Breaking News

Your Ad Spot

Jan 19, 2017

KITENGO CHA KUMALIZA MALARIA ZANZIBAR CHAFANYA MKUTANO WA WADAU KUTATHMINI HALI YA MARADHI HAYO ILIVYO KWA SASA

zab1
Meneja Kitengo cha kumaliza Malaria Zanzibar Abdalla Suleiman Ali akifungua mkutano wa siku moja wa wadau wa Malaria uliofanyika Hoteli ya Ocean View Kilimani Mjini Zanzibar.
zab2
Afisa uchunguzi wa vimelea vya Malaria Zanzibar Safia Mohammed Ali akiwasilisha mada ya njia za kukabiliana na maradhi hayo katika mkutano wa wadau wa Malaria uliofanyika Hoteli ya Ocean View Kilimani .
zab3
Naibu Meneja wa ZAMEP Faiza Bwanakheri akitoa mada ya njia za kudhjibiti na kumaliza Malaria Zanzibar katika mkutano wa wadau wa Malaria uliofanyika Hoteli ya Ocean View.
zab4
Baadhi ya wadau wa Malaria walioshiriki mkutano wa siku moja katika Hoteli ya Ocean View wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa katika mkutano huo.(Picha na Makame Mshenga).

Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar  
Meneja Kitengo cha kumaliza Malaria Zanzibar Abdalla Suleiman Ali amesema mashirikiano ya pamoja yanahitajika kuanzia ngazi ya shehia hadi Taifa katika kufikia malengo ya kumaliza maradhi hayo nchini.

Alisema kazi ya kumaliza  Malaria Zanzibar sio kazi rahisi kama inavyofikiriwa na watu wengi lakini nguvu za pamoja za wadau mbali mbali wa ndani na nje ya nchi zinahitajika.
Meneja Abdalla Suleiman alieleza hayo katika mkutano wa siku moja wa wadau wa Malaria uliozungumzia hali ya ugonjwa huo ulivyo hivi sasa na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kupitia kitengo hicho uliofanyika Hoteli ya Ocean View Kilimani Mjini Zanzibar.


Alisema pamoja na Zanzibar kupata mafanikio makubwa katika kukabiliana na Malaria bado zipo baadhi ya sehemu maradhi hayo yanaendelea kujitokeza na ni vigumu kukabiliana nayo kwa vile kunahitajika ufuatiliaji wa karibu kwenye familia zinazotoka wagonjwa hao.

Aliongeza kuwa kabla ya kuanzishwa kitengo cha kumaliza Malaria, Zanzibar ilifikia kuwa na wagonjwa zaidi ya laki tatu  kwa mwaka  lakini hivi sasa wagonjwa  wa malaria hawazidi elfu nne kwa mwaka.

Alisisitiza kuwa lengo la Wizara ya Afya kupitia Kitengo cha kumaliza Malaria ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2022 Zanzibar hakuna mtu anaeugua Malaria.

Akitoa mada ya hali ya Malaria ilivyo hivi sasa, Ofisa wa  Kitengo hicho Wahida Shirazi alisema Kisiwa cha Unguja kunawagonjwa wengi zaidi wa maradhi hayo ukilinganisha na Pemba na Wilaya ya Kati inaongoza kwa wagonjwa wengi ikifuatiwa na Wilaya za Magharibi.

Alikumbusha kuwa Wilaya ya Chake Chake inaongoza kwa kuwa na wagonjwa kidogo zaidi wa Malaria na baadhi ya shehia za Wilaya hiyo hazijatoa mgonjwa hata mmoja kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Hata hivyo Ofisa huyo alisema Kitengo cha kumaliza Malaria Zanzibar kimegundua wagonjwa wengi wa malaria hivi sasa ni wenye tabia ya kusafiri mara kwa mara nje ya Zanzibar na wanaamini wanapata ugonjwa huo wakati wa safari zao.

Akizungumzia umuhimu wa kutumia vyandarua katika kupambana na Malari Afisa wa Kitengo hicho Mwinyi Khamis alisema iwapo vitatumika vizuri vinaepusha maradhi hayo kwa asilimia sitini hivyo amewashauri wananchi kuendelea kuvitumia kikamilifu.

Baadhi ya wadau walioshiriki mkutano huo walikishauri kitengo cha kumaliza mlaria  kutoa elimu zaidi kwa wananchi wanaokataa nyumba zao kupigiwa dawa badala ya kuviachia vyombo vya dola kutumia nguvu kukamililsha kazi hiyo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages