.

OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI KUENDELEZA USHIRIKIANO NA VYOMBO VYA UTOAJI HAKI

Feb 16, 2018

Na Mwandishi Maalum
Mwanasheria  Mkuu wa  Serikali  Mhe.  Dk.Adelardus  Kilangi,  amesema,  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  itaendelea kushirikiana na kufanya  kazi kwa karibu na  Mahakama ya  Afrika  ya Haki za Watu na Binadamu ( AfCHPR)  pamoja na Mahakama ya Haki ya  Afrika   Mashariki ( EACJ).

Ametoa uhakikisho huo kwa nyakati tofauti wakati alipokutana na kufanya  mazungumzo na   Marais wa Mahakama  hizo   Jijini Arusha, akiwa katika ziara ya kujitambulisha.

" Napenda niwahakikishie kwamba, Serikali na Ofisi yangu tutaendelea kushirikiana na kufanya kazi  nanyi  ili  kwa  pamoja tutekeleze majukumu yaliyombele yetu kwa ufanisi na katika  ukamilifu wake". Akasisitiza  Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kwa upande wake  Rais wa  Mahakama ya Haki ya Afrika  Mashariki Mhe.  Jaji Dk.Emmanuel Ugirashabuja,  amemueleza Mwanasheriak Mkuu  wa  Serikali kwamba, Mahakama hiyo inazitigemea  Ofisi  za Wanasheria  Wakuu wa Serikali ikiwamo  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Tanzania katika utekelezaji wa majukumu yake na kwamba, ushirikiano   baina ya   pande hizo mbili ni jambo la muhimu sana.

Naye Rais wa  Mahakama ya Afrika ya Haki za Watu na  Binadamu, Mhe.Jaji  Sylvain Ole amebainisha  kuwa  Mahakama hiyo imekuwa  ikipata  ushirikiano mzuri kutoka Tanzania ikiwemo  Ofisi  ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

" Tumekuwa  tukipata ushirikiano  mzuri kutoka   Ofisi ya  Mwanasheria  Mkuu wa Serikali  ambapo Mawakili wa Serikali   wamekuwa wakiiwakilisha vema Serikali katika  Mashauri  mbalimbali". Amesisitiza Jaji Sylvan Ole.

Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali moja ya majukumu yake ya msingi ni kuiwakilisha Serikali  katika  mashauri mbalimbali yanayofunguliwa dhidi ya  serikali  katika Mahakama  ya Haki ya Afrika  Mashariki na  Mahakama ya  Afrika ya Haki za Watu na Binadamu.

Katika ziara yake hiyo, Mwanasheria  Mkuu wa Serikali pamoja na kufanya mazungumzo na viongozi  mbalimbali pia alipata fursa ya kutembelea   na kujionea utendaji kazi wa mahakama   pamoja  na mfumo wa  habari na mawasiliano wa mahakama hiyo  unavyofanya kazi.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª