Breaking News

Your Ad Spot

Dec 15, 2016

ALIYETOBOLEWA MACHO USO KWA USO NA SCORPION

Kwa mara ya kwanza mshitakiwa katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi, Salum Njwete maarufu Scorpion, amekutana na mlalamikaji katika kesi hiyo, Said Mrisho katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, iliposikilizwa jana.
Mrisho, ambaye ndiye shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, aliieleza mahakama hiyo kuwa alichomwa visu tumboni na mgongoni kabla ya kutobolewa macho.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga mbele ya Hakimu Mkazi, Flora Haule, Mrisho alidai kuwa wakati tukio hilo linaendelea, alimkariri mshitakiwa kwa kumuangalia usoni.
Akielezea tukio lilivyotokea, alidai Septemba 6, mwaka huu saa nne usiku alikuwa kazini kwake Tabata Segerea kwa kazi yake ya kinyozi na baada ya kufunga ofisi, alikwenda kituoni kusubiri usafiri wa kwenda nyumbani kwake Makuburi, karibu na Ubungo.
Alidai wakati anasubiri usafiri, ilipita bajaji na kumuuliza anakokwenda, ambapo alimwambia kwamba anakwenda Ubungo na mwenye bajaji alidai anakwenda Buguruni, ila anaweza kumsogeza hadi Tabata Relini ili akapande magari ya Ubungo.
‘’Wakati nishapanda bajaji na tumeelewana anifikishe Tabata Relini ghafla dereva huyo aliniomba apite njia ambayo ni fupi kutokezea Buguruni, ambapo hapo ndiko nitakapochukulia magari ya Ubungo kwani naishi Makuburi,” alidai Mrisho.
Alidai baada ya kufikishwa Buguruni Kwa Mnyamani, aliona wauza kuku na kusogea kwa ajili ya kununua ili kupeleka nyumbani kwake.
‘’Kulikuwa kuna wafanyabiashara wengi wa kuku eneo la Buguruni kituo kinaitwa Kwa Mnyamani kama saa 4:40 usiku ambapo nilinunua kuku mmoja kwa Sh 6, 000,” alidai.
Akiendelea kutoa ushahidi, Mrisho alidai wakati anaendelea na manunuzi na kuongea na muuzaji, aliona mtu amesimama upande wake wa kulia na alianza kumuita.
‘’ Aliniambia ‘broo’ nina shida. Nami nilimgeukia na kumuuliza una shida gani kama una shida sema nakusikiliza kama naweza kukusaidia nikusaidie, lakini mtu huyo hakujibu ambapo niliendelea na manunuzi,’’alidai.
Shahidi alidai wakati anaendelea na manunuzi alishikwa na hofu, kwani mkono wake alikuwa amevaa cheni ya silva na mfuko wa suruali, ulikuwa na fedha iliyokuwa inaonesha kutuna.
‘’Ghafla nilishtukia ninachomwa visu mkononi na bega la kushoto ambapo nilipogeuka niliendelea kuchomwa na nikaanza kupiga kelele ya mwizi lakini sikupata msaada, kwani nilishangazwa kuona watu wananiona lakini hawanipi msaada,’’alidai na kuongeza: 
‘’Yule mtu alijibu hakuna mtu wa kumsaidia ambapo aliendelea kumchoma visu vinne tumboni na kuanguka chini wakati huo kuna watu walikuwa wanamwita Scorpion, kwamba tayari umeshaua huku akiendelea kunikagua mfukoni,’’alidai.
Alidai wakati anaendelea kukaguliwa, mshitakiwa alimkanyaga mkono wake na kumkata cheni ambayo alikuwa amevaa mkononi na shingoni. Pia, alidai kuwa alivyodondoka chini alidondoka chali kwa hiyo alikuwa na nafasi ya kumkariri vizuri jinsi alivyo, kwa kuwa kulikuwa na mwanga wa taa.


Aliiambia mahakama kuwa, mshitakiwa aliendelea kumkagua mfukoni na kuchukua fedha zote na kwamba alisikia sauti kuwa, “Salum mwache huyo keshakufa sasa ukimchukulia na simu ndugu zake watajulishwaje?” Shahidi alidai baadaye alivuliwa fulana na kumfunga mkononi kisha akamburuza kumpeleka barabarani huku akiwaambia wenye magari wamgonge.


“Muda huo nilikuwa sijatobolewa macho ambapo niliwekwa barabarani ili nigongwe na gari, lakini yalikuwa yananipita nilikaa barabarani kama nusu saa wakati huo yeye kasimama pembeni. “Baada ya muda alinivuta pembeni na kunipiga kisu cha jicho la kushoto ambapo nilipoteza fahamu kwa muda na baadaye nilisikia mtu anadai yeye ni raia mwema anataka kunisaidia ambapo nilimpa simu na kuanza kuwasiliana na ndugu zangu,’’alidai.


Shahidi huyo alidai baada ya muda alisikia gari la polisi limefika na kumchukua hadi kituoni kwa ajili ya kupewa Fomu Namba Tatu(PF3) kwa ajili ya matibabu. 


Aidha, alidai kwa kuwa alikuwa anasikia maumivu, alichukuliwa maelezo akiwa ndani ya gari ambapo baadaye alifikishwa Hospitali ya Amana na kupewa huduma ya kwanza.


Shahidi huyo alidai alipofika Amana, alikutana na ndugu zake na baada ya muda alipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo alipewa kitabu cha kusaini kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji tumboni. 


Pia alidai baada ya muda, daktari wa macho alimfanyia uchunguzi na kueleza kuwa macho yametobolewa, ambapo alikaa hospitali kwa siku sita.


Kabla ya kuanza kutoa ushahidi huo, mshitakiwa ambaye alipandishwa kizimbani saa 3.35 asubuhi, aliomba mahakama isianze kusikiliza shauri hilo hadi wakili wake wa utetezi afike. 


Mahakama hiyo ilikubaliana na ombi hilo, ambapo baada ya dakika 15 kupita wakili alifika na kuanza na usikilizwaji.


Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, mshitakiwa ambaye ni mwalimu wa karate, alitenda kosa hilo Septemba 6, mwaka huu maeneo ya Buguruni Sheli wilayani Ilala.


Ilidaiwa mshitakiwa aliiba cheni ya dhahabu gramu 38 yenye thamani Sh 60,000, kibangili cha mkononi na Sh 331,000 pamoja na pochi, vyote vina thamani ya Sh 476,000, mali ya Said Mrisho.


Ilidaiwa kabla ya wizi huo, alimchoma na kisu tumboni mgongoni na machoni. Kesi hiyo itaendelea na ushahidi Desemba 28, mwaka huu na mshitakiwa alirudishwa rumande.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages