Breaking News

Your Ad Spot

Oct 19, 2017

MAJADILIANO YA MAKINIKIA YAMALIZIKA KWA MAFANIKIO MAKUBWA

Rais Dk. John Magufuli, akishuhudia wakati Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi (Wapili kushoto) na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick Gold, Prof. John Thornton (wapili kulia) wakitia saini ripoti ya majadiliano kati ya Tanzania na Kampuni hiyo, Ikulu jijini Dar es Salaam, leo. Kulia ni Ofisa uendeshaji wa Barrick Richard William  na kushoto ni Mmoja wa waliokuwa wawakilishi wa Tanzana katika majadiliano hayo Prof. Florens Luoga.
-------------------------------------------------------------------------------------- DAR ES SALAAM, TANZANIA
Majadiliano kati ya Tanzania na timu ya wawakilishi wa kampuni ya Barrick Gold inayomiliki migodi ya madini hapa nchini yamekamilika na makubaliano kati ya pande hizo yametiwa saini leo19 Oktoba 19, 2017 mbele ya Rais Dk. Johne Magufuli Ikulu, Jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu imesema timu ya Barrick Gold Corporation imeongozwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni hiyo Prof. John Thornton wakati timu iliyowakilisha Serikali ya Tanzania imeongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi.

Miongozi mwa mambo waliyokubaliana ni kutekeleza mwelekeo mpya wa biashara ya madini ambapo kutakuwa na mgawanyo sawa wa faida (yaani Tanzania kupata asilimia 50 na Barrick Gold Corporation kupata asilimia 50 ya faida) na kuundwa kwa kampuni ya ubia wa usimamizi wa migodi ya madini iliyopo Tanzania ambayo itakuwa na makao makuu yake Mwanza na ofisi ndogo Dar es Salaam nchini Tanzania badala ya nchini Uingereza.

Mengine ni kufunga ofisi za uhasibu na fedha zilizopo Johannesburg Afrika Kusini na kuhamishia Tanzania na kutekeleza masharti yote ya mabadiliko ya sheria mpya ya madini na rasilimali za nchi ya mwaka 2017.

Aidha, Barrick Gold Corporation imekubali kuwepo kwa wawakilishi wa Serikali katika bodi za migodi yake yote hapa nchini, kazi mbalimbali za kwenye migodi kufanywa na kampuni za Kitanzania, Migodi kutoa ajira za kudumu kwa wachimbaji, wachimbaji hao kuishi majumbani kwao badala ya kuishi kwenye makambi ya migodi na mashauri yote ya kesi mbalimbali kufanywa hapa nchini.

Kampuni ya Barrick Gold pia imekubali kutoa Dola za Kimarekani Milioni 300 sawa na takribani Shilingi Bilioni 700 kama malipo ya kuonesha nia njema ya kufidia fedha zilizotokana na upotevu wa mapato kupitia biashara ya kampuni hiyo.

Akizungumza baada ya kutia saini makubaliano hayo Prof. Thornton amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa msimamo wake unaojenga misingi ya biashara ya kuaminiana na uwazi, ambayo ni muhimu na ya namna yake kwa biashara katika karne hii ya 21.

Prof. Thornton amesema Barrick Gold Corporation watazingatia makubaliano haya na wanaamini kuwa yamefungua ukurasa muhimu utakaowezesha kufanya biashara kisasa.

Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amezipongeza timu zote mbili yaani Tanzania na Barrick Gold Corporation kwa kazi kubwa ziliyofanya kufikia makubaliano hayo na kwa kipekee amempongeza Prof. Thornton kwa nia yake thabiti ya kukubali kufanyika kwa mazungumzo na kukubali mambo yaliyofikiwa.

Mhe. Rais Magufuli amesema makubaliano hayo yataisaidia nchi kuzalishaji ajira zaidi, kupata manufaa mbalimbali yanayostahili ikiwemo fedha za kugharamia huduma za kijamii kwa wananchi na yanajenga msingi imara ambao utaiwezesha Tanzania kunufaika na rasilimali zake za madini.

Mhe. Dkt. Magufuli amemuagiza Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Kabudi kuunda timu zitakazoshughulikia biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi pamoja na migodi mingine ya dhahabu haraka iwezekanavyo ili nchi iweze kunufaika ipasavyo.

“Nataka machimbo yote ya dhahabu mchakato kama huu ufanyike, pia nakuagiza Prof. Kabudi biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi nako ni lazima kufuate utaratibu huu, asiyetaka aondoke” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Pia Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi hizi badala ya baadhi yao kuzibeza kwa kuwa zina manufaa kwa taifa na wananchi wake.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages