Breaking News

Your Ad Spot

Jul 8, 2017

MANISPAA YA ILALA YAPIGWA FAINI YA SH. MILIONI 25 KWA KUTOHUDUMIA IPASAVYO DAMPO LA PUGU KINYAMWEZI

NA EVELYN MKOKOI
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia Mkaguzi wa Mazingira wa Kanda ya Mashariki Jaffari Chimgege, limeipiga faini ya Sh. milioni 25 Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, kutokana na kosa la uchafuzi wa mazingira.

Ilala imetozwa faini hiyo baada ya kupatikana na kosa la kutohudumia ipasavyo dambo la Pugu Kinyamwezi  na hivyo kutoa harufu mbaya, vumbi na maji yenye sumu kali  na kuhatarisha kwa afya ya wakazi wa maeneo jirani, viumbe hai na mzingira kwa ujumla.

Hatua hiyo ilifikiwa jana kufuatia ziara ya Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Luhaga Mpina, aliyofanya katika Manispaa ya Ilala kwa kufanya ukaguzi wa dampo hilo la Pugu Kinyamwezi kutokana na malalamiko ya wakazi wa mtaa wa Viwege uliopo katika Kata ya Majohe yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Mtaa huo, Amina Rashid.

Katika malalamiko hayo Amina alieleza kuwa dampo hilo linakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za vumbi na maji yenye kemikali kwenda katika maeneo ya makazi.

Kufuatia malalamiko hayo Naibu Waziri Mpina, ameitaka Halmashauri ya Jiji kutayarisha mpango mkakati utakaoweza kila Manispaa kuwa na dampo lake ili kulipunguzia mzigo dampo hilo la Pugu Kinyerezi, ambalo kwa sasa linatumika kupokea takataka zote za Halmashauri za jiji la Dar es Salaam na hivyo kulemewa.

"Hakuna kitu nisichopenda katika utendaji wangu kama kuona taasisi za serikali zikiwa za kwanza katika suala zima la uchafuzi wa mazingira, faini hiyo jiji mtailipa ndani ya siku 14, na kuhakikisha mnarekebisha  matobo yote yanayolalamikiwa kupitisha maji na kupeleka katika makazi ya wananchi pamoja na kujenga mifereji ya maji ya mvua, na maji ya sumu yaende katika mkondo sahihi wa maji hatarishi na bila kusahau kuruhsu maji hayo baada ya kujiridhisha na vipimo vinavyotakiwa", alisema Mpina.

Aidha Mpina alibaini kuwepo kwa udhaifu mkubwa katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na kuondosha taka katika Manispaa za jiji na kuutaka uongozi wa jiji hususan Mkurugenzi wa Jiji kufuatilia madeni hayo kikamilifu, na kutoa muda wa uwasilishwaji wa fedha hizo, huku akisisitiza kuwa  ni vyema ghahama za uondoshwaji wa taka zikatokana na taka zenyewe na siyo kutoa fedha za kuhudumia taka kutoka katika vyanzo vingine vya mapato. 

Mpina aliitaka Manispaa ya jiji  kutafuta namna bora ya kuondosha taka sumu na kuanuru taka zote za matairi katika jiji la Dar es Salaam zitafutiwe sehemu tofauti na namna pekee ya kuzitekekeza.

Awali akitoa taarifa ya hali ya mazingira  na usimamizi wa taka katika dampo  la Pugu Kinyamwezi, Mkuu wa Idara ya usimamizi taka wa jiji la hilo, Shedrack Maximillian alimweleza Waziri Mpina kuwa jiji linakabiliana na changamoto mbali mbali ikiwa ni pamoja dampo kupata moto, kutokuwa la kisasa na maji yenye sumu kwenda katika makazi ya wananchi.

Alisema Manispaa ya Ilala imetenga kiasi cha Sh. Bilioni moja kwa mwaka wa fedha ulioisha na kuzungumza na wadau wa maendeleo ikiwa ni mkakati madhubuti wa kuweza kuboresha dampo hilo kinalotumika kwa kiasi kikubwa na Manispaa zote za jiji la Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Raisi Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina (kulia) akiwa ameambatana na Meya wa Jiji la Dar es salaam, Isaya Mwita (kushoto) wakati wa ziara ya kukagua uchafuzi wa mazingira katika dampo la Pugu Kinyamwezi, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages