Breaking News

Your Ad Spot

Oct 20, 2017

RAIS DK. MAGUFULI ATUMA SALAM ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA ASKOFU MSEMWA

RAIS DK. JOHN MAGUFULI
IKULU, DAR ES ASALAAM
Rais Dk. John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Mhashamu Tercisius Ngalalekumtwa kufuatia kifo cha Askofu wa Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi Mhashamu Castory Msemwa, kilichotokea jana Oktoba 19, 2017 nchini Oman.

Mhashamu Askofu Castory Msemwa amefariki dunia Mjini Muscat akiwa safarini kuelekea nchini India kwa Matibabu.

"Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Baba Askofu Msemwa, kilichotokea huko Oman, Baba Askofu Msemwa ametoa mchango mkubwa sio tu katika kutimiza majukumu yake ya huduma za kiroho bali pia katika kuisaidia jamii kupata huduma mbalimbali anazostahili binadamu na amekuwa akitoa ushirikiano mkubwa kwa taasisi nyingine zikiwemo za Serikali katika kudumisha amani, upendo, umoja na kuwahudumia wananchi, mchango wake utakumbukwa daima" Taarifa iliyotolewa na Ikulu jijini Dar es Salaam, imemkariri Rais Dk Magufuli akisema.

Taarifa hiyo imesema, Rais Magufuli amemuomba Rais wa TEC Mhashamu Tercisius Ngalalekumtwa kumfikishia pole nyingi kwa Maaskofu wote wa TEC, Mapadre, Makatekista na waumini wote wa Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi kwa msiba huu mkubwa uliotokea na amesema anaungana nao katika kipindi cha majonzi na maombi kwa Marehemu.

"Raha ya milele umpe ee Bwana na mwanga wa milele umuangazie, Marehemu Askofu Castory Msemwa apumzike kwa amani, Amina"  Amemalizia Rais Magufuli.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages