.

RAIS DK. MAGUFULI AAGIZA MKANDARASI WA MRADI WA MAJI LINDI ANYANG'ANYWE PASSPORT

Mar 3, 2017

LINDI, TANZANIA
Rais Dk. John Magufuli, amecharuka na kuagiza kushikiliwa kwa hati za kusafiria za mwakilishi wa kampuni ya ukandarasi ya Overseas Infranstructure Alliance Private Limited ya India, Rajendra Kumar pamoja na wasaidizi wake mpaka hapo kampuni hiyo itakapokamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa Ng'apa Mjini Lindi ambao ulipaswa kuwa umekamilika tangu tarehe 17 Machi, 2015.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 03 Machi, 2017 alipotembelea mradi huo ambao unatarajiwa kuzalisha zaidi ya lita za ujazo milioni 5 za maji kwa siku kwa ajili ya wakazi wa Mji wa Lindi ambao wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji.

Dk. Magufuli ameelezea kusikitishwa na usimamizi mbaya wa mradi huo ambao tayari kiasi cha Sh. Bilioni 21.8 zimetolewa kati ya Sh. Bilioni 29 zilizopangwa kutumika hadi kukamilika kwake, na ameonya kuwa endapo mradi huo hautakamilika katika kipindi cha miezi minne kuanzia sasa atachukua hatua dhidi ya wanaopaswa kuusimamia.

"Ikipita miezi minne nisilaumiwe, hatuwezi kukubali wananchi wa Lindi wanashida ya maji, fedha zimetolewa, mkandarasi anaamua kupeleka fedha India, mradi umecheleweshwa kwa miaka miwili na mkandarasi hayupo kwenye eneo la ujenzi halafu mnaopaswa kumsimamia mnamuangalia tu wakati sheria zipo, kwa nini hamkumfukuza muda wote huu?" amehoji Rais Magufuli.

Mapema akitoa maelezo kuhusu mradi huo Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema mradi huo unatekelezwa kwa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) na Jumuiya ya Ulaya (EU) ambapo hadi sasa umefikia asilimia 85 na kwamba mkandarasi amesimamisha kazi kutokana na kuishiwa fedha.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช