Breaking News

Your Ad Spot

Jan 26, 2017

RAIS DK MAGUFULI MGENI RASMI SIKU YA SHERIA NCHINI

Benjamin Sawe-Maelezo.
Rais John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Sheria nchini zitakazofanyika mwanzoni mwa mwezi ujao katika viwanja vya Mahakama jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Kaimu Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema mahakama itawaelimisha wananchi jitihada mbalimbali ilizochukua zenye lengo la kuboresha huduma zake kupitia mpango mkakati wa miaka mitano inaoutekeleza katika kutoa haki kwa wakati na kuwezesha ukuaji wa uchumi.

Amesema kabla ya kilele cha maadhimisho hayo, mahakama itafanya matembezi maalum yatakayoongozwa na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi  na yataanzia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuishia katika viwanja vya Mnazi mmoja.

Katika matembezi hayo Rais Mstaafu Mwinyi atazindua rasmi maadhimisho ya wiki ya elimu ya sheria ikiwa ni sehemu ya sherehe za kuelekea maadhimisho ya kilele cha siku ya sheria nchini.

Aidha ametoa rai kwa wananchi kutembelea sehemu zote zilizoandaliwa kwa ajili ya utoaji elimu ya sheria nchini kwa ajili ya kujifunza na kupata huduma mbalimbali za Kisheria.

Alizitaja huduma hizo ni pamoja na taratibu za ufunguaji mashauri katika ngazi mbalimbali za mahakama, taratibu za kesi za mirathi, taratibu za kesi za dhamana, taratibu za rufaa, ndoa na talaka, taratibu za kupokea na kushughulikia malalamiko na Msaada wa Kisheria.

Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini hufanyika kila mwaka mwanzoni mwa mwezi wa pili na mwaka huu yamebeba ujumbe wa Umuhimu wa Utoaji Haki kwa Wakati Kuwezesha Ukuaji wa Uchumi.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages