.

AYATULLAH KHAMENEI AMJIBU TRUMP : IRANI HAIMUOGOPI YEYOTE, MAREKANI ISUBIRI MAJIBU 10 FEBRUARI

Feb 7, 2017

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa taifa la Iran litajibu vitisho vilivyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani katika maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Ijumaa ijayo.
Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei ambaye alikuwa akihutubia maafisa wa kikosi cha Jeshi la Anga la Iran waliokwenda kuonana naye amesema kuwa, matamshi na hatua za Rais mpya wa Marekani zimewadhihirishia waziwazi walimwengu yaliyokuwa yakisemwa na Iran katika kipindi chote cha miaka 38 iliyopita kuhusu ufisadi wa pande zote wa utawala wa Marekani.
Akizungumzia matamshi ya Trump ambaye amesema Iran inapaswa kuishukuru serikali ya rais aliyeondoka madarakani wa Marekani, Barack Obama, Ayatullah Khamenei amehoji akisema: Tutaishukuru kwa kitu gani? Kwa sababu ya kuunda kundi la kigaidi la Daesh? Kuziteketeza nchi za Iraq na Syria au kuunga mkono uhaini wa mwaka 2009 nchini Iran?
Maafsia wa Jeshi la Anga la Iran waliokwenda kuonana na Amiri Jeshi Mkuu
Amesisitiza kuwa, Obama ndiye aliyeliwekea taifa la Iran vikwazo eti vya kulemaza ingawa hakuweza kufikia lengo lake, na hakuna adui yeyote atakayeweza kulilemaza taifa la Iran.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, Donald Trump anapaswa kupongezwa kwa sababu ametusaidia kudhihirisha sura na utambulisho halisi wa Marekani. Amesisitiza kuwa, wakati wa kampeni za uchaguzi wa Rais wa Marekani na baada yake Trump alidhihirisha waziwazi ufisadi wa kisiasa, kiuchumi, kimaadili na kijamii wa mfumo unaotawala Marekani.
Ametilia mkazo udharura wa kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu SW na kutowaamini wala kutegemea mashetani hususan Shetani Mkubwa (Marekani) na kusema: Kutegemea mashetani ni sawa na mtu mwenye kiu anayefuata sarabi akidhania kuwa ni maji.
Mkutano wa leo wa maafsia na wafanyakazi wa Jeshi la Anga la Iran na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu umefanyika kwa mnasaba wa tukio la kihistoria la tarehe 8 Februari 1979 wakati maafisa wa jeshi hilo walipotangaza baia na utiifu wao kwa Imam Ruhullah Khomeini katika kilele cha harakati za Mapainduzi ya Kiislamu mwaka 1979.
Maafisa wa Jeshi la Anga la Iran
Ayatullah Khamenei amelitaja tukio hilo kuwa lilikuwa na uhimu wa aina yake katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Jeshi la Anga la kipindi cha utawala wa taghuti (Shah) lilikuwa na uhusiano wa karibu sana na utawala wa kisiasa uliokuwa tegemezi kwa Marekani na haukudhania kuwa, kamwe ungeweza kupata kipigo kikali kutoka kwa jeshi hilo. 
Ayatullah Khamenei amesema, ni makosa makubwa sana kuwa na imani na mashetani na kuwa na matumaini na wale wanaopinga kuwepo kwa utawala wa Uislamu. 

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช