Breaking News

Your Ad Spot

Mar 7, 2017

MeTL GROUP YAJIDHATITI KUTOA AJIRA KWA USAWA BAINA YA WANAWAKE NA WANAUME

Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group) imesema itaendeleza sera yake ya kutoa ajira bila kufanya ubaguzi wa kijinsia baina ya wanawake na wanaume. Hayo yamesemwa na mwakilishi wa MeTL Group, Catherine Decker wakati wa kongamano la kuadhimisha siku ya wanawake lililoandaliwa na Shirikisho la Wafanyakazi nchini Tanzania (TUCTA). Catherine amesema kampuni ya MeTL imeamua kuweka utaratibu huo wa kuweka usawa kwa wafanyakazi kati ya wanaume na wanawake ili kuwapa nafasi wanawake kushiriki katika shughuli za maendeleo lakini pia kuepusha matukio ya unyanyasaji wa kijinsia kazini.

Mwakilishi wa MeTL Group, Catherine Decker akizungumza katika kongamano la kuadhimisha siku ya wanawake.
“Kama kampuni ya MeTL imeweka sera katika kuwasaidia wanawake, sera hiyo ni kuangalia uwiano kati ya mwanamke na wanaume kila mwaka. Sababu ya kufanya hili ni kuhamasisha usawa ndani ya kampuni yetu,” amesema Catherine na kuongeza. “Kama kampuni tunatambua umuhimu wa usawa katika kuepusha matukio ya unyanyasaji wa kijinsia, sera hii inatusaidia katika kuwafatilia wafanyakazi wetu lakini pia inatutengenezea mazingira mazuri ya kupambana na matatizo kama ya utovu wa nidhamu na vitendo vya unyanyasaji ya kijinsia.” 
Baadhi ya watu waliohudhuria kongamano hilo.
Aidha Catherine amesema MeTL imekuwa ikiandaa mashindano mbalimbali ambayo yamekuwa yakiwahusisha wanawake na wanaume ili kuwakutanisha wafanyakazi wa kampuni kutoka sehemu mbalimbali kwa lengo la kufahamiana na kufurahi kwa pamoja. “Itambulike kuwa MeTL sio tu mwajiri wa wafanyakazi hawa au kampuni bali ni familia moja ambayo inalenga kuboresha maisha ya watu kwa viwango mbalimbali na huwa tunaanda matukio ya michezo ambapo wanaume na wanawake hukutana na kushiriki vyema,” amesema Catherine. 
Mbunge wa Urambo, Magreth Sitta kongamano la kuadhimisha siku ya wanawake.
Kwa upande wa mgeni rasmi katika kongamano hilo, Mbunge wa Urambo, Magreth Sitta amewataka kutumia vyema nafasi za kazi wanazopata katika mashirika mbalimbali na kuwashauri kuwa ni vyema wakaweka utaratibu wa kuwashirikisha wanaume katika mipango yao. “Wanawake ni vyema mkashirikiana na wanaume, kama kuna jambo mnawambia ili kulifanya kwa pamoja, hata mimi siri ya kufika hapa nilipo ni sababu ya kuwashirikisha, mkifanya hivyo mtakuwa mmefanya jambo jema sana,” alisema Magreth.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages