Breaking News

Your Ad Spot

Jan 23, 2017

MATAPELI YA KUTUMIA SIMU ZA MKONONI YACHARUKA, SERIKALI YAWATAKA WANANCHI KUKAA CHONJO

**KATI YA NOVEMBA NA DESEMBA 2016, ILIFANYIKA MIAMALA YA
SH. TRILIONI 13.07 KWA SIMU
Na Fatma Salum- MAELEZO
Serikali imewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya utapeli unaofanywa kwa kutumia simu za mkononi.

Imesema, utapeli huo umezidi kuongezeka kutokana na miamala ya fedha kwa simu za mkononi nayo kuongezeka kwa kiasi kikubwa akitoa mfano kuwa kati ya Novemba na Desemba mwaka jana pekee,  jumla ya fedha zilizopita kwenye mitandao ya simu za mkononi ilifikia kisi cha sh. trilioni 13.07.

Akizungumza na Waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, leo, Kaimu Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala amesema kuna ongezeko kubwa la matapeli wanaoghushi utaratibu wa mawasiliano na kuwalaghai watu kutuma pesa kwa simu za mkononi.

Amesema, pamoja na kutahadharisha kwananchi, Serikali kupitia TCRA na vyombo vya usalama vinalishughulikia tatizo hilo, ili kuweza kukabiliana nalo kwa nguvu zake zote.

“Usitekeleze maagizo yoyote yanayohusu fedha kwa mawasiliano ya simu hata kama yanatoka kwa mtu unayemfahamu, mpigie aliyekutumia ujumbe kwa namba nyingine ili kuthibitisha’’ alifafanua Semu.

Alitahadharisha kuwa mtu akipokea taarifa kwa njia ya simu au ujumbe mfupi wa maandishi kuwa ametumiwa fedha kimakosa na kutakiwa kuzirudisha asifanye hivyo mpaka atakapojiridhisha na uhalali wa taarifa hiyo.

Aidha aliwataka wananchi kutoa taarifa polisi kuhusu matapeli na kuwasilisha malalamiko yao ya huduma za mawasiliano kwa TCRA kupitia sanduku la posta 474 Dar es salaam au wafike kwenye ofisi za TCRA zilizo karibu au wapige simu namba 0784 558270, 0784 558271 na barua pepe (malalamiko@tcra.go.tz)

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages