.

CHOUGHULE ASAIDIA WAGONJWA OCEAN ROAD, AIOMBA SERIKALI KUBORESHA ZAIDI HUDUMA KWENYE TAASISI HIYO

Aug 27, 2017

Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kivukoni, Sharik Choughule akikabidhi mafuta ya kupikia kwa Ofisa Muuguzi Msaidizi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, leo, alipofika kutoa msaada wa vyakula ikiwemo unga, mchele, maharage na mafuta ya kupikia.
--------------------
OCEAN ROAD, DAR ES ASALAAM
Serikali imeombwa kuongeza jitihada za kuangalia huduma katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, ili kuondoa kero zinazowakabili  wagonjwa.

Akizungumza baada ya kutembelea baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika Taasisi hiyo, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kivukoni, Sharik Choughule, alisema, wagonjwa wamemweleza kuwa baadhi ya huduma za matibabu hazitolewi kwa wakati.

"Wagonjwa wanasema, mjonjwa anaweza kukaa hadi miezi mitatu akisubiri matibabu ya kupigwa mionzi, kutokana na Taasisi kuwa na mashine tatu tu za kufanya matibabu hayo. Hii siyo hali nzuri kwa taasisi kama hii ambayo ni tegemeo kubwa karibu Tanzania nzima", alisema Choughule.

"Mimi kama kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi naiomba Serikali ichukue hatua za makusudi ili angalau adha hii ipungue kwa wagonjwa, kwa sababu ni jambo la kusikitisha mtu kukaa wodini miezi mitatu hajapata matibabu kwa sababu ya upungufu wa vitendea kazi.

Mbali na vitendea kazi kuonekana ni vichache lakini inaonyesha pia kuwa madaktari ni wachache kulingana na kiwango cha idadi ya wagonjwa katika taasisi hiyo, hivyo pia kwa hilo tunaiomba serikali ifanye jitihada za kuongeza wataalam hao" alisema.

Choughule ambaye amechaguliwa hivi karibuni, alitembelea wagonjwa katika Taasisi hiyo baada ya kukabidhi kwa uongozi, msaada wa vyakula ambavyo ni pamoja na unga, maharage, mafuta ya kupikia na sabauni kwa ajili ya huduma ya chakula cha wagonjwa kwenye kituo hicho.

"Badala ya kufanya sherehe ya siku yangu ya kuzaliwa ambayo ni tarehe na mwezi kama wa leo (Agosti 27) nikiwa na Ndugu na rafiki  zangu nimeona afadhali ninunue chakula hiki, na kuwazawadia hawa ndugu zetu waliolazwa katika taasisi hii wakihangaishwa na ugonjwa huu mbaya wa saratani", alisema Choughule.

Alisema, mbali na kujisikia faraja kusaidia wagonjwa, lakini anajisikia faraja zaidi kwa kuwa anawasaidia akiwa kiongozi wa CCM, Chama ambacho alisema ni chama cha wanyonge na wenye shida.

Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kivukoni, Sharik Choughule akikabidhi maharage kwa Ofisa Muuguzi Msaidizi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, leo, alipofika kutoa msaada wa vyakula ikiwemo unga, mchele, maharage na mafuta.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช