Breaking News

Your Ad Spot

Jul 27, 2017

NDUGAI ACHAGULIWA KUWA BOSI WA MASPIKA AFRIKA

Spika Job Ndugai
Spika wa Bunge Job Yustino Ndugai (Mb), amechaguliwa kuwa Mwenyekiti  wa Maspika na Viongozi wa Bunge katika Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Barani Afrika. 

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Bunge mjini Dodoma, leo, imesema Spika Ndugai amechaguliwa katika uchaguzi ambao umefanyika  katika Mkutano wa Maspika wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Barani Afrika uliomalizika leo Mjini Abuja.

Kwa wadhifa huo, Ndugai ataongoza Maspika wenzake toka Mabunge na Mabaraza ya kutunga Sheria  63 yaliyoko katika nchi 18 za Jumuiya ya Madola kwenye Bara la Afrika. Wadhifa huo ni wa miaka miwili kuanzia sasa hadi mwaka 2019 kutakapofanyika uchaguzi mwingine.

Nchi wanachama wa Umoja wa Mabunge Barani Afrika ni pamoja na Afrika  ya Kusini, Botwana, Cameroon ,Ghana, Kenya, Lesotho,   Msumbiji, Mauritius, Malawi, Nigeria, Namibia, Rwanda, Seychelles, Sierra Leone, Swaziland, Tanzania, Uganda na Zambia.

"Kwa hakika nawashukuru Maspika wenzangu kwa kunipa dhamana hii ya kuwa Mwenyekiti wao, ni heshima kwangu binafsi lakini zaidi Kwa Tanzania. Ni matumaini yangu kwamba Bunge letu litaendelea kung'ara kitaifa na kimataifa tukiwa Bunge moja lenye Upendo na mshikamano". Ndugai amesema baada ya kuchaguliwa kwake.


Huu ni wadhifa wa nne kwa Ndugai katika masuala ya Bunge kwenye medani ya Kimataifa. Amewahi kuwa Mwakilishi wa Nchi za Afrika Mashariki katika Kamati ya Utendaji ya Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Duniani mwaka 2008-2011, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii ya Umoja wa Mabunge ya Afrika, Pacific na Carribbean na Jumuiya ya Ulaya  mwaka 2011-2014 na Rais wa Baraza la Mabunge ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC – PF)

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages