Breaking News

Your Ad Spot

Aug 10, 2017

RAIS DK. MAGUFULI AKUTANA NA BILL GATE NA KAIMU BALOZI WA MAREKANI, TANZANIA KUPATA DOLA MILIONI 575 ZA MAREKANI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akizungumza na Mwenyekiti wa  Tasisi ya Bill and Melinda Gates Foundation Bill Gates aliyemtembelea  Ikulu jijini Dar es Salaam leo Agosti 10, 2017.
---------------------------------------------------
IKULU, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Bill and Mellinda Gates imetenga Dola za Marekani Milioni 350 sawa na takribani Shilingi Bilioni 777.084 za Tanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta ya kilimo, afya na mifumo ya kielektroniki ya upatikanaji wa taarifa.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu jijini Dar es Salaam, leo, imesema, Mwenyekiti Mwenza wa taasisi hiyo Bw. Bill Gates amesema hayo leo tarehe 10 Agosti, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

Bw. Bill Gates amesema kama ambavyo taasisi yake imeshirikiana na Tanzania kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha huduma za afya hapa nchini, fedha hizo zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi zaidi ya afya ikiwemo kupunguza vifo vya uzazi, kukabiliana na ugonjwa wa malaria, kuimarisha lishe na kukabiliana na utapiamlo, zitaelekezwa katika sekta ya kilimo ambako zitasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao, kuzalisha mbegu bora na kuboresha ufugaji utakaoongeza chakula na pia zitasaidia kuweka mifumo ya kisasa ya upatikanaji wa taarifa.

Bw. Bill Gates ameelezea kufurahishwa na maendeleo ya uchumi wa Tanzania pamoja na uongozi na msimamo wa Rais Magufuli juu ya kutaka miradi hiyo ilete matokeo yenye manufaa, na amesema atakuja Tanzania mara nyingi ili kuimarisha zaidi ushirikiano na kufuatilia utekelezaji wa miradi.

Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Bw. Bill Gates kwa mchango mkubwa unaotolewa na taasisi ya Bill and Mellinda Gates katika miradi mbalimbali hapa nchini ikiwemo fedha ambazo taasisi hiyo itazitoa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa na amemhakikishia kuwa Serikali yake itahakikisha fedha hizo zinaleta matokeo yaliyokusudiwa.

Mazungumzo kati ya Mhe. Rais Magufuli na Bw. Bill Gates yamehudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Ufugaji na uvuvi Dkt. Charles Tizeba na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.

Wakati huo huo, Mhe. Magufuli amekutana na kufanya Mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Dkt. Inmi Patterson ambaye amesema Marekani itatoa fedha za nyongeza kiasi cha Dola Milioni 225 sawa na Shilingi Bilioni 499.500 za Tanzania katika mwaka ujao kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo itakayogusa sekta za elimu, afya, lishe bora, utawala bora.

Mhe. Inmi Patterson amesema Marekani imeongeza fedha hizo katika miradi inayotekelezwa hapa nchini kwa sababu ina dhamira ya dhati ya kushirikiana na Tanzania na itahakikisha uhusiano na ushirikiano huu unaendelezwa na kukuzwa zaidi.

Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Balozi Inmi Patterson kwa mchango mkubwa ambao Marekani imekuwa ikiutoa kwa Tanzania na amemhakiki kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano wake na Marekani, na pia amemuomba awahimize wafanyabiashara na wawekezaji wengi zaidi wa Marekani waje kuwekeza na kufanyabiashara hapa nchini kutokana na fursa lukuki zilizopo.

Mhe. Rais Magufuli pia ameiomba Marekani kusaidia kujenga hospitali kubwa ya kitaifa katika makao makuu ya nchi Mkoani Dodoma ili kuongeza uwezo wa Mkoa huo kutoa huduma za matibabu ikilinganishwa na ilivyo hizi sasa.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages