Breaking News

Your Ad Spot

Jan 27, 2017

MAMA SAMIA AZINDUA JENGO JIPYA LA UBALOZI WA INDIA JIJINI DAR ES SALAAM

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan (kushoto) akiweka jiwe la msingi la ufunguzi wa jengo jipya la Ubalozi wa India lililopo mtaa wa Shaaban Robert jijini Dar es Salaam
Balozi wa India hapa nchini Bw. Sandeep Arya (wa pili kushoto) akimuonesha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan picha mbali mbali zenye kuonyesha historia ya urafiki baina ya Tanzania na India wakati wa ufunguzi wa jengo jipya la ubalozi wa India jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa ufunguzi wa Jengo jipya la Ubalozi wa India hapa nchini.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa ufunguzi wa Jengo jipya la Ubalozi wa India lililopo mtaa wa Shaaban Robert jijini Dar es Salaam.
Balozi wa India hapa nchini Bw. Sandeep Arya akihutubia wakati wa uzinduzi wa Jengo jipya la Ubalozi wa India hapa nchini.
Vikundi vya Utamaduni wa Kihindi vikionyesha uwezo wa kuzicheza ngoma za asili.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassana ameishukuru Serikali ya India kwa ufadhili wake wa miradi ya maji katika miji 17 nchi ambayo inalenga kupunguza tatizo la maji kwa wananchi wengi nchini.

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam katika hafla ya Maadhimisho ya miaka 68 ya Siku ya Kitaifa ya Jamhuri ya India sherehe ambazo zimeambatana na Uzinduzi rasmi wa majengo ya ofisi mpya ya Ubalozi wa India hapa nchini.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema ufadhili wa miradi ya Maji pamoja na miradi mingine unaofanywa na Serikali ya India kwa Tanzania Bara na Zanzibar unadhihirisha wazi mahusiano mazuri yaliyopo yaliyoasisiwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mahatma Gandhi wa India.

Makamu wa Rais amesisitiza kuwa India ni moja ya washirika muhimu katika juhudi za kuwaletea wananchi maendeleo na Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu katika maeneo mengi ikiwemo ya kikanda na kimataifa kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa pande Mbili yaani Tanzania na India.

Amesema kwa miaka mingi sasa mahusiano ya kindugu yamekuwa yaakiimarika katika sekta mbalimbali ikiwemo kisiasa,kidiplomasia,kibiashara, masuala ulinzi, utamaduni na mwingiliano wa watu na watu.

Makamu wa Rais pia ameishukuru Serikali ya India kwa msaada wake wa shilingi milioni 500 alioutoa kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera ambao walikubwa na tetemeko la ardhi mwaka jana.

Ameeleza kuwa Mahusiano kati ya India na Tanzania yamekuwa na manufaa makubwa ambapo idadi kubwa ya watanzania wanaenda kupata mafunzo mbalimbali nchini India hasa Madaktari na wamekuwa msaada mkubwa katika kuokoa maisha ya Watanzania.

Katika hafla hiyo, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye hotuba yake alitoa salamu za rambirambi kwa Serikali ya India kufuatia ajali ya treni iliyotokea katika Jimbo la Andhra Pradesh na kusababisha vifo vya watu 30 na kujeruhi wengine.

“Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania napenda kutoka salamu za Pole kwa familia za wafiwa na majeruhi katika kipindi hiki kigumu kwa kumwomba Mwenyezi Mungu azipumzishe roho za marehemu mahali pema peponi na tunawaombea majeruhi wapone haraka. ’’

Kwa upande wake, Balozi wa India hapa nchini Sandeep Arya amemhakikishia Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Serikali ya India itaendelea kudumisha na kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa pande zote Mbili.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages