Breaking News

Your Ad Spot

Jan 18, 2017

MTWARA ICHUNGUZWE SABABU ZA KUFELI KIDATO CHA PILI-MAJALIWA

MAJALIWA CU ELIMU MTWARA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi Wizara wa Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwenda mkoani Mtwara kufanya uchunguzi ili kubaini sababu zilizosababisha shule tisa za mwisho katika matokeo ya kidato cha pili kutoka mkoani humo.
Pia ameziagiza halmashauri nchini kushirikiana na Idara ya Ukaguzi ili kuhakikisha wanawasimamia vizuri walimu jambo litakalowezesha kuboresha ufundishaji na hatimaye kupata matokeo mazuri.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana , Januari 17, 2017 wakati akizungumza na watumishi na wananchi wa mkoa wa Katavi alipowasili Ikulu ndogo ya Mpanda kwa ajili ya kufungua duka la dawa la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda.
Kwa mujibu wa matokeo hayo kati ya shule 10 za sekondari zilizofanya vibaya kwenye mtihani huo, tisa zinatoka katika Mkoa wa Mtwara na moja Tanga. Shule za Mtwara zilizofanya vibaya ni Chingungwe, Malocho, Naputa, Chanikanguo, Mtiniko, Michiga, Msimbati, Salama na Lukodoka huku ya Tanga ikiwa ni Nywelo.
“Viongozi wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) waende Mtwara wakafuatilie kwa kina wajue kuna nini hadi shule tisa kati ya 10 zilizofanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya kidato cha pili mwaka jana zitoke huko,” amesisitiza.
Mbali na kuuagiza huongozi wa wizara hizo kwenda mkoani Mtwara pia Waziri Mkuu amewataka wasimamie vizuri mikoa ambayo awali ilikuwa na matokeo mabaya na sasa inafanya vizuri na wahakikishe shule za mikoa hiyo hazishuki na badala yake ziendelee kupata matokeo mazuri zaidi.
Awali, akisoma taarifa ya mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Mstaafu, Raphael Muhuga alisema katika matokeo ya mtihani kidato cha pili ya mwaka jana mkoa wake ulishika nafasi ya pili kitaifa ukiongozwa na mkoa wa Geita.
Alisema kwa sasa wanajipanga kuhakikisha katika mitihani ya mwaka huu wanashika nafasi ya kwanza kitaifa, hivyo alitoa wito kwa watendaji wa Idara ya Elimu, wakuu wa shule, wazazi na walezi kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha malengo hayo yanafanikiwa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, JANUARI 17, 2017.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages