Serikali ya Burundi imeanza kuwaondoa
wanajeshi wake wanaohudumu katika Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa
Afrika nchini Somalia Amisom kutokana na mgogoro wa mshahara.
Gaston Sindimwo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Burundi amesema
kuwa, serikali ya Bujumbura imeamua kutekeleza maamuzi hayo magumu
kutokana na kutotiliwa maanani ombi lake la kutaka kadhia ya mishahara
na marupurupu ya wanajeshi wake walioko Somalia itatuliwe haraka
iwezekanavyo. Sindimwo amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema
kuwa: "Tungependa kuendelea kusaidia mchakato wa kurejesha amani na
uthabiti nchini Somalia, lakini tunalazimika kuanza kuwaondoa askari
wetu kwa kuwa hawajalipwa mishahara na marupurupu yao kwa zaidi ya miezi
12 sasa."
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi ambaye mwezi uliopita alitishia
kuwaondoa wanajeshi wa nchi yake walioko Somalia iwapo askari hao
hawangelipwa mishahara yao kufikia mwezi huu, sasa amewaagiza mawaziri
wa mambo ya nje na ulinzi wa nchi hiyo kuanzisha mchakato wa kuwaondoa
wanajeshi wa nchi hiyo Somalia. Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Disemba,
Rais Nkurunziza alisema nchi hiyo itaushtaki Umoja wa Afrika katika
vyombo vya mahakama vya kimataifa kwa kukiuka muafaka uliofikiwa na
pande zote kuhusiana na mishahara ya askari wa Amisom.
Burundi ambayo ina askari 5,432 ndani ya Amisom, ni nchi ya pili
baada ya Uganda kwa kuwa na idadi kubwa ya askari wa kulinda amani
nchini Somalia. Kikosi hicho kimetumwa Somalia lengo likiwa ni kuendesha
mapambano ya kulitokomeza kundi la kigaidi la wanamgambo wa al Shabab
ambalo linataka kuipindua serikali kuu ya Somalia.
Amisom ilijikuta katika kipindi kigumu cha kuwalipa mishahara
wanajeshi zaidi ya 22 elfu wa nchi za Afrika zilizotuma askari wake
Somalia zikiwa ni pamoja na Kenya, Ethiopia na Djibouti, baada ya Umoja
wa Ulaya EU kupunguza bajeti yake kwa kikosi hicho cha kulinda amani,
kwa asilimia 20 mapema mwaka huu.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269