Breaking News

Your Ad Spot

Feb 15, 2018

TRA KUWAFUTIA LESENI MAWAKALA WA FORODHA WADANGANYIFU

Na Rachel Mkundai, Tunduma
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere ametishia kuwafutia leseni mawakala wa forodha wanaofanya udanganyifu katika kadhia za wateja wao wanazoziwasilisha katika ofisi za TRA pindi wanapotoa au kuingiza mizigo nchini kwani hizo ni njama za kuwepa kodi.
Bw. Kichere ametoa onyo hilo alipokuwa akizungumza na mawakala wa forodha wanaofanya shughuli zao katika mpaka wa Tanzania na Zambia uliopo katika mji mdogo wa Tunduma mkoani Songwe akiwa katika ziara yake kutembelea mikoa ya nyanda za juu kusini.
Kamishna Kichere amesema kumekuwepo na baadhi ya mawakala wa forodha ambao huwasilisha nyaraka zenye taarifa za uwongo au zinazoonesha idadi pungufu ya bidhaa zilizopo kwenye mizigo tofauti na uhalisia.
“Kusema ukweli sitawavumilia maajenti (mawakala) ambao watakuwa wanaongepea serikali, nitafuta leseni zao, tukiwakamata mnaenda kubumba bumba nyaraka zenye ankara za uwongo, nitafuta leseni” alisisitiza Kamishna mkuu wa TRA.
Hali kadhalika, Kichere amewataka mawakala wa forodha hao kushirikiana na maafisa wa TRA kwa kutoa taarifa sahihi za kadhia za wateja wao ili waweze kukadiriwa kodi stahiki wanayotakiwa kulipa na kuilipa kodi hiyo kwa hiyari kwa kuwa wote ni watanzania wanaoshirikiana kujenga taifa moja.
Nao mawakala wa forodha katika mpaka wa tunduma wameufurahia ujio wa kamishna mkuu na kuahidi kushirikiana na maafisa wa TRA kwa kuwa taasisi hiyo ni kiungo muhimu kati yao na wateja wao.
Mmoja wa mawakala hao Bw. Edwin Mwendo amesema ni vyema mawakala wakatimiza wajibu wao kulingana na taratibu za forodha kwa kuepuka rushwa na kuwasilisha kadhia zenye taarifa sahihi ili kuepuka mkono wa sheria endapo watabainika kuwa wanakwepa kodi.
Mwakilishi mwingine wa wakala wa forodha Bw. Alan Upamba amesema ili kuepuka migongano katika kazi za forodha ni vyema pande zote mbili za maofisa wa TRA pamoja na mawakala kufuata taratibu zote za kiforodha ambazo zitapelekea ukusanyaji mzuri wa kodi na hivyo kuleta maendeleo kwa taifa.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ndiyo yenye mamlaka ya kuwasajili Mawakala wa forodha nchini na wanatakiwa kufanyakazi kwa mujibu wa Sheria na taratibu za forodha na kuhakikisha kodi sahihi inalipwa kwa Serikali bila kukwepa.  

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages