azam

FLAVIAN MATATA KUNADI VIVUTIO VYA UTALII KIMATAIFA

Jan 25, 2015

Na mwandishi wetu
MWANAMITINDO maarufu nchini anayetamba Marekani, Flaviana Matata, atashiriki kwenye tangazo la kunadi vivutio vya utalii.

Tayari wataalamu wa kampuni ya Pursuit Productions ya nchini Marekani, wameanza kazi ya kuandaa tangazo hilo visiwani jana.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema jana kuwa, hatua hiyo ni mkakati wa kukuza na kuendeleza utalii wa Tanzania ndani na nje ya nchi.

Alisema wizara yake itaendelea kutekeleza mikakati hiyo kwa lengo la kuvutia watalii hasa wa nje na kwamba, ana uhakika hilo litafanikiwa.

Miongoni mwa mikakati inayotekelezwa kwa sasa wizara hiyo ni pamoja na kutangaza vivutio vya utalii nchini kupitia viwanja vikubwa vya michezo Barani Ulaya na Marekani.

Alisema kampuni ya ambayo pia inafanya kazi na wasanii wakubwa wa Hollywood, wanaendelea na kazi ya utayarishaji wa tangazo hilo kisha watakwenda Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Nyalandu alisema tangazo hilo litainadi Tanzania na vivutio vyake katika televisheni kubwa za kimataifa na pamoja na zile za hapa nchini.

“Wataalamu wa Hollywood wapo Zanzibar na wameanza kazi hiyo leo (jana), litakuwa tangazo zuri na litakalotangaza vivutio vyetu vyote vya utalii kimataifa.

“Tangazo hili ni mkakati wa kuendelea kunadi vivutio vyetu na kuvutia wageni wengi zaidi, litakuwa fupi na lenye kuvutia zaidi,” alisema Nyalandu.

Alisema matayarisho ya tangazo hilo yatachukua wiki tatu hadi kukamilika kwake na kwa kuanzia litarushwa kwenye luninga za CCN ya Marekani na BBC World mwezi Machi, mwaka huu.

Aliongeza kuwa mpango huo ni utekelezaji wa mkakati wake wa kuhuisha mtazamo wa dunia kuhusu Tanzania alioutangaza bungeni mwezi Juni, mwaka jana.

Alisema Flaviana, ambaye anafanya shughuli zake nchini Marekani na kuiletea sifa kubwa Tanzania, ushiriki wake katika tangazo hilo utaongeza hamasa kubwa.

“Tangazo la watanzania kwa ajili ya kuvutia watalii katika kona zote za dunia, Flaviana ni Mtanzania hivyo maslahi ya watanzania yamezingatiwa,” alisema Nyalandu.

MBATIA KUTIMULIWA UKAWA?

theNkoromo Blog
HALI inazidi kuwa mbaya ndani ya Kambi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kufuatia taarifa za mgogoro mkubwa uliopo kati ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilbroad Slaa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia.

Chanzo cha mgogoro huo ambao unafukuta, ni madai ya Slaa ya kutomwamini Mbatia anayedai ni pandikizi anayetumiwa na serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuvuruga umoja huo.

Inaelezwa, Slaa anamshutumu Mbatia kuwa ni Afisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, hivyo ni hatari kwa ustawi wa umoja huo, na kuna uwezekano akasababisha kusambaratika kwake iwapo ataendelea kuwepo.

"Ukiwa nje huwezi kuona hali halisi ya mambo, kwa tulio ndani ndio tunaona kila kitu, huu umoja hauwezi kufika popote maana watu hawaamiani hata kidogo na kuna migogoro kila kukicha"

"Sasahivi Slaa anashinikiza Mbatia aondolewe UKAWA, anadai akiachwa atavuruga mpango wa kwenda ikulu" kilisema chanzo chetu kilichopo ndani ya kambi ya UKAWA.

Chanzo hicho kilisema, msimamo huo wa Slaa umewapa wakati mgumu vongozi wengine wa kambi hiyo na wanaona wakimtosa Mbatia watasababisha mgawanyiko wa wanachama, hivyo kuna uwezekano mkubwa wakampuuza Katibu Mkuu huyo.

"Slaa hapendi kumuona Mbatia akiwa UKAWA, ila Mbatia ni muhimu zaidi kuliko Slaa kwenye umoja huu maana anawakilisha chama na iwapo chama chake kitatoka kutasababisha mpasuko, kwahiyo kuna uwezekano mkubwa wakampuuza katibu mkuu, ila wakimpuuza unamjua mambo yake, ataanza vurugu ndani ya chama" kilisema chanzo chetu.

Aidha, mbunge mmoja wa CUF akizungumza na mwandishi wa habari hizi alisema, baadhi ya wanachama wa UKAWA wanamshutumu Mbatia kuwa mmoja wa walioshinikiza kambi hiyo kususia mchakato wa Katiba mpya na kushawishi wasirudi bungeni.

"Kuna mambo yanatia mashaka sana na leo viongozi wetu wanajuta, uamuzi wa kususia bunge la Katiba haukuwa sahihi, vongozi wetu walipotoshwa kususia bunge. Naamini kama tungebakia bungeni na kushindana kwa hoja, kingeeleweka"

"Mbatia alikuwa kinara wa kusisitiza tusirudi na kuna taarifa feki zilikuwa zinakuja ambazo zilionekana wazi mchakato ungekwama, lakini tumeona kilichotokea, CCM na baadhi ya wabunge wa UKAWA wakaendelea na wameandika walichotaka, na kwa hali ilivyo katiba wanayotaka wao itapita" alisema mbunge huyo kutoka Zanzibar (jina tunalihifadhi).  

Mbunge huyo alisema, hali hiyo inaonyesha wazi kuna watu ndani ya kambi hiyo wanatumika na CCM, na mbinu ya kushawishi UKAWA wasirudi bungeni ilikuwa ni maagizo maalum yenye lengo la kuwapa nafasi CCM kupitisha mambo waliyotaka kwenye Katiba mpya.

Taarifa zaidi zinasema, jambo jingine ambalo linampotezea imani Mbatia kwa baadhi ya viongozi wenzake, ni uhusiano wake na kigogo mmoja mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), ingawa mwenyewe mara kadhaa amekuwa akikana madai hayo na kushusha lawama kwa CCM kuhusika kusambaza madai hayo.

Inaelezwa, Mbatia amekuwa karibu na kigogo huyo na wamekuwa wakikutana mara kwa mara nyumbani kwake maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupeana maelekezo ambayo hawana shaka yanalenga kufanya hujuma kwa kambi hiyo.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliozungumza na mwandishi wa habari hizi wamesema, kambi ya UKAWA ipo kwenye wakati mgumu ukiachilia mbali mgawanyiko uliopo katika suala la kuteua mgombea Urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, kuna hali ya kutoaminiana na kila mmoja anamuona mwenzake ni msaliti.

"Kabla hawajaungana Chadema waliwahi kukishutumu CUF kuwa ni tawi la CCM (CCM B), Wenje (Ezekiel Wenje) aliwahi kuwashutumu CUF kuwa ni chama cha mashoga, Chadema hao hao walishamuita Mbatia ni mbunge wa Rais Kikwete kwa kuwa aliteuliwa na Rais hivyo ni mbunge anayefuata maagizo ya CCM" alisema John Malingumu mchambuzi wa masuala ya kisiasa.

Mchambuzi huyo aliongeza kuwa, kila mmoja ndani ya kambi hiyo ameungana na mwenzake kwa malengo binafsi, ila hakuna mwenye imani na mwenzake.

"Pale kuna unafki mkubwa, kila mmoja amebaki na historia yake kichwani ya mambo ambayo walifanyiana kabla hawajaungana, utakumbuka pia Chadema waligoma kuunda Kambi ya Upinzani na CUF, haya yote hayajafutika"

MUHONGO AJIUZULU, RAIS KIKWETE AFANYA MABADILIKO MADOGO BARAZA LA MAWAZIRI

Jan 24, 2015

NA BASHIR NKOROMO, DSM
WAKATI aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ametangaza kujiuzulu, Rais Jakaya Kikwete ametangaza marekebisho madogo ya Baraza lake la Mawaziri.

Taarifa iliyotangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi  Ombeni Sefue leo, imesema, nafasi iliyoachwa na Profesa Muhongo sasa itashikwa na George Simbachewene, huku nafasi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Oratibu na Bunge ikichukuliwa na Dk. Mary Nagu.

Kulingana na taarifa hiyo, aliyekuwa Waziri wa Chakula na Kilimo Christopher Chiza anakuwa Waziri wa Uwezeshaji na Uwezeshaji, huku Dk. Harisson Mwakyembe akipewa nafasi ya Uwaziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Waziri William Lukuvu anakuwa waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Profesa Anna Tibaijuka kabla ya kujiuzulu kufuatia sakata la Tegeta ESCROW.

Naye Stephen Wasira katika mabadiliko hayo, anakuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, wakati aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta anakuwa Waziri wa Uchukuzi na Jenista Mhagama akipewa nafasi ya Uwaziri wa  Sera na Uratibu wa Bunge.

Taarifa imesema, aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba Angela Kairuki anakuwa Naibu wa Ardhi Nyumba na Makazi,  huku Steven Masele akipata nafasi ya Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano.

Wengine ni Ane Kilango Malecela anayekuwa Naibu Waziri wa Elimu, Ummy Mwalimu Naibu Waziri wa Sheria na Katiba na Mwijage Naibu Waziri wa Nishati na Madini.

NYALANDU AITISHA KIKAO KUJADILI CHANGAMOTO ZA UTALII

NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ameendelea na jitihada za kutafuta ufumbuzi wa kudumu kuhusiana na changamoto zinazowakumba wadau wa biashara ya utalii nchini.

Katika kuhakikisha hilo linafanyika kwa mafanikio na kwa haraka, Nyalandu ametangaza kuanza kwa vikao vitakavyowakutanisha wataalamu wa Wizara zinazohusika na maliasili na utalii za Tanzania na Kenya kwa lengo la kujadiliana masuala mbalimbali iili yapatiwe ufumbuzi kwa maslahi ya pande zote.

Hatua hiyo imetokana na hivi karibuni Serikali ya Kenya kuyazuia magari ya utalii kutoka Tanzania kuingiza watalii kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, hivyo kusababisha usumbufu mkubwa.

Hata hivyo, Nyalandu aliingilia kati kwa kuzungumza na Waziri wa Utalii wa Kenya, Phillys Kandie na kufikiwa kwa makubaliano ya kuruhusiwa na hapo wazo wa wizara hizo kukutana likaibuliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Nyalandu alisema vikao ya wataalamu hao vitaanza rasmi Februari 3, mwaka huu, jijini Arusha ambapo vitahusisha pia wataalamu kutoka Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Alisema vikao hivyo vitajadili masuala mbalimbali ili kuhakikisha changamoto zote zinawaikabili sekta ya utalii kwa nchi hizo mbili zinapatiwa ufumbuzi.

Aliongeza kuwa hatua hiyo pia inalenga kuimarisha ushirikiano pamoja na kuongeza ulinzi kwenye mbuga za wanyama na mapori ya akiba dhidi ya mtandao wa ujangili.

Hata hivyo, aliweka wazi kuwa hoja kuhusiana na mpaka wa Borongoja haitajadiliwa kwenye vikao hivyo kwa kuwa si sehemu ya ajenda.

“Nchi zetu hizi zinategemeana sana katika biashara ya utalii hivyo, kuna makubaliano tuliyafikia muda mrefu huko nyuma lakini yanaonekana kuanza kuwa na changamoto hivyo ni lazima tujadili ili tuweze kusonga mbele. Hatutaki watalii wanaokuja kupumzika wasumbuke kwani itakuwa ni hasara kwa wafanyabiashara wetu na kutahatarisha uchumi wa taifa…daima lazima tusonge mbele,” alisema Nyalandu.

Aliongeza kuwa baada ya mkutano wa wataalamu utafuatiwa na wa makatibu wakuu wa wizara hizo utakaofanyika Februari 4 mwaka huu kisha utahitimishwa na wa mawaziri utakaofanyika Februari 5.

Nyalandu alisema ana imani mikutano hiyo itatoka na mwanga mpya na maboresho kwa sekta ya utalii na kusisitiza maslahi ya pande zote yatazingatiwa.

Alisema kuwa nia ya Tanzania ni kuendeleza Jumuia ya Afrika Mashariki na mahusiano yake mazuri na si kugombana na kuharibu uhusiano huo.

Alisema daima Tanzania itakuwa makini kuhakikisha mahusiano yanakaa sawa katika majadiliano hayo na kwamba kusije kutokea jambo likaleta madhara kwa watu wengine.

Nyalandu aliongeza Tanzania itafanya biashara za utalii na watu wengine kuhakikisha wanaendelea kulinda rasilimali za taifa sambamba na wafanyabiashara wakubwa wa kitalii na wadogo.

KITUO CHA SHERIA NA HAKI ZA BINADAMU CHAZUNGUMZIA CHANGAMOTO ZA UTEKELEZAJI SHERIA YA MAONI YA KATIBA

Jan 23, 2015

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.Hellen Kijo-Bisimba (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi, wakati akitoa taarifa kuhusu changamoto za utekelezaji wa sheria ya kura ya maoni ya Katiba. Kulia ni Mratibu wa Katiba wa LHRC, Anna Henga na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Ezekiel Massanja.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo

Wapiga picha na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.

Dotto Mwaibale

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema kina wasiwasi na mchakato wa kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika kwa sabau ya muda mdogo ulibaki ikizingatiwa daftari la wapigakura halijafanyiwa marekebisho pia watanzania wengi hawana uelewa na katiba iliyopendekezwa.


Kituo kimetoa mapendokezo kwa Serikali kuahirisha tarehe ya kupiga kura ya maoni kwa kile kilichodaiwa katiba inayopendekezwa inamapungufu na yasiporekebishwa muda huu yanaweza kuathiri kura ya maoni na kuwakosesha watanzania wengi  kushiriki haki yao kikatiba.

Akizungumza Dar es Salaam leo Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, DK. Hellen Kijo- Bisimba alisema kituo hicho kimekuwa na utaratibu wa kufuatilia mchakato wa katiba, kubaini mapugufu mengi likiwemo la muda mdogo na wananchi wengi kutoelewa vizuri katiba inayopendekezwa.

"Mchakato wa kura ya maoni unaenda kukamilika Februari 28 kwa mjibu wa sheria ya kura hiyo.Tume ya Taifa ya Uchaguzi inapaswa kuboresha daftari la wapiga kura ndipo kura ipigwe, ukizingatia zimebaki siku takribani 25 kufikiaki hitimisho,sisi tunaona kuna changamoto ya muda na ni vyema zoezi hilo lisongezwe mbele,"alisema.

 Aliongeza kuwa vifaa vya BRV vinavyotarajiwa kutumika kwa mara ya kwanza na tume ya uchaguzi vimeonesha changamoto katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na hivyo kituo hicho kinawasiwasi na mchakato mzima wa upatikaji wa katiba iliyo bora.

"Kifungu cha 10 katika katiba inayopendekezwa kimezungumzia vituo vya kupigia kura, kwamba vitapangwa kulingana na maeneo yaliyo na watu wengi katika maeneo husika wasiwasi wangu hapa tume inaweza kutotumia majimbo ya zamani na kutengeza majimbo mpya,"alisema.

Bisimba alisema changamoto nyingine katika mchakatio huo ni Usajili wa kamati za kura ya maoni katika kuikubali au kuikataa kura hiyo katiba inaelekeza kamati ni lazima ipeleke maombi kabla ya siku 21 kupigwa kwa kura ya maoni.

"Utaratibu ambao sisi kulingana na uzoefu wetu wa kufanya kazi tunaona haya ni masharti magumu yanayoekekezwa kwenye kamati za kura, kwani inawataka pia kueleza vyanzo vya mapato yao kitu ambacho kinaweza kusababisha  kamati zingine kutopata usajili,"alisema.

