Breaking News

Your Ad Spot

Jan 24, 2018

SERIKALI YAMPANDISHA MTU KIZIMBANI KWA KUTOA TAARIFA ZA UONGO

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, DODOMA

Serikali imemshtaki John Hima (29) kwa kosa la kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Namba 9 ya mwaka 2015.

Akisoma kesi hiyo namba 9 ya mwaka 2018 katika Mahakama ya Wilaya ya Bahi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Suniva Mwajumbe, Inspekta Msaidizi Amani amesema kuwa mshtakiwa ametenda kosa hilo Januari 7 mwaka huu katika kijiji cha Nghulukano, Kata ya Chikola, Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa mshitakiwa ni mwajiriwa wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) akiwa ni mkusanya taarifa (mdadisi) katika Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi wa Mwaka 2017/2018 kwa Tanzania Bara. 

Hata hivyo baada ya kusomewa mashtaka hayo, Mdadisi Hima alikana mashitaka na kesi hiyo itasomwa tena tarehe 7 Februari, 2018 ambapo amerudishwa rumande baada ya kukosa wadhamini.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama, Mwanasheria wa NBS Oscar Mangula amesema kuwa, mtuhumiwa Hima aliingia mkataba na NBS kuwa mmoja wa wadadisi wa Utafiti huo unaoendelea hivi sasa ambao ulianza Desemba mwaka jana.

“Kwa mujibu wa sheria akiwa kama mdadisi majukumu yake alitakiwa kuwa katika eneo la kazi kulingana na mkataba na kiapo alichopata  ambapo yeye kwa makusudi aliamua kutelekeza majukumu hayo na kuwa nje ya kituo cha kazi hivyo kwa mujibu wa sheria ya Takwimu ametenda kosa la kijinai” amesema Mwanasheria Mangula.

Mwanasheria Mangula ameongeza kuwa, “Mkataba wa kazi ni wa miezi 12 ambapo ulianzia Desemba 2017 hadi Novemba 2018 lakini mdadisi huyu aliacha kutimiza majukumu yake kuanzia tarehe 7 Januari ambapo sisi tulifika pale tarehe 13 na 14 Januari mwaka huu ila hakuweza kufanya kazi yake kama ilivyotakiwa”.

Mwanasheria Mangula alieleza kuwa kesi hiyo inawakumbusha wadadisi waliopewa jukumu la kukusanya taarifa za kitakwimu kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mikataba yao ya ajira, kiapo na mafunzo waliyopewa ili kuepuka kutenda makossa ya kijinai kama analodaiwa kutenda na mtuhumiwa. 

Aidha, inawakumbusha wananchi umuhimu wa kuendelea kutoa ushirikiano kwa wadadisi mbalimbali wanaopewa jukumu la kukusanya taarifa za kitakwimu kwani kufanya hivyo ni kutekeleza matakwa ya Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages