.

UINGEREZA YAIPA TANZANIA MSAADA WA SHY TRILIONI MOJA

Aug 23, 2017

IKULU, DAR ES SALAAM
Uingereza imetoa msaada wa Dola za Marekani Milioni 450 sawa na takribani Shilingi Trilioni 1 za Tanzania kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.


Taarifa iliyotolewa leo na Ikulu jijini Dar es Salaam, imesema, msaada huo umetangazwa leo tarehe 23 Agosti, 2017 na Waziri wa Nchi anayeshughulikia maendeleo ya kimataifa na masuala ya Afrika katika Ofisi ya Mambo ya Nje na Jumuiya ya Madola ya Uingereza Mhe. Rory Stewart muda mfupi baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar es Dar es Salaam.

Mhe. Rory Stewart amesema fedha hizo zitaelekezwa katika maeneo mbalimbali ya maendeleo hususani katika kuinua ubora wa elimu na kuongeza idadi ya watoto wanaopata elimu, kuimarisha miundombinu hasa barabara na bandari, kuinua kilimo cha kibiasharana viwanda kama vile viwanda vya pamba na nyama.

Mhe. Rory Stewart amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kazi kubwa iliyofanywa na Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa na hatua zilizochukuliwa kuimarisha elimu kwa kuwapa nafasi Watanzania wengi zaidi kupata elimu.

“Nimetembelea shule moja hapa Dar es Salaam jana, na nimejionea jinsi sera ya kutoa elimu bila malipo ilivyoleta mabadiliko makubwa katika kuongeza idadi ya wanafunzi, nimezungukia shule, nimezungumza na wazazi na nimezungumza na walimu, idadi ya wanafunzi imeongezeka karibu mara mbili, hili ni jambo kubwa sana kutokea kwa muda mfupi na linaleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu, elimu ni kila kitu”amesema Mhe. Rory Stewart.

Amebainisha kuwa wananchi wa Uingereza wanaipenda Tanzania na Serikali yao itaendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali ya uhusiano na ushirikiano na kwamba ana matumaini kuwa msaada ilioutoa utasaidia kuinua uchumi na maisha ya Watanzania.

Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rory Stewart kwa kuja nchini na amemuomba ampelekee shukrani zake kwa Malkia Elizabeth II na Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe. Theresa May kwa msaada mkubwa uliotolewa kwa lengo na kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Mhe. Rais Magufuli amesema Uingereza ndio nchi inayoongoza kwa uwekezaji hapa nchini na amemhakikishia Mhe. Rory Stewart kuwa Tanzania inatambua mchango mkubwa wa nchini hiyo katika maendeleo ya Tanzania.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametaka Watanzania waelewe kuwa hatua zinazochukuliwa na Serikali dhidi ya rushwa zina manufaa makubwa kwa nchi na amesema Serikali itahakikisha fedha za msaada zilitolewa na Uingereza zinasimamiwa vizuri.

“Na ndio maana tuwaomba Watanzania waendelee kutuunga mkono katika mapambano dhidi ya rushwa, rushwa ni ugonjwa mbaya sana, tukijisafisha katika rushwa nchi yetu itakwenda mbele, katika juhudi tunazofanya wapo wengine wanalalamikalalamika lakini matokeo yake ni makubwa na ndio maana ndugu zetu Waingereza wanaona.

“Pia nitoe wito kwa Watanzania kulipa kodi, hatuwezi siku zote tukawa tunategemea kodi za kutoka kwa nchi marafiki kama Uingereza, ni lazima tujenge mazingira ya Watanzania kuamini kuwa kulipa kodi ni kitu muhimu katika maendeleo yao” Amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. Sarah Cooke, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช