.

NDEGE MBILI ZA BOMBARDIER ZILIZONUNULIWA NA RAIS DK. MAGUFULI ZAINGIZA SH. BILIONI TISA

Mar 31, 2017

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la ATCL, Bw. Lasislaus Matindi anasema wamefanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni 9 kwa katika kipindi cha miezi minne kwa kutumia ndege hizo mbili zilizonunuliwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli, nakuleta utata mkubwa na wapinzani wa siasa nchini waliodai kuwa hazikuwa na tija kwa Taifa.

Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) ilianzishwa mwezi Novemba 2002 baada ya Serikali kubinafsisha lililokuwa Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania Corporation, ATC); katika Shirika hilo, Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) lilinunua hisa asilimia 49 ndani ya ATC. Hata hivyo ubia kati ya ATCL na SAA ulikabiliwa na matatizo ya kiuendeshaji na kulazimika kusitishwa mwezi Agosti 2006 na ATCL kurejeshwa tena Serikalini kwa asilimia 100.
KUTOKA MAKTABA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akiwa na maafisa na viongozi wengine mbalimbali akikata utepe kuzindua rasmi ndege mbili mpya aina ya Bombadier Q400 zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es salaam Jumatano Septemba 28, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli na mkewe Mama Janeth Magufuli pamoja na maafisa wengine waandamizi wakiwa kwenye ndege mojawapo baada kuzindua rasmi ndege mbili mpya aina ya Bombadier Q400 zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es salaam Jumatano Septemba 28, 2016. PICHA NA IKULU.

MAGAZETI YA LEO, MACHI 31, 2017

MAGAZETI MENGINE/> BOFYA HAPA

RAIS DK. MAGUFULI APONGEZWA KUIWEZESHA TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE

Mar 30, 2017

Frank Mvungi-Maelezo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amepongezwa kwa kuiwezeshaTaasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kufanya upasuaji wa kihistoria tangu kuanzishwa kwake.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo na Daktari Bingwa wa Moyo Dkt. Bashir Nyangassa wakati wa hafla fupi ya kuwaaga madaktari bingwa wa moyo kutoka Hospitali ya Saifee ya Mumbai nchini India waliosaidia kufanikisha upasuaji huo wa kuvuna  mishipa ya damu mguuni na kupandikiza katika mishipa  ya moyo iliyoziba (CABG-Coronary Artery Bypass Graft) kwenye moyo .

Upasuaji huu uliwahusisha madaktari 6 toka Hospitali ya Saifee umesaidia kuwaongezea ujuzi wataalamu wa Taasisi hiyo na kuokoa fedha nyingi ambazo zingetumika kuwasafirisha nje wagonjwa ili waweze kupata matibabu.
“Kama wagonjwa hawa wangeenda kutibiwa nchini India Serikali ingelipia zaidi ya shilingi bilioni 2.1 kama gharama za matibabu” Alisisitiza Dkt. Nyangassa. “

Akizungumzia upasuaji mwingine uliofanyika  kwa wagonjwa 8 Dkt. Nyangassa amesema kuwa ni upasuaji wa milango miwili hadi mitatu ya moyo ambayo ilikuwa na matatizo kwa kuibadilisha.

Kwa upande wa upasuaji wa bila kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa Cath Lab tumetoa huduma mbalimbali za matibabu ya moyo bila kufungua kifua (catheterization) kwa wagonjwa 12 ambao tumezibua mishipa ya damu ambapo mgonjwa mmoja mshipa wake ulikuwa umeziba kwa asilimia 100” Aliongeza Dkt. Nyangasa.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo  kutoka  Hospitali ya Saifee ya nchini India Dkt. Yunus Loya amesema kuwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete umeonyesha mafanikio makubwa na utakuwa wa kudumu.

Aliongeza kuwa Taasisi ya Moyo ya Kikwete ina wataalamu wazuri na siku za usoni watakaobobea zaidi na hivyo Tanzania itanufaika sana na uwepo wa Taasisi hiyo.

Tangu kuanza kwa mwaka huu Taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau wake wa nje ya nchi imefanya upasuaji bila kufungua na kufungua kifua kwa wagonjwa 79.

Mwaka 2016 Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Bohara Duniani Mtakatifu Dkt. Syedna Aliqadr Mufaddal Saifuddin alifanya ziara yake hapa nchini na katika ziara hiyo kiongozi huyo alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Dkt. John Magufuli na kumuahidi kuleta madaktari wa moyo. nchini watakaoshirikiana na Madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na kufanya matibabu kwa wagonjwa.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo kutoka Hospitali ya Saifee, ya Mumbai nchini India Dk. Aliasgar Behranwala (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo wa JKCI Dkt. Bashir Nyangasa na Mkurugenzi wa Upasuaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge (katikati) mara baada ya kumaliza kambi ya siku tatu ya upasuaji wa Moyo katika Taasisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam, ambapo madaktari wa JKCI walishirikiana na Madaktari 6 kutoka nchini India. Madaktaria hao wamekuja nchini kufuatia ahadi ya Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Mabohora Duniani Mtakatifu Syedana Muffadal Saifuddin Saheb kwa Rais Dkt. Magufuli alipomtembelea Ikulu Jijini Dar es Salaam mapema tarehe 13, Oktoba 2016.

UWT WAKASIRIKA CHADEMA NA CUF KUTEUA MIDUME TU UBUNGE AFRIKA MASHARIKI

Dar es Salaam
Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) umekipongeza na kukishukuru Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa  uamuzi wake wa kuteua wagombea wa Ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki kwa uwiano ulio sawa baina ya wanaume na wanawake.

Akizungumza na waandishi wa habari, leo katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa UWT, Amina Makilagi, amesema, kwa uteuuzi huo umedhihirisha kuwa CCM ianatambua na kuthamini mchago wa wanawake katika maendeleo ya Jamii.

" Umoja wa wanawake Tanzania, tunaishukuru Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM iliyokutana jana tarehe 29/3/2017 chini ya Mwenyekiti Dk. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kuteua wagombea wa Ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki kwa uwiano ulio sawa baina ya wanaume na wanawake {50/50}, wanawake 6 na wanaume 6. UWT inatoa shukrani na pongezi kwa uteuzi huo unaodhihirisha kuwa CCM inatambua na kuthamini mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii yetu", amesema  Makilagi.

Amesema wakati UWT iikiipongeza CCM,  haikufurahishwa na uteuzi uliofanywa na vyama vya CHADEMA na CUF katika uteuzi wao wa nafasi hizo, akisema haukuzingatia usawa wa kijinsia kwa kuteua wagombea wote wanaume.

"UWT unavitaka Vyama hivyo kujifunza na kuiga mfano wa CCM katika teuzi zake kwa kuzingatia uwiano sawa na kutambua nafasi ya wanawake, kwani UWT inaamini wapo wanawake wengi wenye uwezo, maarifa na sifa za kugombea katika vyama hivyo ambao wangeliweza kupewa nafasi", amesema.

Katika hatua nyingine, UWT imeihsukuru na kuipongeza CCM kwa uteuzi wa watendaji wake kwa nafasi ya Katibu wa Mkoa na Wilaya ambapo asilimia 30 ya Makatibu walioteuliwa ni wanawake na hivyo kuiomba CCM na Serikali yake kuendelea kuwateua wanawake katika nafasi mbalimbali za Uongozi na Uwakilishi kwenye vyombo vya Maamuzi.

Makilagi amesema UWT inawahamasisha wanachama wake na wanaCCM wenye sifa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa ndani wa Chama na Jumuiya zake ambapo kwa UWT uchaguzi ngazi ya Tawi utaanza tarehe 1- 10/04/2017 hatua ya kuchukua na kurejesha fomu. 

"Natoa mwito kwa wanachama wenye sifa kuchukua fomu katika Ofisi zote za Matawi 24,770 ya UWT zilizopo Tanzania Bara na Zanzibar.

Aidha, nawasihi Viongozi, watendaji na wanachama wote wa UWT/CCM kutojihusisha na vitendo vya rushwa na ukiukaji wa Katiba, Kanuni na taratibu za uchaguzi katika kutafuta uongozi, kwani kufanya hivyo kutawaondolea sifa na atakayebainika atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Kanuni za Maadili ya Chama na kwa sheria za Nchi", alisema.

Pia Makilagi amsema, UWT inaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk. John Magufuli kwa utekelezaji nzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015 – 2020 na kupongeza hatua ya Serikali kuzuia makontena yenye mchanga wa madini na kuunda Tume itakayobainisha kiwango cha madini kilichomo. Lengo likiwa kuhakikisha rasilimali zetu zinawanufaisha Watanzania wote.

BENKI ABC YAFUNGUA TAWI TEGETA, DAR ES SALAA

Na Mwandishi Maalum
Benki ya ABC imeendelea kupanua wingo wake kwa kufungua tawi lake jipya eneo la Tegeta jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuhudumia ongezeko la idadi ya wateja katika eneo hilo, hatua ambayo inaifanya sasa Benki hiyo kuwa na jumla ya matawi matano hapa nchini.

Akizungumza  wakati wa ufunguzi wa tawi hilo, Waziri wa Fedha na Mipango Philip Mpango alisema ni uamuzi mzuri kwa kupeleka huduma za kibenki kwenye maeneo ya nje ya jiji la Dar es Salaam kwa kuwa huduma nyingi za kibenki zinapatikana kati kati ya jiji la Dar es Salaam. ‘Nachukua fursa hii kuwapongeza uongozi wa benki ya ABC kwa kuja na mbinu hii ya kufungua tawi lenu hapa Tegeta. Ni vizuri kufahamu ya kwamba maeneo kama haya ndio yenye Watanzania wengi ambao wanahitaji huduma za kibenki na hivyo inakuwa ni rahisi kuwafikia wale ambao bado hawana huduma hizo,’ alisema Mpango.

Akiongea kuhusu huduma zitolewazo na benki hiyo, Waziri Mpango alionyesha kuridhishwa kwake kwamba benki hiyo inatoa huduma kwa zaidi ya wafanyakazi 60,000 wa serikali kwa kuwapa mikopo pamoja fursa ya kuwekeza. ‘Kwa jinsi mnavyohudumia wafanyakazi wa serikali, fanyeni hivyo hivyo kwa sekta binafsi na watawaamini na kutumia huduma zenu’, aliongeza Mpango.

Mpango alitoa wito kwa Watanzania kujiwekea utaratibu wa kujiwekea akiba kwani ndio njia pekee kwa mtu kuweza kutimiza malengo yake. ‘Kuweka akiba kuna faida nyingi zikiwemo kufikia malengo lakini pia inajenga imani kwa benki pale mtu atapohitaji kupata mkopo. Waziri Mpango pia alitoa wito kwa benki ya ABC pamoja na taasisi zingine za fedha kufikiria kupunguza riba ya mikopo kwani ni Watanzania wengi ambao wamekuwa na nia ya kukopa lakini riba kubwa kwenye mikopo hiyo imekuwa ikiwakatisha tamaa. 

Aliwaomba Watanzania pia kujijengea utaratibu wa kulipa mkopo kwa wakati pale wanapokopa kwani kwa kufanya hivyo kunazidi kujiongezea imani na pia inatoa fursa kwa wengine kukopa.

Akiongea kwenye uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya ABC Dana Botha alisema kufungua tawi la Tegeta ni hatua kubwa ya kuleta huduma za kibenki karibu na wananchi. Hii ni hatua kubwa kwetu benki ya ABC kufungua tawi hapa Tegeta kwani kunaendana na malengo yetu ya kuwafikia wananchi kwa karibu na kuwa moja ya benki zenye mafanikio katika nchi ambazo tunafanya biashara, alisema Botha.


Botha aliwaomba wakazi wa Tegeta pamoja na maeneo ya karibu kuchukua fursa ya benki kuwa karibu nao na kupata huduma zote za kibenki. ‘Sisi kama taasisi tumekuwa tukifanya kazi kwa bidii kufanikisha malengo yetu. Hii ndio sababu tunaendelea kukua na kwa mwaka 2017 benki yetu imeshinda 2017 Banker Afrika, Southern Africa Awards as the Best Emerging Bank – Southern Africa. Ushindi wetu utatokana na kura ambazo zitapingwa na wateja pamoja na wale wote wote waliojisajili. Hii imekuwa moja ya malengo yetu kuendelea kushinda tuzo nyingi zaidi kwa ubora wa huduma zetu, alisema Botha.

Benki ya ABC pia ina malengo ya kujitanua zaidi kwa kufungua matawi mengine mawili kwenye mikoa ya Dodoma na Mwanza kwa mwaka huu.
 Waziri wa Fedha na Mipango Philip Mpango akimpongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya ABC Tanzania Jonas Kapolo, baada ya kuzindua tawi la benki hiyo Tegeta, Dar es Salaam, jana.  Wapili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Dana Botha.
Uzinduzi ukiendelea
Uzinduzi ukiendelea
Waziri wa Fedha na Mipango Philip Mpango akipokea maelezo ya jinsi ya kufungua akaunti kutoka kwa Meneja Huduma kwa wateja wa benki ya ABC ya kufungua tawi jipya la Tegeta la benki hiyo jijini Dar es Salaam.

MWENYEKITI WA CCM TAWI LA MPARANGE RUFIJI APIGWA RISASI NA KUFARIKI DUNIA

Mbunge wa Rufuji Mohamed Mchengerwa.


Na Mwamvua Mwinyi, Ikwiriri
MWENYEKITI wa chama cha mapinduzi (CCM) tawi la  Mparange na mjumbe wa serikali ya kijiji cha Ikwiriri Kaskazini ,wilayani Rufiji mkoani Pwani, Michael Lukanda,ameuawa kwa kupigwa risasi ya kichwani na watu wasiojulikana.
Watu hao  wanadaiwa kuwa ni wawili waliotumia usafiri wa pikipiki ambapo mmoja walimpiga risasi marehemu mlangoni akiwa anataka kuingia nyumbani kwake kisha walitokomea.
Tukio hilo limefuatia baada ya mwenyekiti wa kitongoji cha Mparange kijijini hapo, Bakari Mpanawe kunusurika kifo baada ya kupigwa risasi ya tumboni na mkononi march 19.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Pwani ,Onesmo Lyanga ,alikiri kutokea kwa tukio hilo usiku wa kuamkia march 29.
Alisema tukio hilo ni la tano kutokea ndani ya mwezi huu ,likihusisha uhalifu wa kutumia silaha za moto .
Kamanda Lyanga ,alieleza kwamba wanaendelea kuwasaka watu waliohusika kufanya matukio hayo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria .
Kwa upande wake ,katibu  wa CCM wilayani Kibiti, Zena Mgaya ,alisema hali ya kiusalama sio shwari katika baadhi ya maeneo wilaya  ya Kibiti na Rufiji kijumla.
Alisema hali hiyo inajenga hofu kwa viongozi kupitia CCM ambao baadhi yao wameamua kukimbia miji  kwa kuhofia kuuawa .
Zena alibainisha kwamba,matukio ya aina hiyo yanawasababishia  kuishi pasipo na amani  na wanaccm kuhofia kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi zijazo za chama na serikali za vijiji na vitongoji.
Alihamasisha wanaccm kugombea nafasi mbalimbali bila kuweka uoga  kwani kifo kinapangwa na mungu .
Nae diwani wa kata ya Dimani ,Ramadhani Manyema ,alisema kuna wenyeviti wa vitongoji na vijiji vinne wamekimbia miji  yao wakihofia maisha yao .
Alisema kukimbia maeneo yao ya kazi kumetokana na kutokea matukio ya hivi karibuni ambapo  kuna Mwenyekiti wa kijiji cha  Nyambonda pamoja na wenyeviti wa vitongoji viwili na mtendaji wa kijiji hicho kupigwa risasi .
Maeneo mengine ni Jaribu Mpaka ambako OC CID na mgambo wa maliasili walipigwa risasi na kufariki  na huko eneo la Kifugo tendaji alijeruhiwa kwa kupigwa risasi .
Manyema alieleza ,hali ya kiusalama sio shwari hivyo wanatilia mashaka kama watafanikiwa katika zoezi la uchaguzi wa chama .
Aliliomba jeshi la polisi mkoani Pwani ,lishuke vijijini  ambapo hali sio nzuri pasipo kukaa mjini pekee .
Akizungumza katika ziara yake wilayani Kibiti,katibu  wa CCM mkoani Pwani, Hassan Mtenga aliwataka wazazi na walezi kuwafuatilia nyendo watoto wao kwani wapo vijana wanaotumika kwenye matukio ya kiuhalifu .
Mtenga alisema ifikie hatua ya watu kubadilika kwa kuacha kuficha  wahalifu kisa  ni ndugu ,jamaa ama marafiki .
BODI YA WADHAMINI YA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE (JKCI) YAFANYA KIKAO CHAKE CHA KWANZA JANA JIJINI DAR ES SALAAM

Katibu wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi akisoma taarifa ya Taasisi katika kikao cha kwanza cha Bodi hiyo kilichofanyika jana Machi 29, 2017,  Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ambaye pia ni Daktari Bingwa wa upasuaji wa Magonjwa ya Moyo na mishipa ya damu Prof. William Mahalu. 
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye pia ni Daktari Bingwa wa upasuaji wa Magonjwa ya Moyo na mishipa ya damu Prof. William Mahalu akiongoza kikao cha kwanza cha bodi hiyo kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam. 
Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia taarifa ya Taasisi hiyo iliyokuwa ikisomwa na Katibu ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi katika kikao cha kwanza cha Bodi kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam. 

Picha na Anna Nkinda – JKCI

MAGAZETI YA NDANI NA NJE YA TANZANIA LEO MACHI 30,2017


Magazeti zaidi>Bofya Hapa

TUNA VITU VINNE MUHIMU TUMESHINDWA KUVITUMIA

Julian Msacky

WAKATI wa uhai wake, Mwalimu Julius Nyerere alitupa somo muhimu kuwa ili tuendelee tunahitaji vitu vinne. 

Uongozi bora, siasa safi, ardhi na watu. Huu ni mtaji muhimu kwa nchi yoyote inayotaka kupiga hatua kimaendeleo.

Kwa nchi yangu Tanzania Mungu ameijalia ardhi na watu. Vitu hivi viwili vipo vya kutosha, lakini vinatumika inavyotakiwa?
     Hayati Mwalimu Julius Nyerere

Ni kwa namna gani vinatumika vizuri kuharakisha maendeleo ya nchi na kukuza uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.

Tuelewe vipi kwa mfano tunapoambiwa uchumi wetu umekuwa lakini neema hiyo haionekani kwa wananchi?.

Ni baba gani anakuwa tajiri (uchumi mzuri), lakini familia yake inaishi maisha ya kubangaiza asubuhi hadi jioni? 

Tunadhani uchumi unapokua unatakiwi uonekane kwa wananchi wa kawaida lakini kama si hivyo lazima yawepo maswali.

Mwananchi asiyeweza kumudu milo mitatu kwa siku utamwambia uchumi wa nchi umekua wakati lishe inamshinda.

Kwenye ardhi yetu tunaitumia ipasavyo? Tunaitumia vizuri kwa ajili ya kilimo bora kama tunavyoimba au imejikalia tu?

Kama tungetumia ardhi yetu vizuri leo hii habari za ukosefu wa chakula ingetoka wapi? Habari ya njaa ingetoka wapi?

Binafsi naamini ardhi yetu haijatumika vizuri ndiyo maana wafugaji na wakulima wanavimbiana kila kukicha.

Kwa ardhi tuliyonayo tunashindwa nini kuipangilia vizuri ili wafugaji wafuge kwa amani na utulivu ndani ya nchi yao?

Ukubwa wa ardhi uliopo ni aibu kuona wakulima na wafugaji wanashikana mashati kwa sababu hii na ile. 

Hili ni eneo ambalo hajaweza kulitumia vizuri kiasi kwamba watu wanajazana mijini kwa sababu ya ubunifu mdogo.

Kwa miaka mingi sasa tumeshindwa kuifanya ardhi yetu kuwakomboa wananchi kiuchumi kwa sababu haijapimwa.

Tatizo ni kwamba uongozi bora haupo. Tunapokosa uongozi bora maana yake mambo yetu yanafanyika ovyo ovyo.

Yanakuwa hivyo kwasababu viongozi hawajitambui. Hawajui majukumu yao kwa wananchi ni yapi. Kwa hili kuna ombwe.

Matokeo yake idara nyingine zinajiendesha kwa kulegalega na kimazoea na hivyo kujishindwa kusonga mbele.

Kwa mfano, ngazi ya halmashauri zetu hiki kinachoitwa uongozi bora upo kwa jina au tumekuwa maharibi wa kuzunguka ofisini? 

Ni ofisa gani wa halmashauri leo hii anajua mkulima analima kitu gani? Ni ofisa gani anajua mfugaji anafuga nini na kwa vipi?

Tembelea wananchi uone wanavyopata hasara kwa kukosa wa kumwelekeza alime nini kwenye eneo lake.

Ardhi iliyotakiwa kulima muhogo analima chai. Ardhi iliyotakiwa kulima viazi analima katani. Ni tatizo kweli kweli.

Nenda kwa wafugaji. Wanapoteza mifugo kwa magonjwa yanayoepukika kwa vile tu amekosa kuelekezwa tiba ni nini.

Ndiko tulikofikia kama nchi wakati tunatamani kuwa nchi ya viwanda. Kwa hali hii itawezekana kweli?

Mahali ambapo wakulima wanalima wasichoweza kuvuna na kufuga wasichoweza kupata. Hii ni shida.

Tunahitaji uongozi bora ili kutuondoa hapa tulipo. Uongozi bora haupimwi kwa matamko au lugha kali majukwaani.

Uongozi bora hupima kwa namna watendaji wanavyotimiza majukumu yao kama sheria na taratibu za kazi zilivyo.

Ikumbukwe mahali pasipo na uongozi bora (good leadership) hata ashuke malaika ni vigumu kupata maendeleo. 

Kuna umuhimu suala hili likasisitizwa kuanzia shuleni ili taifa liondokane na ukame wa viongozi bora.

Tukiwa na viongozi bora kilimo kitakwenda vizuri, wafugaji watafuga vizuri, elimu itakuwa bora na mambo mengine mengi.

Ili yote hayo yawezekane ni lazima tuwe na siasa safi. Kwa maana ya kukubali mawazo tofauti ili kusonga mbele.

Kupitia siasa tutashauriwa namna gani tuunganishe nguvu kukabiliana na changamoto zilizopo.

Ni muhimu kwa sababu haijawahi kutokea mawazo ya wateule wachache yakaleta rutuba katikati ya kundi la watu.

Ndiyo maana hata Yesu aliwashirikisha wanafunzi wake ili kutengeneza fikra pana kwa lengo la kuinjilisha vizuri.

WADAIWA SUGU NA TANESCO WAONJA JOTO YA JIWE MKOAN KIGOMA

Mar 29, 2017

Na Rhoda Ezekiel Kigoma.

SHIRIKA la umeme Tanzania TANESCO Mkoani Kigoma imesitisha huduma za umeme kwa Mamlaka ya Maji safi na Mazingira KUWASA, kufuatia deni la umeme la shilingi bilioni 1.3 ambalo halijalipwa tangu mwaka 2013 hadi sasa hali inayopelekea kukosekana kwa Maji Manispaa ya Kigoma na kupelekea dumu moja la maji kuuzwa shilingi 1000.

Akizungumza na Globu ya Jamii, Kaimu Mkurugenzi wa KUWASA, Muhandisi Mbike Jones alisema Mamlaka ya Maji ilikatiwa umeme wiki iliyopita kufuatia deni lililokuwa linadaiwa tangu mwaka 2013 na limeshindwa kulipwa kutokana na Mamlaka hiyo kutegemea fedha hizo kulipwa na Wizara ya maji.

Jones alisema KUWASA ilijitahidi kufanya mazungumzo na TANESCO waweze kurudisha umeme na kudai kuwa ni maelekezo kutoka Makao makuu, mpaka sasa Wizara imejitahidi kufanya mzungumzo na Wizara ya fedha na kudai kuwa watalitatua tatizo hilo baada ya mazungumzo na Shirika la umeme waweze kulipa kidogo kidogo.

Alisema Mpaka sasa KUWASA inadai taasisi za serikali milioni 380 na Wananchi milioni 330, hali inayopelekea kukwamisha zoezi la ulipwaji wa deni hilo kushindwa kulipwa, na aliwaomba Wananchi na Taasisi zinazo daiwa kulipia madeni hayo ili maji yaweze kurudishwa na kuepukana na kero hiyo.

" niwaombe wananchi wawe wavumilivu na waendelee kuchemsha maji wanayo yachota kwenye vyanzo vya maji, ili kuepukana na magonjwa ya milipuko na wawe wavumilivu jitihada zinaemdelea za kuhakikisha tatizo hilo linakwisha na kuendelea kupata maji kama mwanzoni", alisema Jones.

Nao Baadhi ya Wakazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji , Athumani Rashidi na Destina Paulo walisema kumekuwa na tatizo la maji hali inayopelekea Dumu moja la maji kuuzwa shilingi 1000 hali niyopelekea Wananchi wenye kipato kidogo kushindwa kumudu gharama hizo na kushindwa kununua.

Paulo alisema kwasasa wanalazimika kwenda kuchota maji kwenye mito na Visima vilivyoko mbali na mji kilomita nane kutokea Mjini hali hiyo inawapelekea kushindwa kukabiliana na kero hiyo, na waliiomba serikali na mamlaka inayo husika kuliahughurikia suala hilo ilikuepukana na kero hiyo.


Baadhi ya wakazi kutoka maeneo mbalimbali wakichota maji kwenye vyanzo vya maji vinavyopatikana mjini humo.

WANANCHI BINAFSI WANAWEZA KUKOPA (MOGEJI) MORTGAGE MOJA KWA MOJA KWENYE MABENKI: MTAALAMU BoT


NA K-VIS MEDIA/Khalfan Said
WANANCHI binafsi wanaweza kwenda kwenye mabenki na kuomba mikopo ya fedha za ujenzi, (Mortgage Finance), bila ya kuanza kupitia kwenye taasisi nyingine za fedha.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi-Usimamizi wa Mabenki  Benki Kuu ya Tanzania, (BoT),  Bw. Eliamringi Mandari, (pichani juu), wakati akiwasilisha mada juu ya utaratibu wa mikopo ya fedha kwa ajili ya ujenzi, (Mortgage Finance) na utunzaji taarifa mteja (mkopaji) katika kitunza taarifa cha kibenki, (Databank) kwenye semina ya Waandishi wa Habari za Uchumi na Fedha leo Machi 29, 2017 inayoendelea kwenye ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (tawi la Zanzibar), mjini Unguja.
“Watu wengi hawajui kama kuna fursa hii ya ku-mortgage, kwa maana ya kujenga, kununua au kurekebisha nyumba yako, na katika kudhamiria kufanya hayo, benki inaweza kutoa masharti ambayo ni ya kurejesha fedha (mkopo) huo kwa muda mrefu kati ya miaka 5 hadi 20.” Alisema.
Hata hivyo alisema kama ilivyo kwa masharti mengine yahusuyo kukopa, hata fursa hii ya kukopa fedha kwa ajili ya ujenzi vigezo na masharti pia huzingatiwa ili benki iweze kutoa mkopo huo.
Aidha kuhusu mfumo wa taarifa unaosaidia mkopeshaji,(lender), kumjua mkopaji, (borrower), ujulikanao kama, Credit Reference System, (DBS), alisema Sheria namba 48 ya BoT kuhusu masuala ya kubadilishana taarifa za mikopo, kwa mabenki na taasisi nyingine za fedha inalazimisha mabenki na taasisi hizo kutuma taarifa za wateja (wakopaji), kwenye Databank ya BoT kila mwezi, alisema Bw. Mandari
Alisema pia BoT, inaandaa utaratibu utakaolazimisha wakopeshaji binafsi na Taasisi za Kibinafsi, (NGOs), zinazojihusisha na utoaji mikopo, kusimamiwa, (Regulated), katika utoaji wa taarifa za mteja (mkopaji), katika kitunza taarifa cha kibenki, (Databank), ili kuwaondolea usumbufu wananchi.
 “Ni kweli Sheria  inaitaka Benki Kuu kusimamia taasisi za fedha zinazochukua amana kutoka kwa wananchi, kwa kuwasilisha taarifa hizo za wakopaji kwenye mfumo huo wa BoT wa Databank, lakini kwa sasa wakopaji binafsi na taasisi za hiari zinazojishughulisha na utoaji mikopo ya kifedha, bado sera inaandaliwa ili na wao waweze kusimamiwa.” Alisema.
Alisema, wakopaji binafsi na NGOs zinazojihusisha na utoaji mikopo, zimekuwa zikitumia mabavu wakati mwingine katika kufuatilia marejesho ya mikopo kutokana na utaratibu usio wazi wa kukopa, na wakati mwingine wakopaji wanarejesha mikopo kwa riba kubwa, alifafanua.
 Bw. Eliamringi Mandari, akiwasilisha mada hiyo
Meneja Msaidizi Msoko ya Ndani wa BoT, Bw.Genes Kimaro,  akiwasilisha mada juu ya Majukumu ya Kurugenzi ya Masoko ya Fedha, Utekelezaji wa Sera ya Fedha wa BoT.
 Bw.Genes Kimaro
 Mchambuzi wa Masuala ya Fedha wa BoT, Bw.Mohammed Kailwa, (kushoto), akijibu baadhi ya hoja wakati akisaidiana na Meneja wa Masoko ya Ndani, Kurugenzi ya Masoko ya Fedha (BoT), Bw.Reverian Felix
 Baadhi ya waandishi wa nhabari za Uchumi na Fedha wanaohudhuiria semina hiyo
Meneja wa Fedha na Utawala, Bodi ya Bima ya Amana ya BoT, Bw. Richard Malisa, akitoa mada jinsi Bodi ya Bima ya Amana inavyokinga amana za wananchi

 Mwandihi wa Clouds TV, Bw. Austin Beyadi, (kulia), akihariri habari wakati semina ikiendelea. Kushoto ni Grace Semfuko wa Star Tv.
 Mmiliki wa Mtandao wa TZ Business News Online, Jaston Binala, akizungumza kwenye semina hiyo
Afisa Uhusiano Mkuu, Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki wa BoT Bw. Lwaga Mwambande, (kulia), akifafanua jambo wakati wa semina hiyo
 Meneja Msaidizi-Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki wa BoT, Bi. Vicky Msina, (kushoto), akizungumza jambo na Mwandishi wa habari wa Shirika la Habari Zanzibar, (ZBC), wakati wa mapumziko ya mchana ya semina hiyo.
Mwenyekiti wa Semina, ambaye pia ni mwandishi wa habari wa gazeti la Raia Mwema, Bw. Ezekiel Kamwaga, akizungumza kwenye semina hiyo
 Bi. Vicky Msina, (kulia), na Bw. Lwaga Mwmbande kutoka Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki, BoT, wakifuatilia mijadala na mada zilziokuwa zikitolewa
 Bi. Vicky (kulIa), akiwa na Bi. Flora Mkemwa kutoka Idara ya Uhusiano na Itifaki BoT
 Mchumi Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Utafiti na Sera za Uchumi wa BoT, Bw. Lusajo Mwankemwa, akifuatilia mjadala

PROFESA MUHONGO : WANANCHI LIPENI UMEME OFISI ZA TANESCO PEKEE

Na Veronica Simba – Singida
 
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewataka wananchi wote, hususan wanaounganishiwa huduma ya umeme vijijini, kufanya malipo husika katika Ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) peke yake na siyo kwa mtu mwingine yeyote.
Aliyasema hayo hivi karibuni kijijini Mkwese, Wilaya ya Manyoni wakati akizindua Mradi Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) katika Mkoa wa Singida.
Profesa Muhongo alisema kuwa wananchi wengi wamekuwa wakitapeliwa na watu mbalimbali kwa kuombwa rushwa ili waunganishiwe umeme au kulipishwa gharama zaidi ya zile zinazostahili, na baada ya kufuatilia, imebainika kuwa wanaofanya utapeli ni watu wasiohusika kabisa na uunganishaji umeme.

Ili kuepuka utapeli huo, Waziri Muhongo amewataka wananchi kufahamu taratibu zinazopaswa kufuatwa wakati wa kuunganishiwa umeme ikiwa ni pamoja na kujua kiasi wanachopaswa kulipia na ni nani wa kumlipa.
Aidha, aliitaka Tanesco kuhakikisha inaendelea na zoezi la kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma zote wanazotoa ili wananchi wawe na uelewa wa kutosha na hivyo kuepuka kutapeliwa.
Alisema kuwa, baadhi ya wananchi wanadhani kuwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ndiyo wenye jukumu la kuchukua malipo kutoka kwa wananchi wanaounganishiwa umeme vijijini.
“Anayepokea malipo yote ya umeme ni Tanesco. Siyo REA wala Wizara. Wananchi mjue hilo. Mwingine yeyote akidai malipo ya umeme, kataeni,” alisisitiza.
Waziri Muhongo aliwataka Wakuu wa Wilaya mbalimbali kuhakikisha wanamkamata na kumweka ndani mtu yeyote anayepita katika maeneo yao na kudai malipo ya umeme kutoka kwa wananchi wakati siyo Ofisa wa Tanesco.
“Mambo ya malipo yote yanafanywa Tanesco. Wala huyu Mkandarasi hakusanyi fedha. Kama ataomba fedha za kuunganishia watu umeme au za nguzo, huo ni wizi na utapeli. Lazima mumshtaki.”
Akielezea kuhusu utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Profesa Muhongo alisema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha inaundoa umaskini wa wananchi kwa kuwapatia huduma muhimu ikiwemo umeme.
“Injini mojawapo nzuri na muhimu ya kuondoa umaskini wetu ni kuhakikisha tunakuwa na umeme wa uhakika, unaotabirika na wa bei nafuu.”
Alisema, Serikali inatambua kuwa wananchi walio wengi wanaishi vijijini ndiyo maana Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ambayo inaishia mwezi wa sita mwaka huu, fedha zake nyingi zilipelekwa kwenye miradi hususan ya umeme vijijini.
Profesa Muhongo alisema kuwa, ili kuwapunguzia wananchi gharama ya kufuata huduma ya kuunganishiwa umeme kwenye Ofisi za Tanesco ambazo ziko mbali, Serikali imeagiza maafisa wa shirika hilo kutangaza tarehe watakapofika kugawa fomu za kujiandikisha pamoja na vituo vitakavyotumika kufanyia malipo.
Alitoa rai kwa Serikali za Vijiji kutoa ushirikiano kwa Tanesco, ikiwezekana kuwapatia chumba au Ofisi ya kutolea huduma kwa siku watakazopanga kutoa huduma katika vijiji husika.
Waziri Muhongo alieleza kuwa, kwa Mkoa wa Singida, Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu utatekelezwa kwa vipindi viwili tofauti ambapo sehemu ya kwanza itahusisha upelekaji umeme katika vijiji 185 kwa gharama ya shilingi bilioni 47.36. Aliongeza kuwa utekelezaji wa sehemu hiyo ya kwanza umeanza mwezi Februari mwka huu na unatarajiwa kukamilika ifikapo Machi 2019.
Alimtaja Mkandarasi Nakuroi Investment Co. Ltd ambaye alimtambulisha pia kwa wananchi na kumkabidhi kwa viongozi wa Serikali na Wabunge wa Singida, kuwa ni mmoja wa makandarasi watakaoshiriki katika utekelezaji wa Mradi husika katika Mkoa huo.
Aidha, Profesa Muhongo alieleza kuwa, sehemu ya pili ya mradi huo mkoani Singida, itaanza kutekelezwa baada ya sehemu ya kwanza kukamilika mwaka 2019 ambapo vijiji 82 vitapatiwa umeme na hivyo kufikisha umeme katika vijiji vyote vya Mkoa wa Singida ifikapo Mwaka 2021.
Uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu kwa Mkoa wa Singida ulihudhuriwa na wananchi, viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na baadhi ya wafadhili wa Mradi husika ambao ni Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Katarina Rangnitly na Balozi wa Norway nchini, Hamme Hanie Kaarstad.
ยช