.

WATU 11 WAUAWA KATIKA MAPIGANO KATIKATI YA DRC

Feb 14, 2017

Watu wasiopungua 11 wameuawa Jumatatu katika eneo la katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya kuzuka mapigano baina ya jeshi la serikali na wanamgambo watiifu kwa chifu wa jadi aliyeuawa mwaka jana.
Kwa mujibu wa Jean Rene Tshimanga, mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiraia ya Kasai, mapigano hayo ya yamejiri karibu na mji wa Tshimbulu, mji ambao jeshi liliua wanagambo 60 siku ya Ijumaa.
Tshimanga amesema bado hajaweza kubaini ni wanagamabo au wanajeshi wangapi waliouawa katika mapigano hayo. Hadi sasa maafisa wa utawala na wale wa jeshi hawajatoa taarifa rasmi kuhusu mapigano hayo.
Chifu Kamuina Nsapu aliuawa mwaka jana na vikosi vya usalama vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Tangu wakati huo, miji kadhaa na vijiji vya mji wa Kasai ya Kati na Kasai ya Mashariki imekuwa ikishuhudiwa vurugu, machafuko na mapigano kati ya vikosi vya kulinda usalama na wanamgambo hao wanaomuunga mkono kiongozi wao wa zamani Kamuina Nsapu.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamekuwa yakishuhudia machafuko kwa zaidi ya miongo miwili sasa na yanahesabiwa kuwa ngome ya makundi ya waasi yakiwemo makundi ya waasi kutoka nje ya nchi hiyo kama LRA, FDLR na ADF-Nalu.
Mapigano yanaripotiwa kukithiri kote Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na hatua ya Rais Joseph Kabila ya kukataa kuondoka madarakani baada ya muhula wake wa urais kumalizika mwezi Disemba mwaka jana.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช