.

RAIS DK MAGUFULI ATUMA SALAM ZA RAMBIRAMBI AJALI YA DALADALA MWANZA

Oct 9, 2017

IKULU DAR ES SALAAM
“Kwa mshtuko na masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya vifo vya watu 12 waliopoteza maisha baada ya gari la abiria walilokuwa wakisafiria kutumbukia katika ziwa Victoria Mkoani Mwanza, nawapa pole sana wote waliopoteza jamaa zao katika ajali hii, nawaomba wawe na moyo wa uvumilivu, ustahimilivu na subira katika kipindi hiki cha majonzi”

Hiyo ni sehemu ya salamu za rambirambi alizozitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella kufuatia ajali ya basi la abiria (Daladala) lililozama katika ziwa Victoria baada ya kugonga vizuizi vya kivuko cha Kigongo Wilayani Misungwi na kisha kutumbukia na kuzama majini.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu jijini Dar es Salaam, leo imesema Rais Magufuli amemtuma Mongella kufikisha salamu zake za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wote waliopatwa na msiba huu na amesema anaungana nao katika maombolezo.

Aidha, Rais Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na majeruhi watatu walionusurika katika ajali hii wapone haraka ili waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª