.

KUCHAGULIWA TENA MUGABE KUGOMBEA URAIS KATIKA UCHAGUZI WA 2018 NCHINI ZIMBABWE

Dec 18, 2016

Rais Robert Mugabe wa Zimbambwe amechaguliwa tena kubeba bendera ya chama tawala cha Zanu-PF katika uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwaka 2018.
Mugabe amechaguliwa tena kupeperusha bendera ya chama hicho katika mkutano wa kila mwaka wa chama cha Zanu-PF uliofanyika jana katika mji wa  Masvingo nchini Zimbabwe. Katika mkutano huo wajumbe wa chama tawala walitangaza himaya yao kwa Mugabe kama mgombea pekee wa chama hicho katika uchaguzi ujao wa rais hapo mwaka 2018. 
Mugabe amechaguliwa tena kugombea urais kwa tiketi ya chama tawala cha Zanu-pf mwaka 2018 katika hali ambayo, juma lililopita alitangaza kuwa, juhudi za baadhi ya maafisa wa chama hicho za kutaka kumchagua mrithi wake mtarajiwa zinakinzana na ada ya chama hicho. Mugabe sambamba na kutangaza utayari wake wa kuwania tena kiti cha urais katika uchaguzi ujao alilaani kile alichokitaja kuwa siasa chafu katika chama hicho na kusisitiza kwamba, wajumbe wa chama tawala hawana haki ya kuchukua hatua yoyote ile ya kumchagulia mrithi. Kundi moja ndani ya chama tawala cha ZANU-PF lilikuwa likifanya juhudi za kumtangaza Grace mke wa Mugabe kuwa mrithi wa baadaye wa mumewe huku kundi jingine likiwa linamuunga mkono Emmerson Mnangagwa Makamu wa Rais wa Zimbabwe.
Rais Mugabe katika moja ya mikutano yake ya kisiasa
Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 92 amechaguliwa tena kuwania kiti cha urais kwa tiketi ya chama tawala katika uchaguzi ujao katika hali ambayo, akthari ya wananchi wa nchi hiyo na hata maveterani wenzake wanamtaka aachie uongozi na kukabidhi jukumu hilo kwa mtu mwingine. Kwa muktadha huo mivutano ya kisiasa itaendelea kushuhudiwa nchini Zimbabwe kutokana na hatua ya Rais Mugabe ya kung'ang'ania kuendelea kubakia madarakani huku mikusanyiko na malalamiko ya aina yoyote ile yakikandamizwa vikali na vikosi vya usalama vya nchi hiyo.
Siku chache zilizopita, Shirika la Msamaha Duniani Amnesty International, lilitangaza kuwa, radiamali ya polisi dhidi ya malalamiko na maandamano katika mitaa na barabara za nchi hiyo ni ukiukwaji wa wazi wa haki za raia. Pamoja na hayo, mbinu ya kale ya kuwakandamiza wapinzani kwa kutumia mabavu na kuwatisha wafuasi wa vyama vya upinzani ingali inaendelea katika nchi hiyo.
Wapinzani wengi sambamba na kukosoa sera za Robert Mugabe wanaamini kwamba, kiongozi huyo kutokana na umri mkubwa alionao hawezi tena kuiongoza nchi kama inavyotakiwa huku athari yao wakikosoa siasa zake hususani katika miaka ya hivi karibuni.
Grace, mke wa Rais Mugabe
Hata kama Zimbabwe kama zilivyo athari nchi za Kiafrika inakabiliwa na matatizo ya kiuchumi, umasikini na ukosefu wa ajira, lakini katika miaka ya hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia mgogoro wa kiuchumi ukishadidi kiasi kwamba, wafanyakazi wa serikali hawajapokea mishahara yao kwa miezi kadhaa.  Aidha theluthi mbili ya wakazi milioni 14 wa nchi hiyo wanapitisha maisha yao kwa kufanya biashara ndogo ndogo za mikononi.
Katika wiki za hivi karibuni serikali ya Zimbabwe ikiwa na lengo la kukabiliana na mgogoro wa kifedha inaokabiliwa nao, ilichapisha noti mpya na kuziingiza katika mzunguko wa fedha. Viongozi wa Zimbabwe wanaamini kwamba, sera hizo mpya za kifedha zitaweza kutatua tatizo la uhaba wa fedha naakidi. Hata hivyo wakosoaji wa serikali ya Harare wanasema kuwa, hatua hiyo ya serikali itapunguza thamamani ya akiba ya fedha ya nchi hiyo na kuporomosha thamani yake kufikia kiwango cha chini kabisa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.
Maandamano ya kulalamikia ukosefu wa ajira Zimbabwe
Ukame ni tatizo jingine linaloiandama Zimbabwe. Zimbabwe ambayo wakati fulani ikitambulika kama ghala la nafaka Afrika, hivi sasa  inakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayojulikana kama Elnino. Hali hiyo imemfanya Rais Mugabe atangaze hali ya hatari na kuitaka jamii ya kimataifa iisaidie nchi hiyo ili iweze kujidhaminia bidhaa za chakula.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช