Breaking News

Your Ad Spot

Aug 10, 2017

SERIKALI KUDHIBITI USAFIRISHAJI WA FEDHA TASLIMU MIPAKAN

Washiriki wa warsha ya siku mbili ya maandalizi ya utekelezaji wa Kanuni za Taarifa za Usafirishaji na uingizaji wa fedha tasilimu kutoka na kwenda nje ya nchi wakifuatilia kwa makini mjadala katika warsha hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu (BoT) jijini Dar es Salaam.

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa Kanuni za taarifa za Usafirishaji na uingizaji wa fedha taslimu kutoka na kwenda nje ya nchi (Crossborder Declaration of Currency and Bearer Negotiable Instruments Regulations) ambapo wasafirishaji wa fedha taslimu na wasafiri wote wanaotoka au kuingia nchini, watatakiwa kutoa taarifa za fedha taslimu wanazosafirisha ikiwa fedha hizo zinalingana au zinazidi kiasi cha dola za kimarekani elfu kumi (USD 10,000).

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku mbili ya maandalizi ya utekelezaji wa Kanuni hizo, Kamishna na Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU) Ndugu Onesmo H. Makombe alisema utekelezaji wa kanuni hizi, pamoja na mambo mengine utaiwezesha nchi kuwa na takwimu za usafirishaji fedha taslimu.

“Takwimu hizo zitakazosaidia pamoja na mambo mengine kubaini vitendo vya kihalifu, kupunguza utoroshaji wa mitaji na kuhakikisha kuwa tunapunguza kama siyo kumaliza kabisa usafirishaji wa fedha zitokanazo na uhalifu au/na fedha kwa ajili ya kufadhili ugaidi” alisema Bw. Makombe

Aidha kanuni hizo zimeweka adhabu zitakazochukuliwa dhidi ya wale watakabainika kutaka kupita na fedha zinazolingana au zinazozidi kiwango kilichowekwa bila kutoa  taarifa au watakaotoa taarifa za uongo.

Alizitaja adhabu hizo kuwa ni pamoja na kukamatwa kwa fedha taslimu walizonazo na kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria kama vile kufunguliwa mashtaka.

“Wahalifu pamoja na mambo mengine, wanapenda kusafiri na fedha taslimu kwani wanaogopa kutumia benki kutuma fedha kutokana na umakini unaoongezeka katika benki na udhaifu unaoweza kuwepo mipakani” Alisisitiza Bw. Makombe

Kamishna huyo amewaasa washiriki wa warsha hiyo kutekeleza jukumu hilo  kwa uadilifu na uaminifu mkubwa  ili kuziba mianya yote ambayo wahalifu wanaweza kuitumia kutimiza kusudi lao ovu na kuhatarisha usalama wa nchi.

Kutokana na umuhimu wa ushiriki wa wadau mbalimbali katika utekelezaji wa kanuni hizo warsha hiyo imejumuisha washiriki kutoka taasisi mbalimbali wengi wao wakiwa ni maafisa forodha.

Washiriki hao wametoka Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Fedha na Mipango-Zanzibar, Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kikanda, Mamlaka ya Mapato Tanzania na vikosi vya ulinzi na usalama

Wengine ni Bodi ya Mapato Zanzibar, Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo-Zanzibar, Shirika la Posta,  Benki kuu ya Tanzania, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka-Zanzibar, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka-Tanzania Bara Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania Bara na Zanzibar, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania,  Idara ya uhamiaji na Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages