Breaking News

Your Ad Spot

Dec 22, 2016

HALI YAZIDI KUWA TETE DRC, 52 WAUAWA KATIKA MAANDAMANO, NA MAPIGANO YA KIKABILA

Hali ya mambo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imezidi kuwa tete huku makumi ya watu wakiuawa katika maandamano na mapigano ya kikabila.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema idadi ya watu waliouawa hadi sasa katika maandamano yalioyaoanza Jumatatu dhidi ya Rais Joseph Kabila baada ya muhula wake wa uongozi kumalizika imeongezeka na kufikia watu 34.
Ida Sawyer, Mkurugenzi wa eneo la Afrika ya Kati wa Human Rights Watch amesema, watu 19 wameuawa na maafisa usalama katika maandamano mjini Kinshasa, watano mjini Lubumbashi na sita katika miji bandari ya Goma na Matadi, magharibi mwa nchi. Hata hivyo serikali ya Kinshasa imesema ni watu 22 pekee waliouawa katika makabaliano kati ya waandamanaji na maafisa usalama na kwamba polisi kadhaa pia wameuawa.
Hii ni katika hali ambayo, watu wengine 18 akiwemo afisa wa polisi wameuawa leo Alkhamisi katika mapigano yaliyotokea kati ya makundi mawili hasimu ya waasi katika mkoa wa Mongala, kaskazini magharibi mwa nchi.
Captain Guillaume Djike, msemaji wa polisi katika mkoa huo amesema baadhi wameuawa kwa kufyatuliwa risasi na wengine kwa kukatwa kwa mapanga, baada ya kujiri mapigano kati ya kundi la waasi la Mai Mai Mazembe wa kabila la Nande na wapiganaji wa Nyatura wa kabila la Hutu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeondoka Ban Ki-moon ametoa wito kwa pande zote zinazohusika katika mgogoro wa kisiasa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutatua mgogoro huo kwa njia za amani.

Rais Joseph Kabila wa DRC anayekabiliwa na mashinikizo ya kuachia ngazi
Upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umewataka wananchi kutomtambua tena Joseph Kabila kama rais wa nchi hiyo na umewahimiza kuonesha upinzani wao dhidi ya Kabila kwa njia ya amani.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages