.

SERIKALI: TANZANIA NI SALAMA, HAKUNA KIRUSI CHA ZIKA

Dec 18, 2016

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema hakuna uthibitisho wa kuwepo kwa ugonjwa wa Zika nchini humo.

Ufafanuzi wa Wizara hiyo umekuja siku moja baada ya Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kutoa ripoti ya utafiti uliofanywa na taasisi hiyo kwa kushirikia na Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Bugando, inayoeleza kuwepo maambukizi ya virusi vya Zika katika jamii ya Watanzania.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Tanzania Ummy Mwalimu ametoa ufafanuzi huo kwa waandishi wa habari , ambapo alisema wananchi wanapaswa kuondoa hofu kwa kuwa ugonjwa huo haujaingia nchini.


Zika
Awali, Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini Tanzania (NIMR) ilitangaza  kuwa, virusi vya Zika vimegunduliwa nchini humo. Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini Tanzania (NIMR), Dkt Mwele Malecela, ambaye alitangaza kugunduliwa kwa virusi vya Zika nchini Tanzania, amefutwa kazi.

Taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Ikulu, Gerson Msigwa inasema Rais wa John Magufuli wa Tanzania ametengua uteuzi wa mkurugenzi huyo mkuu. Tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemteua Prof Yunus Mgaya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) saa chache baada ya kumfuta kazi mkurugenzi wa awali Dkt. Mwele Malecela.
Brazil ndiyo chimbuko la mbu wanaosambaza kirusi cha Zika ambacho sasa kimeenea katika nchi 46 duniani tokea kuibuka kwa mara ya kwanza mwaka 2015. Kirusi hicho pamoja na mambo mengine husababisha wanawake wajawazito kujifungua watoto wenye vichwa vidogo na walio na matatizo ya ubongo.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช