Breaking News

Your Ad Spot

Mar 1, 2010

AJALI YAUA 21 KITANGIRI TABORA

WATU 21 wamekufa na wengine 45 wamejeruhiwa katika ajali ya basi iliyotokea eneo la Kitangiri, kati ya Nzega na Igunga, mkoani Tabora.
     Ajali hiyo iliyotokea jana, ilihusisha basi la Kampuni ya AM aina ya Scania, lenye namba za uzajili T 316 AZR.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora Liberatus Barlow, akizungumza na Uhuru kwa njia ya simu jana usiku, alisema ajali hiyo ilitokea saa 10.15 jioni wakati basi hilo lilipokuwa likisafiri kutoka Arusha kwenda Mwanza.
     Alisema kati ya waliopoteza maisha, 12 ni wanaume, wanawake watano na watoto wanne, wawili wa kike na wa kiume wawili.
     Kamanda Barlow alisema majeruhi ambao hali zao ni mbaya wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora.  Kwa mujibu wa Kamanda Barlow, maiti zimehifadhiwa katika hospitali hiyo.
     Alisema baadhi ya majeruhi walisema ajali hiyo ilisababishwa na mwendo kasi wa dereva. Barlow alipozungumza na Uhuru alisema alikuwa njiani akielekea eneo la tukio.
     Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), wamekuwa wakiweka mikakati kadhaa ya kudhibiti ajali.
      Miongoni mwa mikakati hiyo ni ufungaji wa vidhibiti mwendo, jambo ambalo limekuwa likipata upinzani kutoka kwa wamiliki wa mabasi.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages