum.

"Kwa mbunge wetu huyu migogoro ni kawaida yake ukiona kasulu kuna migogoro ujue kuna watu wanaochochea, ikumbukweMwaka 2010 kamati ya Siasa ya Mkoa ilimpa azabu ya kalipio mbunge huyo kutokana na migogoro kwakuwa yeye anadai anawatu juu watatengua adhabu hiyo ndio maana anaendelea na migogoro hiyo inayo sababisha Halmashauri kushindwa kufanya shughuli za maendeleo suala ambalo hatulifurahii sisi kama Chama". alisema.

Alisema Madiwana hao watano baada ya kupewa adhabu waliachana na mgogoro huo lakini mpaka sasa Mbunge huyo pamoja na Diwani wa Kata ya Murusi alie kosa nafasi hiyo bado wanaendeleza Mgogoro huo suala ambalo halina masilahi katika chama zaidi ya kudhohofisha halmashauri yetu ya Mji wa Kasulu.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti maalumu Josephen Ngeza buke alisema hawezi kwenda kwenye halmashauri ya kasulu kuingia kwenye kikao na kufanya vurugu kwakuwa sheria ninazifahamu ninauwezwa kufanya vurugu hata nikiwa nje siwezi kupiga kura sehemu mbili yeye ni Mjumbe wa Halmashauri ya kakonko anacho hitaji ni yeye kupewa heshima kama Mbunge wa Mkoa anapo fika katika Halmashauri ya Wilaya ya kasulu nikeshimike kama Mbunge.

" Mimi sio kwamba simuhitaji Mweenyekiti sina shida na mwenyekiti wala kurudi kwenye Baraza la mji wa kasulu mimi nitabaki Kakonko lakini ninacho hitaji niheshima mimi kama mwenyekiti wa UWT na Mbunge wa Mkoa mzima,Siwezi kuleta malalamiko yangu kwamba mtu kanifanyia vurugu nyumbani kwangu nisisikilizwe na hata Zinduse mwenyewe amekwisha ridhika na Mwenyekiti",alisema Ngezabuke.

CCM KIBAHA MJINI KUZINDUA KESHO KAMPENI ZA UCHAGUZI MDOGO WA UDIWANI KATA YA MISUGUSUGU


Wajumbe wakifuatilia jambo katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Kibaha Mjini, kilichofanyika ili kuweka mikakati ya ushindi katika uchaguzi mdogo  wa kata ya Misugusugu,ambapo kesho itazindua kampeni zake (Picha na Mwamvua Mwinyi) 
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini, kinazindua kampeni zake kesho za uchaguzi mdogo wa Udiwani Kata ya Misugusugu, huku kikiwa kimejipanga kushinda kwa kishimndo katika uchaguzi huo kutokana na mikakati ambayo kimejiwekea.
Uchaguzi huo unarejea kwa sababu march 31/ 2016, mahakama ya mkoa wa Pwani ilitengua uteuzi wa diwani wa chama hicho Addhudad Mkomambo ambae alishinda katika uchaguzi mkuu uliopita.
Aidha katika uzinduzi huo mwenyekiti wa CCM mkoani Pwani,Mwinshehe Mlao anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Katibu wa CCM Kibaha Mjini,Abdallah Mdimu ,aliyasema hayo katika kikao cha halmashauri kuu ya CCM wilaya ,kilichokaa ili kujiwekea mikakati madhubuti ya kupata ushindi kwenye uchaguzi huo.
Alieleza kwamba uchaguzi huo ulitenguliwa kutokana na namba saba kuzidi kwa hesabu kati ya waliopiga kura na kura walizopata wagombea wa vyama vyote hivyo mahakama kufanya maamuzi hayo ili kujiridhisha.
“Wapiga kura wote walikuwa 4,830,waliopiga kura 3,191,huku katika matokeo CCM ilipata kura 1,545,chadema 1,525,ACT 66 na CUF 55 "

KILIO CHA MBUNGE RIDHIWANI CHASIKIKA, RC NDIKILO ATOA MWEZI MMOJA KWA WAFUGAJI

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid  Mwanga akizungumza kwa wananchi  katika mkutano wa kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji katika kijiji cha Kitoga kata ya Vigwaza  
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo akitoa maelekezo kwa wanakijiji baada ya kufika katika kijiji cha Kitonga kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji.

