Breaking News

Your Ad Spot

Dec 22, 2016

JAJI SEMISTOCLES KAIJAGE MWENYEKITI MPYA WA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI-NEC

Ikulu, Dar es Salaam
Rais Dk. John Magufuli, leo tarehe 22 Desemba, 2016 amemteua Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jaji Semistocles Kaijage kuwa Mwenyekiti mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Taarifa iliyosambazwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jijini Da es Salaam, imesema Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi ameeleza kuwa Jaji Semistocles Kaijage ameteuliwa kuongoza Tume hiyo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia tarehe 20 Desemba, 2016.

Kufuatia uteuzi huo, Jaji Semistocles Kaijage anachukua nafasi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Damiani Lubuva ambae muda wake wa kushika wadhifa huo umemalizika rasmi tangu tarehe 19 Desemba, 2016.

Kadhalika Rais Magufuli amemteua Jaji Mstaafu Hamid Mahamoud Hamid kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kipindi kingine cha miaka mitano, kuanzia tarehe 20 Desemba, 2016.

Jaji Mstaafu Hamid Mahamoud Hamid alikuwa Makamu Mwenyekiti wa NEC na amemaliza kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano mnamo tarehe 19 Desemba, 2016.

Pia Rais Magufuli amemteua Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa,  Jaji Harold Reginald Nsekela kuwa Kamishna wa Maadili katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia tarehe 20 Desemba, 2016.  

Jaji Mstaafu Nsekela anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Mstaafu Salome S. Kaganda ambae amestaafu mnamo tarehe 10 Desemba, 2016.

Taarifa hiyo ya Ikulu imesema, katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewateua Majaji wanne wa Mahakama Kuu kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani kuanzia leo tarehe 22 Desemba, 2016. Majaji hao,  Jaji Dk. Gerald Ndika, Jaji Jackobs Mwambegele, Jaji Rehema Kiwanga Mkuye na  Jaji Sivangilwe Sikalalilwa Mwangesi

Wateule wote waliotajwa katika taarifa hii wataapishwa kesho Ijumaa, tarehe 23 Desemba, 2016 saa 3:00 asubuhi Ikulu Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages