.

SIMULIZI ZA KUSISIMUA : VIJANA WENYE MSIMAMO MKALI WA MLIMANI - MKAPA WALIMWITA 'PROFESA' WA UJAMAA

Dec 14, 2016

Image may contain: 1 person, eyeglasses, sunglasses and closeup

Mwanazuoni Born Again Pagan ameendelea kusimulia kupitia mtandao wa mjengwablog. Kwa wakati huo ilikuwa ni dhamira au busara (prudence) ya vijana hao wachache wenye msimamo mkali kuyaona matukio hayo yakitoa changamoto; wakapata fursa (opportune) kuyatafsiri ili yawe na maana maishani.

Ni wakati huo zilionekana ishara za Kushindwa kwa siasa na sera za ki-Bepari, chini ya Mpango wa Taifa ya Maendeleo wa Miaka Mitatu-Mitatu (ulioishia mwaka 1965). Mipango hii ilizalisha matabaka ya akina “ma-naiza” na “ma-kabwela” (mithili ya hali ilivyo sasa nchini kwetu) Ikumbukwe kwamba mfumo wa mipango hiyo ulitungwa na Mashirika ya Kimataifa ya Fedha (Benki Kuu ya Dunia na Mfuko wa Fedha).
Kujengeka kwa matabaka hayo ya “ma-naiza” na “ma-kabwela” kulichangia sana kuelekea kwenye
wimbi la Ujamaa wa ki-Afrika. Wimbi hili lilitingisha sana, eti, maslahi ya wakubwa wengine kwa kuogopa kile Waziri Mkuu wa u-China Chou-en-Lai alichokiita “Afrika imeiva tayari kwa mapinduzi” (Africa is ripe for a revolution) – kufuatia safari yake katika nchi kadhaa za ki-Afrika, ikiwemo Tanzania.
Ni wakati huo, akapinduliwa  Rais wa Ghana Kwame Nkrumah, ikiwa ni pamoja na nchi nyingi za Magharibi na Amerika kushirikiana katika kuunga mkono askari wa kukodiwa (mercenaries) walioranda-randa na kutamba-tamba katika nchi changa za Uwanda wa Joto wa Afrika na kutumika katika kupindua serikali zake.
Ni wakati huo kikazaliwa Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki: Makerere (Udaktari na Kilimo), Nairobi (Uhandisi na Biashara), na Dar (Sheria na Elimu) na kuvunja uhusiano wa ki-taaluma na London University. Tukawa na digirii zetu za Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki badala ya za London University. Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki kiliwakutanisha vijana wengi.

Ni wakati huo kukatangazwa Azimio la Arusha: Tanzania ilikaribisha “frustrated socialists”, ambao hawakuweza kupata ukumbi wa kufundisha au kutekeleza hayo ya Ujamaa huko kwao Ulaya. Baadaye, baadhi yao walikuja Tanzania, hasa baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha.
Azimio la Arusha liliwavuta, sio tu “frustrated socialists”, bali hata wale ambao hawakuwa –wenye kutaka kutekeleza mfumo mpya wa maendeleo vjijini. Kwani kiini cha Azimio la Arusha kilikuwa na mambo mawili makubwa:
Ki-itikadi, lilikusudia kujenga akilini Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Ki-mkakati, liliashiria, kwa makusudi, kutekeleza mkakati uliojaa michakato ya kuleta mapinduzi ya uchumi na maslahi ya jamii vijijini (a total rural reform, transformation, transistion and change), ambayo yalikuwa hayajawahi kutekelezwa katika nchi changa, nje ya u-Uchina, Korea Kasikazini na Kuba!
Mlimani ikawa ndio “kisima cha wanyama wenye kiu” ya itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea pamoja na nia ya kufanikisha mapinduzi ya uchumi na maslahi ya jamii vijijini (rural development strategy)!
Baadaye, nchi za Magharibi zilimshutumu Rais Nyerere kwa kuchomekeza wana-harakati wake wa ki-soshalisti katika nchi tulivu za Ukanda wa Joto wa Afrika (“unleashing his guerrilla socialist locusts in the otherwise tranquil savannah landscape”. Lakini Nyerere alipona kupinduliwa na ma-Bepari wenye kuchukia mwingilio wa Ujamaa!
Ni wakati huo, mgogoro wa Mashariki ya Kati ulijikita katika ukombozi wa wa-Palestina kutoka kuwafikiria kuwa ni wakimbizi tu kwenda katika suala la ukombozi wao. Msimamo huo uliingilia uhusiano wetu na serikali ya Israel, hususan, kufuatia vita ya mwaka 1967 ambapo Israel iliteka sehemu ya Sinai (sehemu ya Misri – Afrika). Tanzania tulivunja uhusiano na serikali ya Israel.
Hadi kufikia wakati huo, Israel ilikuwa imewekeza katika kuanzisha Jeshi la Kujenga Taifa, misaada mingine ya ki-Jeshi la Ulinzi na usalama, utalii (ikiwa ni pamoja na kutujengea Hoteli za ki-talii, kwa mfano, Kilimanjaro kupitia Molonot, biashara ya Karadha, na miradi mingine ya kilimo cha kiangazi (kumwagilia mashamba maji- Bugwema, Mkoa wa Mara).
Ni wakati huo,  Tanzania ikawa ni kisima cha ma-Profesa wenye mlengo wa kushoto (ma-Soshalisti), kwa mfano, kufuatia mapinduzi ya Ghana, wakaja ma-Prof. David Kimble (Political Science) na mkewe (Uchumi); kutoka Denmark akaja Prof. Knud Svendsen kuwa Profesa wa Uchumi (mshauri wa mambo ya uchumi kwa serikali na chama), Prof. Chodak (Sosiolojia), Prof. Osborn (Fisikia), Prof. Welbourne (Elimu) na baadhi ya ma-soshalisti ambao hawakuweza kuhubiri na kutekeleza imani yao makwao (Ulaya na Amerika).
Kulikuwepo na wengine kutoka Visiwa vya Karibe (Caribbeans), kama akina Walter Rodney (Historia) na Carl (Sheria) na wengine kutoka Kenya James Kamenju, Kiara na Cliffe.
Chuo Kikuu kiliwapokea wageni wengi kutoka serikali za Tanzania na vyama vyao vya TANU/Afro-Shirazi. Akina Ben Mkapa, Kingunge Ngombale-Mwiru na G. Mapunda (marehemu sasa) wakawa “ma-profesa” wetu wa Ujamaa. Wakawa wanakuja kutupanua mawazo yetu (kutupiga msasa) tuachane na tabia za u-Koloni mkongwe na u-Koloni Mamboleo (neo-Colonialism) – tuwe wazalendo kwa Tanzania na Afrika.
Ben Mkapa akatueleza ya “juche” (siasa ya kujitegemea) ya Korea Kasikazini. Tukamsikiliza kwa makini; tukayatafukari namna ya kuyatekeleza hayo ya Ujamaa. Sijui siku hizi Ben Mkapa na Kingunge Ngombale-Mwiru wamepotelea wapi na hayo ya Ujamaa? Ama wameona mwanga?
Ikiwa u-Bepari ulionekana mithili ya unyonyaji wa kupe au mithili ya u-nyama, je, leo hii unyonyaji huo umekwisha? Ama wa-Tanzania wa leo wenye nafasi wanakula na hao manyang’au?
Hizi ni simulizi endelevu.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช