Breaking News

Your Ad Spot

Jul 9, 2017

MAONYESHO YA SABASABA YATOA FURSA MASOKO YA NJE

Na Lilian Lundo - MAELEZO
Maonesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yametoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo kupata masoko ya bidhaa zao nje ya nchi.

Hayo yamesemwa leo, Jijini Dar es Salaam  na mfanyabiashara wa korosho kutoka Mtwara Bi. Sakina Ponella katika uwanja wa Mwalimu Nyerere, yanapofanyika maonesho hayo.

"Kutokana na ubora wa korosho ninazouza, nimefanikiwa kupata wateja kutoka nchi za Uturuki, China, Syria na Rwanda," amesema Sakina.

Amesema kuwa mmoja wa wateja hao  waliotembelea banda lake, amehitaji kutumiwa tani 4000 za korosho kila mwezi. Lakini kutokana na zao lenyewe kuwa la msimu, hivyo amemuelisha mteja huyo awe anatumiwa tani nyingi zaidi kipindi cha msimu wa zao hilo badala ya kutumiwa kila mwezi.

Sakina ameongeza kuwa, tayari wamebadilishana namba za simu na wateja hao kwa ajili ya hatua ya kuandikishiana mikataba na kuanza kutuma korosho hizo.

Kwa upande wake, Afisa Masoko wa kampuni ya Moringa (Mlonge)  Natural Product kutoka Arusha, Leah Moses amesema maonesho hayo yamewasaidia kujulikana zaidi nje na ndani yaTanzania.

Amesema kuwa wamefanikiwa kupata wateja kutoka nchi za Kongo, Nairobi na China, ambao pia wamechukua namba za mawasiliano ya kampuni hiyo kwa ajili ya kuagiza bidhaa nyingine zaidi.

Aidha, mfanyabiashara wa vinyago kutoka Mtwara, Bi. Salma Omary amewata wafanyabiashara wadogo wadogo kutumia fursa ya maonesho mbalimbali ya biashara kujitangaza ili kupata masoko ndani na nje ya nchi.

"Wafanyabiashara hawatakiwi kufikiria juu ya kupata faida peke yake katika maonesho kama haya. Lakini wanaweza kutumia fursa ya maonesho ya biashara kwa ajili ya kujitanga zaidi ambapo itawaletea wafanyabiashara wengi zaidi wa kudumu,' amesema Bi. Salma.

Maonesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, yalifunguliwa rasmi Julai 1 mwaka huu na Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Maonesho hayo yalitarajiwa kufungwa Julai 8 mwaka huu. Aidha Rais Magufuli alitoa agizo la kuongezwa siku 5 zaidi ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara kujitangaza, vile vile kwa Watanzania kujifunza juu ya uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo, vya kati na vikubwa.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages