.

PROGRAMU MAALUM YA ELIMU BURE KWA WAFUGAJI NA WAVUVI NCHI NZIMA YAZINDULIWA, WAZIRI APEWA JINA LA 'OLE MPINA'

Apr 12, 2019

Waziri wa mifugo na Uvuvi, Luhaga  Mpina akizindua program ya kitaifa ya mafunzo kwa wafugaji nchi nzima  katika  kijiji cha Kimotorok wilayani Simanjiro.
=======
Na John Mapepele
Wizara imeanza program maalum ya kuwafundisha wafugaji na wavuvi nchini kote kuhusu sheria za mifugo na uvuvi na sheria nyingine, ili kuwawezesha kujua haki zao na kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

Hatua hiyo inasaidia sana wafugaji kujiepusha  na migogoro baina yao na watumiaji wengine  wa ardhi, na  kwa upande wa uvuvi  watafundishwa  ufugaji bora wa samaki, utekelezaji wa sheria na kanuni za uvuvi, udhibiti wa ubora wa mazao ya uvuvi na ushirika wa wavuvi ili kuboresha maisha yao.   
Akizindua programu ya mafunzo hayo Kitaifa katika Kijiji cha Kimotorok Wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina alisema mafunzo kwa wafugaji pia yatawezesha wafugaji kutambua namna ya kutumia fedha zitokanazo na mifugo na mazao yake kwa kuwekeza maeneo mengine kujenga makazi bora, kusomesha watoto, kukata bima ya mifugo na kujiwekea akiba benki.

“Leo tunaanza kuzindua mafunzo kwa wafugaji lengo likiwa ni kuwawezesha kuzijua sheria za mifugo na kutambua haki zao ili kujiepusha na migogoro baina yao na majirani zao wakiwemo wakulima, wahifadhi pamoja na kuelimishwa mbinu za kisasa za namna ya kuboresha maisha na ufugaji",  Alisisitiza Mpina

Alisema kwa pande ufugaji sheria zitakazofundishwa kuwa ni pamoja na Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Namba 17 ya mwaka 2003, Sheria ya Ustawi wa Wanyama namba 19 ya mwaka 2008, Sheria ya Nyanda za Malisho na Raslimali za Chakula cha mifugo Namba 13 ya mwaka 2010 pamoja na Sheria ya Wanyama pori Namba 5 ya Mwaka 2009.

Pia wafugaji hao watafundishwa namna ya kudhibiti magonjwa ya kimkakati 12 ambayo yanadhibitiwa kwa njia ya chanjo ikiwemo Sotoka ya mbuzi(PPR), Homa ya mapafu ya ng’ombe(CBPP), Ugonjwa wa miguu na Midomo(FMD), Homa ya mapafu ya Mbuzi(CCPP),Mdondo(ND)Homa ya Bonde laUfa(RVF).

Magonjwa mengine ni Mapele ya Ngozi (LSD) Homa kali ya Nguruwe(ASF) Ndigana Kali (ECF) Kimeta(Anthrax), Kichaa cha Mbwa (Rabbies) na ugonjwa wa  wa kutupa mimba(brucullosis) na kuokoa vifo vingi vya mifugo vinavyosababishwa na magonjwa hayo.

Pia wafugaji watafundishwa matumizi sahihi ya dawa,chanjo na viuatilifu vya mifugo nchini,uzalishaji wa mbegu bora  za malisho, utunzaji wa nyanda za malisho na machunga , ufugaji kibiashara na kuweka  utaratibu wa kuvuna mifugo na kuanzisha  ushirika wa wafugaji.

Hivyo Waziri Mpina aliwahimiza wafugaji kote nchini kuchangamkia mafunzo hayo kwani ndio yatakayokuwa mkombozi baada ya kuishi kwa zaidi ya mika 50 hivyo Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imedhamiria kwa dhati kuwakomboa kutoka kwenye dhiki na dhuluma waliofanyiwa.

Pia Waziri Mpina alimwagiza Katibu Mkuu wa Mifugo kuhakikisha anakarabati bwawa la Narakauo katika Kijiji cha Loibosoit kwenye Wilaya ya Simanjiro katika kipindi cha miezi miwili toka sasa ili kutatua tatizo sugu la maji kwa ajili ya kunywesha mifugo na binadamu.

Mpina alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Yefled Myenzi kufanya marekebisho kwa majosho yote yaliyoharibika kabla ya Juni 30 mwaka huu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha wafugaji nchini George Bajuta aliishukuru Wizara ya Mifugo kwa uamuzi wake wa kuanzisha mafunzo hayo kwa mara ya kwanza ambayo hayajawahi kutolewa kwa wafugaji nchini na kwamba yatawasaidia kubadilisha maisha ya wafugaji ambao walikuwa wakidharaulika na kufukuzwa kila mahali walipokuwa wanakwenda kwa ajili ya  shughuli za ufugaji.

Pia alimwomba Waziri Mpina kuandaa mwongozo utakaosaidia kuondoa tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali kukamata hovyo mifugo kuitesa kwa muda kwa muda mrefu huku mingine ikipotea kwa kutaifishwa.

Mafunzo ya sekta za Mifugo na Uvuvi yataendeshwa katika Wilaya zote 185 nchini na yatawafuata wafugaji na wavuvi kwenye maeneo yao na kwa kuanza kwa upande wa mifugo  yatatolewa kwenye wilaya mbili za awali za Simanjiro na Kaliua mkoani Tabora, ambapo kwa upande wa  Sekta ya Uvuvi mafunzo ya awali yatatolewa kwenye  katika  wilaya za Mafia, Bagamoyo, Mkuranga, Kigambni na Kinondoni.
=====
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akivishwa shuka  la Kimasai na mzee wa mila wa kabila hilo Ezekiel Lesenga, kumsimika katika uongozi wa sekta na kupewa jina la Ole Mpina,  wakati wa  uzinduzi wa program ya kitaifa ya mafunzo kwa wafugaji nchi nzima  katika  kijiji cha Kimotorok wilayani Simanjiro.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga  Mpina akiwahutubia wafugaji wa  kijiji cha Kimotorok wilayani Simanjiro wakati wa uzinduzi wa program ya kitaifa ya mafunzo kwa wafugaji nchi nzima.

NEEMA YA VIWANDA VIKUBWA VYA NYAMA DUNIANI YATUA NCHINI

Apr 4, 2019

>Ni kutokana na mapinduzi makubwa Wizara ya Mifugo ndani ya  mwaka mmoja.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina  (Mwenye koti la bluu) akitoa kitambaa  kwenye jiwe la msingi kuashiria uzinduzi wa Kiwanda cha Nyama cha Tan Choice Kibaha  mkoani Pwani chenye uwezo wa kuchinja ng’ombe 100-1500 kwa siku na mbuzi 4000-4500 kwa siku.

Na John Mapepele
Mapinduzi makubwa yanayofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika udhibiti wa magonjwa, bidhaa za mifugo zinazoingia nchini kinyume cha sheria, uboreshaji wa mbali za mifugo, utoroshaji wa mifugo nje ya nchi,  uzalishaji wa mifugo na uzalishaji wa malisho bora ya mifugo vimeanza kuwavutia wawekezaji wa viwanda vya nyama kuja kuwekeza na kutoa ajira kwa wanachi na kuchangia kwenye mapato ya Serikali ya awamu ya tano.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina kwa  nyakati tofauti wakati alipokuwa akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa kiwanda cha nyama cha Tan choice Tanzania, ambacho ni kikubwa kuliko viwanda vyote Afrika Mashariki na Kati kinachojengwa Kibaha Pwani na wakati wa utiaji wa saini makubaliano  awali baina ya Tanzania na Misri ujenzi wa miongoni mwa miradi mikubwa barani Afrika wa kiwanda cha uchakataji wa nyama na utengenezaji wa  bidhaa mbalimbali zitokanazo na Ngozi.

Mpina amesema kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, dunia imeshuhudia uanzishwaji wa  miradi mikubwa  miwili ya viwanda vya kuchakata nyama ndani ya wiki moja ambapo kumekuwa na uwekaji wa jiwe la msingi na utiaji saini wa makubaliano ya ujenzi ambayo itakuwa na manufaa kwa pande zote.

“Ujenzi wa kiwanda cha hiki unapeleka salamu njema kwa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC),SADC,IGAD na mataifa mengine ambayo inategemea mazao ya mifugo kutoka Tanzania aliongeza Mpina.

Amesema kukamilika kwa viwanda hivyo viwili kutawezasha kuchinja zaidi ya ngombe 3000 mbuzi  na kondoo 10000 kwa siku ambapo pia itatoa ajira za kwa watanzania zaidi ya watu 6000. 

"Ilani ya CCM ibala ya 8 (d) na 25(p) inatusisitiza sana sisi sote tuliopewa dhamana, kuhamasisha sekta binafsi kujenga viwanda vya nyama ili kuongeza thamani na kukuza uchumi wa nchi na wadau katika mnyororo mzima wa thamani"
alisisitiza Mpina kwenye hotuba yake ya uwekaji wa jiwe la msingi kwenye kiwanda cha Tan Choice.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha nyama cha Tan choice Tanzania Rashid Abdilah ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutoa miongozo  na  ushirikiano wa karibu ambao umewawezesha kujenga  kiwanda  na kufikia asilimia 85  ndani ya miezi sita na kuahidi kukamilisha kiwanda hicho na kuanza uzalishaji ifikapo agosti 2020. 

Akizungumza  mara baada ya kushuhudia utiaji wa  saini makubaliano ya awali ya kiwanda cha Ruvu Intergrated Industry Waziri Mpina amesema  kiwanda  hicho ni cha aina yake, ambapo ngombe wazima wataletwa na kupumzishwa katika eneo maalum kabla ya kuchinjwa(holding ground) hatimaye watachinjwa na mwisho kupata nyama yenye kiwango cha kimataifa(ISO) na hadhi  ya kuwa na ithibati ya halal.

Aidha amesema kiwanda hicho kikianza kufanya kazi kitafanya kazi ya kutengeneza  bidhaa nyingine za mifugo kama mikanda mikoba na viatu na chakula cha  mifugo.

Amesema asilimia 1.4 ya mifugo yote duniani inapatikana Tanzania na asilimia 11 ya  mifugo yote Afrika ipo Tanzania hivyo  kuna  uhakika wa malighafi ya kutosha  kwa ajili ya viwanda vinavyoanzishwa ambapo alitoa muda usiozidi  miezi mitatu kwa  timu ya wataalam wa Tanzania na Misri kukamilisha  mara moja na upembuzi yakinifu ili mkataba rasmi wa ubia (Joint Venture Agreement) na uendeshaji wa kiwanda uwe umesainiwa.

Aidha, Mpina aliiomba Serikali ya Misri kuendelea kuwekeza katika maeneo mengine  ya mifugo na uvuvi hususan  katika uendeshaji wa shirika  la Uvuvi Tanzania(TAFICO) ambalo Serikali tayari imeshalifufua, Hiifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, viwanda vya kuchakata samaki, ufugaji wa samaki baharini na maji  baridi.

Amesema  fursa za uvuvi wa ukanda  wa uchumi wa Bahari Kuu(EEZ) ni kubwa kwa Tanzania kuwa eneo la kilomita 223,000 unafaa kwa ajili ya uvuvi wa samaki aina ya Jodari na utalii wa majini unaojali mazingira.

Kwa upande wake Balozi wa Misri Abulwafa amesema hatua ya uwekaji wa saini hati ya makubaliano hayo ni kielelezo cha ushirikiano uliodumu  kwa zaidi ya miaka 50 baina ya nchi zote mbili.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji Mahmoud Mgimwa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Pwani Ramadhani Maneno walipongeza   hatua ya Wizara  ambapo walisema kuwa wizara inatekeleza 

Chimbuko la mradi ujenzi wa kiwanda cha Ruvu ni kutokana na mashirikiano mazuri na majadiliano baina ya Rais Dk.John Pombe Joseph Magufuli na Rais wa Misri Abdel Fattah  El Sis  yaliyofanyika Agosti 2017 na  pia kufuatia  kikao cha ujumbe wa Waziri wa Mifugo wa Misri Desemba 2018 na Waziri Mpina ofisini kwake jijini Dodoma.

Utiaji wa saini kwa mradi huo umefanywa na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa(NARCO) Profesa Philemoni Wambura na Mwenyekiti wa Kampuni ya NECAI ya Misri, Ahmed Hassan Mohamed katika hafla iliyofanyika kwenye Ofisi  ndogo za Wizara ya Mifugo jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Mwanzoni mwa wiki hii, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli amewaagiza viongozi wote nchini kuhakikisha  wanaondoa  vikwazo vyote dhidi ya wawekezaji ambao wanadhamira ya dhati ya kuwekeza katika maeneo mbalimbali  ya kuimarisha uchumi, kuzalisha ajira, kuongeza mapato ya Serikali na kustawisha  maisha ya wananchi wakati akifunguakiwanda cha kubangua Korosho chaYalin Cashenut Company Ltd  kilichopo eneo la Msijute Mtwara vijijini.
ยช