Breaking News

Your Ad Spot

Aug 10, 2017

MFUMO WA PLANREP KUIMARISHA USALAMA WA NYARAKA ZA SERIKALI

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Morogoro.
Mfumo ulioboreshwa wa kuandaa Mpango wa Bajeti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa (PlanRep) unategemea kuimarisha usalama wa nyaraka za Serikali kwa kuzihifadhi katika mtandao.

Hayo yamesemwa leo Mkoani Morogoro na Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Frank Jacob alipozungumza na mwandishi wa habari hii juu ya umuhimu wa mafunzo yanayoendelea mkoani humo kwa watumiaji wa mfumo huo.

Dkt. Jacob amesema kuwa anaishukuru Serikali pamoja na wafadhili wa mradi huo kwa kuwaza kuurekebisha mfumo huo na kuuboresha ili utumike katika sekta zote.

“Kwa kifupi mfumo ulioboreshwa utakuwa na utunzaji wa nyaraka za Serikali wa hali ya juu kwa sababu mwanzoni kila afisa husika wa kuandaa mipango na bajeti alikuwa akiandaa taarifa hizo na kuzihifadhi katika kompyuta hivyo ikitokea imeharibika au kuibiwa taarifa zote zinapotea lakini kwa sasa tutahifadhi moja kwa moja katika mtandao ambao hauwezi kufuta au kupoteza taarifa yoyote”, alisema Dkt. Jacob.

Dkt. Jacob ameongeza kuwa kuboreshwa kwa mfumo huo kutasaidia kurahisisha kazi kwa sababu kuna taarifa nyingi hasa za takwimu zilikuwa zikiingizwa kwa njia za kawaida zinazotumia muda mrefu lakini kupitia mfumo huo wataweza kuingiza takwimu hizo kiurahisi kufuatia mfumo huo kuunganishwa na mifumo mbalimbali.

Vile vile kulikuwa na changamoto ya kupishana kwa taarifa katika majumuisho kwani kila afisa husika anafanya mahesabu ya taarifa zake kwa kutumia njia za kawaida ambazo kwa bahati mbaya zinaweza zisifanywe kwa usahihi.

Aidha, Dkt. Jacob amefafanua kuwa kupitia mfumo huo Wizara itaboresha utendaji kazi na itawajengea uwezo Mikoa kufanyia kazi changamoto za Halmashauri kwa sababu mfumo huo hautaruhusu taarifa za Halmashauri kwenda Wizara husika moja kwa moja bila kupitia mkoani. 
 
Mfumo huo mpya wa kitaifa umeboreshwa kwa ajili ya kutumika katika sekta zote za umma na umehuishwa na mifumo mingine ya Serikali ili kuboresha usimamizi na kuiwezesha Serikali katika ngazi zote kuweza kufanya kazi kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa jamii.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages