.

MAGAZETI YA NDANI NA NJE YA TANZANIA LEO OKTOBA 21,2017

Oct 21, 2017


Magazeti zaidi>Bofya Hapa

MAHAFALI YA KIDATO CHA NNE YA SHULE INAYOTOA ELIMU KATIKA MFUMO USIO RASMI KWA YATIMA NA WAATHIRIWA WA NDOA NA MIMBA ZA UTOTONI MKOANI SHINYANGA

Shule ya Sekondari  ya Agape Knowledge Open School inayotoa elimu katika mfumo usio rasmi kwa yatima na waathiriwa wa mimba za utotoni,  imefanya Mahafali yake ya kwanza ya Kidato cha Nne ambapo jumla ya wahitimu 29 wametunukiwa vyeti.

Mahafali hayo yamefanyika jana, katika shule hiyo iliyopo mtaa wa Busambilo Kata ya Chibe Manispaa ya Shinyanga, mgeni akiwa Afisa Elimu Taaluma mkoa wa Shinyanga, James Malima ambaye alimwakilisha Mkuu wa mkoa huo, Zainab Telack. 

Mkuu wa shule hiyo, Adili Haruni Nyaluke alisema wahitimu ambao wote ni watoto wa kike walioanza masomo yao mwaka 2014 wakiwa 54 lakini kutokana na changamoto mbalimbali ni wasichana hao 29 tu waliofanikiwa kuhitimu masomo. 

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Agape AIDS Control Programme (AACP), linalomiliki shule hiyo, John Myola alisema mahafali hayo ya kwanza ni ya watoto wa kike ambao wengi wao wamepoteza wazazi kutokana na ukimwi na waliookolewa kutoka katika ndoa na mimba za utotoni na kurudishwa shuleni kupitia mfumo wa elimu usio rasmi wa masafa au elimu ya watu wazima. 

Myola aliwataka wazazi na walezi kuwasaidia watoto hao pindi watakaporudi nyumbani kusubiri matokeo ya kidato cha nne na kukumbusha kwa wahitimu hao hawarudi nyumbani kuolewa.

“Wanaporudi nyumbani siyo kwamba wanarudi kuolewa, bado hawajamaliza masomo, watoto hawa wana uwezo mkubwa darasani, tuna imani watafaulu vyema katika mtihani wao, mnachotakiwa kufanya ni kuwalea katika ustawi unaotakiwa, msiwaache peke yao, msiwaozeshe”, alisema Myola. 

Katika risala yao  wahitimu hao walisema elimu waliyoipata imewapatia msingi mzuri wa kujiunga na elimu ya juu lakini pia imewajengea uwezo mzuri wa kujitambua, kufikiri, kufanya maamuzi sahihi na mambo kadhaa ikiwemo elimu ya ujasiriamali, stadi za maisha na stadi za kazi na afya ya uzazi. 

Wahitimu hao waliomba mamlaka zinazohusika kuhakikisha kesi za watoto wa kike wanaopatiwa mimba udogoni, kuozeshwa mapema, kubakwa, kupigwa na kutelekezwa zinapofikshwa katika vyombo vya sheria haki zisimamiwe ipasavyo na haki  itendeke, wakisema kuwa kesi nyingi za aina hiyo zimekuwa zikichezewa sana na kuwa na mwisho mbaya. 

Wahitimu hao pia walitaka wazazi wanaolazimisha watoto kuolewe na wanaume wanaotia mimba wapatiwe adhabu kali na wanapofikishwa mahakamani kesi zao zisichukue muda mrefu kama sheria zinavyoelekeza. 

Aidha waliyaomba mashirika mbalimbali kushirikiana na shirika la AGAPE linalomjali, kumlinda, kumthamini na kumsaidia mtoto wa kike katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, ndoa na mimba za utotoni mkoani Shinyanga. 

James Malima alisema serikali inatambua jitihada mbalimbali zinazofanywa na shirika la AGAPE katika kumkomboa mototo wa kike kielimu na kuahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana nao bega kwa bega ili kuhakikisha kuwa watoto wa kike wanapata elimu. 

“Watoto wa kike wanapitia changamoto nyingi, kinachotakiwa wazazi na walezi pamoja na jamii kwa ujumla tushirikiane kuwalinda watoto wa kike na tuwapatie elimu, mtoto anapaswa kwenda shule siyo kuozeshwa au kuwapeleka kwenda kufanya kazi za ndani", alionya. PICHA ZA MAHAFALI- BOFYA HAPA

VIDEO: UJENZI WA BANDARI BAGAMOYO KUANZA HIVI KARIBUNI

SERIKALI YAMWAGA AJIRA 400 TRA


Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu 
SHINYANGA, TANZANIA
Serikali inatarajia kuajiri wafanyakazi 400 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kipindi kifupi kijacho ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi katika Mamlaka hayo, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi na makusanyo ya kodi.

Ahadi hiyo imetolewa Mjini Shinyanga na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utendaji wa Mamlaka hayo mkoani humo.

Dkt. Kijaji amesema kuwa taratibu zote zimekamilika na wakati wowote nafasi za ajira zitatangazwa na kwamba nafasi hizo zimelenga kuiwezesha TRA kuwafikia watu wengi zaidi na kuongeza wigo wa makusanyo ya kodi.

“Tunatambua changamoto ya uchache wa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA ndio maana tumeamua kuajiri wafanyakazi hao 400 ambao ni wengi kuliko kada nyingine ili tuweze kuimarisha utendajikazi wa Mamlaka na hivyo kuongeza makusanyo ya kodi zinazotakiwa kwa shughuli za maendeleo nchini” alisema Dkt. Kijaji

Alisema kuwa pamoja na uhaba wa watumishi, anaamini kuwa lengo la mwaka huu la kukusanya shilingi trilioni 17 ambazo Mamlaka hayo imepangiwa yatafikiwa na ikiwezekana kuzidi kwa kutumia wafanyakazi waliopo.

Dkt. Kijaji alitoa rai kwa wafanyakazi wa TRA kuwa waadilifu na kwamba atakayebainika kukiuka maadili yake ya kazi atachukuliwa hatua kali za kinidhamu na kisheria.

Awali Meneja wa Mamlaka ya Mapato mkoa wa Shinyanga Bw. Jumbe Samson, alieleza kuwa mkoa wake umepangiwa lengo la kukusanya Shilingi bilioni 18 na kwamba wanauhakika wa kufikia lengo hilo kutokana na mikakati mbalimbali waliyojipangia ikiwemo kusimamia ukusanyaji kodi kikamilifu katika sekta ya madini.

Kwa upande wake, Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA Bw. Beatus Nchota alisema kuwa Mamlaka yake imejiwekea mipango ya kufungua ofisi zake kila wilaya hapa nchini ili kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali ili lengo walilopewa la kukusanya shilingi trilioni 17 liweze kufikiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Bi. Josephine Matiro, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, alisema kuwa Serikali mkoani humo itahakikisha kuwa TRA inatimiza malengo yake ya kukusanya kodi na kumhakikishia Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji kwamba watasimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na watumishi wengine wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Shinyanga, alipofanya ziara ya kikazi kukagua namna Mamlaka hayo inavyokusanya kodi. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)​

RAIS DK. MAGUFULI ATUMA SALAM ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA ASKOFU MSEMWA

Oct 20, 2017

RAIS DK. JOHN MAGUFULI
IKULU, DAR ES ASALAAM
Rais Dk. John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Mhashamu Tercisius Ngalalekumtwa kufuatia kifo cha Askofu wa Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi Mhashamu Castory Msemwa, kilichotokea jana Oktoba 19, 2017 nchini Oman.

Mhashamu Askofu Castory Msemwa amefariki dunia Mjini Muscat akiwa safarini kuelekea nchini India kwa Matibabu.

"Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Baba Askofu Msemwa, kilichotokea huko Oman, Baba Askofu Msemwa ametoa mchango mkubwa sio tu katika kutimiza majukumu yake ya huduma za kiroho bali pia katika kuisaidia jamii kupata huduma mbalimbali anazostahili binadamu na amekuwa akitoa ushirikiano mkubwa kwa taasisi nyingine zikiwemo za Serikali katika kudumisha amani, upendo, umoja na kuwahudumia wananchi, mchango wake utakumbukwa daima" Taarifa iliyotolewa na Ikulu jijini Dar es Salaam, imemkariri Rais Dk Magufuli akisema.

Taarifa hiyo imesema, Rais Magufuli amemuomba Rais wa TEC Mhashamu Tercisius Ngalalekumtwa kumfikishia pole nyingi kwa Maaskofu wote wa TEC, Mapadre, Makatekista na waumini wote wa Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi kwa msiba huu mkubwa uliotokea na amesema anaungana nao katika kipindi cha majonzi na maombi kwa Marehemu.

"Raha ya milele umpe ee Bwana na mwanga wa milele umuangazie, Marehemu Askofu Castory Msemwa apumzike kwa amani, Amina"  Amemalizia Rais Magufuli.

SPIKA NDUGAI AKUTANA NA KIONGOZI WA CHAMA CHA KIKOMUNISTI CHA URUSI NA KIONGOZI WA BUNGE LA NCHI HIYO

 Spika wa Bunge, Job Ndugai (kushoto) akivishwa nishani maalum ya maadhimisho ya miaka 100 ya Mapinduzi Makuu ya Urusi na Kiongozi wa Chama cha kikomunisti cha Urusi, Komredi Gennady Zyuganov ambae ni Kiongozi wa Chama cha Kikomunisti cha Urusi na kiongozi wa Bunge la nchi hiyo, Spika alipotembea leo ofisini kwa kionhozi huyo akiwa Urusi ambako anashiriki Mkutano wa 137 wa Chama cha Mabunge Duniani.
 Spika wa Bunge Job Ndugai (kushoto) akimkabidhi zawadi Kiongozi wa Chama cha Kikomunisti cha Urusi na kiongozi wa Bunge la nchi hiyo Komredi Gennady Zyuganov, alipomtembelea ofisini kwa kiongozi huyo. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini humo, Jenerali Mstaafu Wynjones kisamba. Spika Ndugai yupo nchini Urusi kushiriki mkutano wa 137 wa Chama cha Mabunge Duniani
Spika wa Bunge, Job Ndugai (wa pili kulia)akifanya mazungumzo na Kiongozi wa Chama cha Kikomunisti cha Urusi na kiongozi wa Bunge la nchi hiyo, Komredi Gennady Zyuganov (wa pili kushoto) alipomtembelea leo ofisini kwa kiongozi huyo katika maadhimisho ya miaka 100 ya Mapinduzi Makuu ya Urusi. Spika Ndugai yupo nchini Urusi, akishiriki Mkutano wa 137 wa Chama cha Mabunge Duniani unaoendelea Jijini St. Petersburg, Urusi

DKT MWANJELWA: TUMIENI USHIRIKA KUPIGA VITA ADUI NJAA, UJINGA, MARADHI NA UMASKINI

Naibu Waziri Wizara ya Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa akiangalia sehemu ya bidhaa za chakula zilizosindikwa kutoka katika Vikundi vilivyoanzishwa chini ya  Ushirika wa Akiba na Mikopo wa TANESCO (TANESCO - SACCOS) katika Viwanja vya Chuo cha Mipango wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya SACCOS, Mkoani DodomaNaibu Waziri – Wizara ya Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa akinunua dagaa walioongezwa thamani kutoka kwa kina Mama wa MWACIWOTE SACCOS ya  Jijini Mwanza. SACCOS hiyo imeundwa na kina Mama Waalimu wa Shule za Msingi na SekondariMgeni Rasmi, Naibu Waziri – Wizara ya Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa akipa maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Ngome SACCOS Brigedia Jenerali Charo Hussein Yateri namna ambavyo inajiendesha kwa mafanikio makubwa ikiwa na Wanachama zaidi ya 12,500 nchini katika Viwanja vya Chuo cha Mipango wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya SACCOS inayoadhimishwa Kitaifa Mkoani DodomaMgeni Rasmi, Naibu Waziri – Wizara ya Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa akipa maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa TANESCO SACCOS Bibi Somoe Ismail namna ambavyo inajiendesha kwa mafanikio makubwa ikiwa na Wanachama zaidi ya 5,612 nchini kote katika Viwanja vya Chuo cha Mipango wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya SACCOS inayoadhimishwa Kitaifa Mkoani Dodoma
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa amewataka Washiriki wa Mkutano wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS), kuvitumia Vyama hivyo kama silaha ya kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo ya kweli.
Dkt. Mary Mwanjelwa ambaye ndiye mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya kuadhimisha Uanzishwaji wa Vyama vya Akiba na Mikopo amesema hakuna ubishi kuwa mafanikio yaliyopatikana kupitia Vyama hivyo yanadhihirisha kuwa ni njia madhubuti ya Wananchi katika kupambana na adui njaa, ujinga, maradhi na umaskini.
Dkt. Mwanjelwa amekaririwa akisema “Nimetembelea mabanda kadhaa ya Vyama vya Akiba na Mikopo kutoka Taasisi za Umma kama Ngome SACCOS, TANESCO SACCOS, Bandali SACCOS, wameniambia kiasi cha mitaji waliyonayo ni unazungumzia mabilioni ya Shilingi za Kizanzania, ambapo Wanachama wanakopeshana kwa riba nafuu na kwa muda mzuri”
“Jambo hilo linatia moyo na niwaombe Viongozi na ninyi Wanachama ambao mmejiunga kwenye Vyama vya Akiba na Mikopo kuwahamasisha wengine kujiunga na Vyama vya Akiba na Mikopo ili tuongeze wigo wa idadi kubwa ya Watanzania”. Amekaririwa Naibu Waziri.
“Na kama Watanzania wengi watajiunga basi tutakuwa na nafasi kubwa kama Taifa kupambana na maadui hawa watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini”. Amekaririwa Naibu Waziri Dkt. Mwanjelwa.
Aidha, Naibu Waziri, Dkt. Mwanjelwa ameuagiza Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini Bwana Tito Haule, kuhakikisha anaitumia nafasi ya kuelimisha umma kuhusu faida na uzuri wa USHIRIKA kupitia Vyama vya Kuweka na Kukopa kama ndiyo silaha ya kupeleka mbele maendeleo ya Ushirika nchi.
“Mrajis elimu kwa Umma ni jambo la muhim sana, hata kama mnafanya mambo mazuri lakini kama Wananchi hawatafahamu kuhusu faida na mambo mazuri yanayohusu kujiunga na Vyama vya Akiba na Mikopo itakuwa ni kazi bure, fanyeni kila linalowezekana ili kuwaelimisha Watanzania”.
Dkt. Mwanjelwa ameongeza kuwa USHIRIKA pia ni njia ya kuongeza tija na uzalishaji katika mazao ya kilimo na kwa njia hiyo, uzalisahaji wa mazao ya kilimo kwa ajili ya viwanda vya kati na vikubwa unaweza kuongezeka kwa kutumia Vyama vya Akiba na Mikopo.
“Msisahau kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamilia katika kulifikisha Taifa kwenye uchumi wa viwanda na Watanzania wengi wanaojihusisha na Sekta ya Kilimo ni zaidi ya asilimia 75 kwa maana hiyo, Vyama vya Akiba na Mikopo pia vitumike katika kuongeza tija na uzalishaji wa malighafi za viwanda vya usindikaji vidogo, vya kati na vikubwa”. Amemalizia Dkt. Mary Mwanjelwa.
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) yalianza rasmi jana tarehe 18 Oktoba na yanafikia kilele leo tarehe 19 Oktoba, 2017 katika Ukumbi wa Chuo cha Mipango, Mjini Dodoma.

MAGAZETI YA LEO OKTOBA 20, 2017

MAJADILIANO YA MAKINIKIA YAMALIZIKA KWA MAFANIKIO MAKUBWA

Oct 19, 2017

Rais Dk. John Magufuli, akishuhudia wakati Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi (Wapili kushoto) na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick Gold, Prof. John Thornton (wapili kulia) wakitia saini ripoti ya majadiliano kati ya Tanzania na Kampuni hiyo, Ikulu jijini Dar es Salaam, leo. Kulia ni Ofisa uendeshaji wa Barrick Richard William  na kushoto ni Mmoja wa waliokuwa wawakilishi wa Tanzana katika majadiliano hayo Prof. Florens Luoga.
-------------------------------------------------------------------------------------- DAR ES SALAAM, TANZANIA
Majadiliano kati ya Tanzania na timu ya wawakilishi wa kampuni ya Barrick Gold inayomiliki migodi ya madini hapa nchini yamekamilika na makubaliano kati ya pande hizo yametiwa saini leo19 Oktoba 19, 2017 mbele ya Rais Dk. Johne Magufuli Ikulu, Jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu imesema timu ya Barrick Gold Corporation imeongozwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni hiyo Prof. John Thornton wakati timu iliyowakilisha Serikali ya Tanzania imeongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi.

Miongozi mwa mambo waliyokubaliana ni kutekeleza mwelekeo mpya wa biashara ya madini ambapo kutakuwa na mgawanyo sawa wa faida (yaani Tanzania kupata asilimia 50 na Barrick Gold Corporation kupata asilimia 50 ya faida) na kuundwa kwa kampuni ya ubia wa usimamizi wa migodi ya madini iliyopo Tanzania ambayo itakuwa na makao makuu yake Mwanza na ofisi ndogo Dar es Salaam nchini Tanzania badala ya nchini Uingereza.

Mengine ni kufunga ofisi za uhasibu na fedha zilizopo Johannesburg Afrika Kusini na kuhamishia Tanzania na kutekeleza masharti yote ya mabadiliko ya sheria mpya ya madini na rasilimali za nchi ya mwaka 2017.

Aidha, Barrick Gold Corporation imekubali kuwepo kwa wawakilishi wa Serikali katika bodi za migodi yake yote hapa nchini, kazi mbalimbali za kwenye migodi kufanywa na kampuni za Kitanzania, Migodi kutoa ajira za kudumu kwa wachimbaji, wachimbaji hao kuishi majumbani kwao badala ya kuishi kwenye makambi ya migodi na mashauri yote ya kesi mbalimbali kufanywa hapa nchini.

Kampuni ya Barrick Gold pia imekubali kutoa Dola za Kimarekani Milioni 300 sawa na takribani Shilingi Bilioni 700 kama malipo ya kuonesha nia njema ya kufidia fedha zilizotokana na upotevu wa mapato kupitia biashara ya kampuni hiyo.

Akizungumza baada ya kutia saini makubaliano hayo Prof. Thornton amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa msimamo wake unaojenga misingi ya biashara ya kuaminiana na uwazi, ambayo ni muhimu na ya namna yake kwa biashara katika karne hii ya 21.

Prof. Thornton amesema Barrick Gold Corporation watazingatia makubaliano haya na wanaamini kuwa yamefungua ukurasa muhimu utakaowezesha kufanya biashara kisasa.

Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amezipongeza timu zote mbili yaani Tanzania na Barrick Gold Corporation kwa kazi kubwa ziliyofanya kufikia makubaliano hayo na kwa kipekee amempongeza Prof. Thornton kwa nia yake thabiti ya kukubali kufanyika kwa mazungumzo na kukubali mambo yaliyofikiwa.

Mhe. Rais Magufuli amesema makubaliano hayo yataisaidia nchi kuzalishaji ajira zaidi, kupata manufaa mbalimbali yanayostahili ikiwemo fedha za kugharamia huduma za kijamii kwa wananchi na yanajenga msingi imara ambao utaiwezesha Tanzania kunufaika na rasilimali zake za madini.

Mhe. Dkt. Magufuli amemuagiza Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Kabudi kuunda timu zitakazoshughulikia biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi pamoja na migodi mingine ya dhahabu haraka iwezekanavyo ili nchi iweze kunufaika ipasavyo.

“Nataka machimbo yote ya dhahabu mchakato kama huu ufanyike, pia nakuagiza Prof. Kabudi biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi nako ni lazima kufuate utaratibu huu, asiyetaka aondoke” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Pia Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi hizi badala ya baadhi yao kuzibeza kwa kuwa zina manufaa kwa taifa na wananchi wake.

Dk.SHEIN AMUAPISHA NAIBU MKUU WA KMKM

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto) akimuapisha Naibu Mkuu wa Kikosi Maalum cha kuzuiya Magendo KMKM Kapteni Khamis Simba Khamis katika hafla iliyofanyika leo katika Ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar, leo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Makamanda wa Vikosi vya Ulinzi baada ya kumuapisha Naibu Mkuu wa Kikosi Maalum cha kuzuiya Magendo KMKM Kapteni Khamis Simba Khamis (wa pili kulia) katika hafla iliyofanyika leo katika Ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar

UJUMBE WA USAID YA MAREKANI WAIPONGEZA TANZANIA

Binagi Media Group
Mapambano dhidi ya ugongwa hatari wa Malaria yameendelea kuonyesha mafanikio mkoani Mwanza, baada ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huo kupungua kutoka asilimia 19.01 mwaka 2011/12 hadi asilimia 15.1 mwaka 2015/16.


Hiyo ni kutokana na juhudi za serikali kupambana na ugonjwa huo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo shirika la misaada la watu wa Marekani USAID ambalo limeendelea kusaidia vyandarua vyenye kinga kwa ajili ya mapambano dhidi ya malaria.

Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza, Dkt.Leonard Subi aliyasema hayo jana wakati wa zoezi la kugawa vyandarua bure katika shule ya Msingi Senge iliyopo Kata ya Bujashi wilayani Magu ambalo lilishuhudiwa pia na ujumbe kutoka USAID Marekani.

Alisema mbali na kuua vimelea vya Malaria kwa kutumia viuatilifu, pia serikali inagawa vyandarua bure katika shule za msingi, vituo vya afya, zahanati pamoja na hospitali ili kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Monica Ngalula pamoja na Marco Yusuph ni baadhi ya wanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya msingi Sese, walishukuru kwa kugawiwa vyandarua hivyo na kwamba vitawasaidia wasing’atwe na mbu wa Malaria wakiwa wamelala nyumbani kama ilivyokuwa hapo awali.

Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka USAID, Chriss Thomas alifurahishwa na juhudi za Tanzania kupambana na ugonjwa wa Malaria na kuahidi ushirikiano zaidi wa kusaidia mapambano hayo ili kuokoa maisha ya watu hususani akina mama wajawazito pamoja na watoto ambao wamekuwa kwenye hatari ya kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Mganga Mkuu mkoani Mwanza, Dkt.Leonard Subi
Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka USAID, Chriss Thomas akizungumza na wanahabari
Ujumbe kutoka USAID Marekani ukiwa shule ya msingi Sese wilayani Magu kushuhudia zoezi la ugawaji vyandarua
Mwanafunzi wa shule ya msingi Sese akipokea chandarua kutoka USAID
Mwanafunzi wa shule ya msingi Sese akipokea chandarua kutoka USAID
Ugeni kutoka USAID Marekani
Shule ya msingi Sese wilayani Magu ni miongoni mwa shule za msingi 941 ambazo wanafunzi wake wananufaika na zoezi la ugawaji vyandarua bure mkoani Mwanza.

MKURUGENZI WA ILEJE ATEMBELEA KILWA

Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Christopher Ngubiagai kulia akisalimiana na mkurugezi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Mkoani Songwe, Haji Mnasi ,mara baada ya Mkurugenzi huyo kufika ofisini kwake jana kwaajili ya kumsalimu  kushoto ni Mkurugenzi  wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi Zabron Bugingo(Picha na Pamela Mollel Kilwa)
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Christopher Ngubiagai kulia akisalimiana na mkurugezi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Zablon Bugingo katikatimkurugezi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Mkoani Songwe  

AMUUA MWENZAKE KWA ULEVI CHALINZE MKOA WA PWANI

Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Mfugaji Lemandra Kishakwi (35) mkazi wa Chamakweza, Chalinze mkoani Pwani, ameuawa kwa kuchomwa kisu maeneo mbalimbali ya mwili na mwenzake Niniyay Silongoy chanzo kikidaiwa ni ulevi.

Aidha jeshi la polisi mkoani hapo, limekamata bangi gunia saba zikiwa kwenye mifuko ya salfet ambazo zina uzito wa kg 7,500 .

Kamanda wa polisi mkoa wa Pwani ,(ACP)Jonathan Shanna akielezea tukio la mauaji alisema limetokea octoba 18 majira ya saa 11.30 jioni,huko Chamakweza.

Alisema kuwa ,Lemandra ambae ni (mmasai )mfugaji aliuawa kwa kuchomwa kisu maeneo ya kwapa la kushoto ,shingoni na mkono wa kulia wakati wakiwa kwenye ulevi.

Kamanda Shanna ,alielezea mtuhumiwa alikimbia kusikojulikana baada ya kufanya tukio hilo na polisi inaendelea na juhudi za kumtafuta .

Mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu wa marehemu mara baada ya uchunguzi wa daktari kukamilika.

Akielezea kuhusiana na tukio la kukamata bangi ,kamanda Shanna alisema askari wakiwa doria eneo la Kwamatias Kibaha ,walipata taarifa kuwa kuna ajali ya gari no.T847 DHT aina ya I.S.T.

"Walipofika eneo la tukio waliwaokoa majeruhi Gudluck Kundaeli Mbowe (24)mkazi wa Kiwalani jijini Dar es salaam aliyekuwa dereva wa gari hilo na Ally Mtena (28) mkazi wa Gongolamboto "

"Wakati wanapekua gari hilo waliikuta ikiwa na gunia saba za bangi zikiwa kwenye salfet ,zenye uzito wa kg 7,500.:";

Kamanda huyo wa polisi mkoani humo ,alibainisha watuhumiwa wamekamatwa ili kuweza kuchukuliwa hatua za kisheria .

MAGAZETI YA NDANI NA NJE YA TANZANIA LEO OCT 19,2017


Magazeti zaidi>Bofya Hapa

MBIO ZA TIGO DODOMA HALF MARATHON ZAZINDULIWA RASM


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana akizungumza na waandishi wa habari anayefuatia ni Kaimu Meneja wa Tigo Kanda ya Kaskazini Henry Kinabo na mwisho ni Mkurungenzi Mtendaji wa Vision Investment, Ally Nchahaga wakizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi rasmi wa mbio ndefu za Dodoma almaarufu Dodoma Marathon. Mbio hizo zimethaminiwa na Tigo Tanzania na zinatarajiwa kufanyika jijini Dodoma mwezi  Novemba mwaka huu
Katibu wa Chama cha Riadha Mkoa wa Dodoma Robert Mabonye , Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana ,Kaimu Meneja wa Tigo Kanda ya Kaskazini Henry Kinabo na Mkurungenzi Mtendaji wa Vision Investment, Ally Nchahaga wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi rasmi wa mbio ndefu za Dodoma almaarufu Dodoma Marathon. Mbio hizo zimethaminiwa na Tigo Tanzania na zinatarajiwa kufanyika jijini Dodoma  mwezi Novemba mwaka huu.

Waandishi wa habari wakichukua matukio katika atika uzinduzi rasmi wa mbio ndefu za Dodoma almaarufu Dodoma Marathon. Mbio hizo zimethaminiwa na Tigo Tanzania na zinatarajiwa kufanyika jijini Dodoma  mwezi Novemba mwaka huu.

ยช