MAREKANI KUWATIMUA WANADIPLOMASIA WA URUSI


Rais Obama  ameamuru kutimuliwa kwa wanadiplomaisa thelathini na tano wa Urusi kufuatia tuhuma za Urusi kutaka kuingilia kati uchaguzi wa Marekani kupitia njia ya mtandao.
Makazi ya wanadiplomasia wawili wa Urusi yamefungwa na baadae kuwekewa vikwazo.
Rais Obama amesema Urusi imekuwa ikiwadhalilisha maafisa wa Marekani na ametahadharisha hatua zaidi kuchukuliwa.
Obama ameendelea kusema wamarekani wote sharti washtushwe na vitendo vya Urusi, hii ikionekana kama njia ya kumjibu mrithi wake Donald Trump ambae amesema kila mtu aishi maisha yake.
Kwa upande wake, rais mteule mara kwa mara amekuwa akizipuuzia taarifa hizo za udukuzi, lakini hivi amesema atakutana na wakuu wa mashushu wa Marekani ili kulijadili hilo.
Urusi nayo imekana tuhuma za kufanya udukuzi mfumo wa mtandao wa chama cha Democratic.
Msemaji wa serikali ya Urusi amesema Urusi nayo italipiza kwa kiwango hicho hicho.

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUKAMATWA KWA WATANZANIA WANAODAIWA NI MAJASUSI NCHINI MALAWI

 
Baadhi ya Vyombo vya habari vya hapa nchini hivi karibuni vilitoa taarifa kuwa, Watanzania 8 wanaodaiwa kuwa ni majasusi wa Serikali ya Tanzania wamekamatwa nchini Malawi kwa tuhuma za kuingia kwenye mgodi wa urani wa Kayerekera uliopo nchini Malawi kinyume cha sheria.
Taarifa hiyo kwa mara ya kwanza ilitolewa na chombo cha habari cha Malawi ambacho kilidai kuwa watu hao wametumwa na Serikali ya Tanzania ili kuchunguza kama Serikali ya Malawi inatengeneza silaha za nyuklia kwa kutumia madini ya urani ya kutoka mgodi huo.
Kufuatia taarifa hizo, Wizara kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi ulifuatilia ili kubaini ukweli wa tukio hilo. Baada ya kufuatilia ilibainika kuwa ni kweli Watanzania 8 kutoka taasisi ya CARTAS iliyo chini ya Kanisa Katoliki Songea mkoani Ruvuma walikamatwa na vyombo vya usalama katika Wilaya ya Karonga ambayo inapakana na Wilaya ya Kyela.
Watanzania hao mara moja walifunguliwa kesi kwa kutuhumiwa kufanya kosa la jinai la kuingia eneo la mgodi bila kibali (criminal trespass).
Ubalozi uliwasiliana na Taasisi ya CARTAS kutaka kufahamu madhumuni ya watu hao kufanya ziara nchini Malawi. Ubalozi ulielezwa kuwa ziara hiyo ilikuwa ni ya mafunzo ambapo walitaka kufahamu juu ya madhara yatokanayo na machimbo ya madini ya urani. Watanzania hao kwa sasa wapo katika gereza kuu la Mzuzu hadi kesi yao itakapotajwa tena tarehe 04 Januari 2017.
Ubalozi unaendelea kufanya mawasiliano na Kanisa Katoliki Songea ili kupata maelezo zaidi kuhusu ziara ya watu hao kwa madhumuni ya kuyawasilisha mamlaka husika ili watuhumiwa waweze kutolewa.Aidha, Wizara kupitia Ubalozi umebaini kuwa CARTAS iliruhusu watu hao kufanya ziara nchini Malawi bila kupata kibali kutoka mamlaka husika na bila kutoa taarifa Ofisi ya Ubalozi kuhusu ziara hiyo.Aidha, kipindi cha kufanya ziara hiyo nchini Malawi hakikuwa muafaka kwa kuwa watumishi wa Serikali ya Malawi wanakuwa katika likizo ya mwaka kuanzia tarehe 22 Desemba hadi 03 Januari 2017. Hii inakwamisha juhudi za kuwafuatilia watu hao ikiwa ni pamoja na kukwama kwa maombi ya kibali cha kuwatembelea watu hao tarehe 28 Desemba 2016.
Wizara inatoa wito kwa mara nyingine kwa taasisi za dini, vyuo vya elimu na watu binafsi kuomba vibali na kufuata sheria za nchi nyingine wanapofanya ziara za mafunzo au ziara nyinginezo ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na ofisi za Balozi zetu kwa madhumuni ya kufahamishwa taratibu zinazotakiwa kufuatwa kabla ya kufanya ziara husika ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.
Wizara, kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi unaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa suala hilo linapatiwa ufumbuzi kwa haraka.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Dar es Salaam, 29 Desemba 2016.
ª