Dk.Bisimba aliongeza kuwa changamoto ambayo kituo kinaona kuwa ni kiini macho ni pale inapoelezwa kwamba wanzazibar waishio Tanzania bara wakipiga kura kura zao zitahesambiwa upande wa zanzibar.
(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com)

MFALME ABDULLAH AFARIKI DUNIA

Jan 22, 2015


HAKIELIMU: UTEKELEZAJI WA BRN KATIKA ELIMU BADO HAURIDHISHI

Na Fatuma Bashir
IKIWA ni mwaka mmoja sasa tango utekelezaji wa mpango wa matokeo  makubwa sasa BRN imeelezwa kuwa hali ya utekelezaji huo bado si ya  kuridhisha.


Imeelezwa kwamba baada ya ya mwaka 2013 Serikali ya Tanzania  kuzindua  mpango maalum  wa ufuatiliaji  utekelezaji  wa mipango na   na utoaji wa huduma  kwa umma unaojulikana kama BRN,  kwa lengo  la kusukuma  maendeleo na kuharakisha utekelezaji mipango  na kuleta  matokeo  yaliyokusudiwa  upesi  kama hatua ya mwanzo ya BRN,   ilichagua  sekta sita  za mfano ambazo ni  Kilimno. Maji,  Elimu, Nishati  na madini, Fedha na Usafirishaji.


Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu  Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki Elimu, Bwana Godfrey Boniventura  alisema, licha ya serikali kuanza kufanya  na kutoa tathmini  ya  mpango huo kupitia jopo la  Kimataifa la Tathmini (IRP), Taasisi hiyo  kama mdau wa Elimu  imefanya tathmini  yake  ili kupima ufanisi  wa  matokeo ya mpango huo  katika sekta hiyo ya elimu kwa mwaka  mmoja  na kubaini kwamba matokeo bado si ya kuridhisha.


Alisema, katika  sekta ya elimu  yaliyopangwa kutekelezwa  katika  kipindi cha mwaka mmoja kati ya 2013/14,  ni pamoja na kuongeza   ufaulu hadi kufikia asilimia 70 mwaka 2014, kutoa ruzuku iliyopamgwa  kwa kila mwanafunzi, kutoa mafunzo ya uongozo kwa walimu 19035  kufikia Septemba 2013, mafunzo kwa walimu 12300 juu ya ufundishaji  wa KKK, kujenga nyumba 500 za walimu kwa shule za sekondari.
Mengine ni kukarabati miundombinu kwa shule 1200 za sekondari na  kuhakikisha kuwa uwiano wa mwanafunzi kwa kitabu unashuka kutoka  kitabu kimoja kwa wanafunzi watano hadi vutabu sita kwa mwanafunzi  mmoja.


Biniventura alisema japokuwa taarifa ya jumla ya jopo la IRP, inasema  mwelekeo wa utekelezaji wa BRN ni mzuri, katika ufuatiliaji uliofanywa  na Haki Elimu katika sekya ya elimu kwa karibu sana imebaini kuwa hali  ya utekelezaji wake bado si ya kuridhisha.


"Mathalani BRN ilipamnga kuongeza kiwango cha ufaulu kwa shule za  sekondari na msingi hadi kufikia asilimia 60 mwaka 2013 na silimia 70  mwaka 2014, pamoja na matokeo kuonyesha matokeo kuonyesha  ongezeko la ufaulu kutoka asilimia 50.6 (2012) hadi kufikia asilimia 50  (2013) kwa shule za sekondari na kutoka asilima 30.7 mwaka 2012  hadi asilimia 50.6 mwaka 2013 kwa shule za msingi, bado lengo la  asilimia 60 halikufikiwa", alisema  Biniventura na kuongeza kuwa,


"Hali hiyo inaonyesha kuwa lengo la ufaulu kwa shule za sekondari  kufikia asilimia 60 kwa mwaka 2013 limefanikiwa kwa asilimia karibu 79  na kwa asilimia 42 tu kwa shule za msingi".


Alisema hata hivyo ufaulu wa sekondari siyo wa kujivunia kwa sababu  matokeo ya mtihani wa mwaka 2013 yametumia viwango vipya vya  madaraja na hivyo haiwezekani kusema yametokana na utekelezaji wa  BRN.


Boniventura alisema kwa upande wa ruzuku BRN, imeshindwa kufikia  lengo la kupeleka ruzuku iliyokamilika katika mwaka wa fedha 2013/14  wakati shule za msingi zilipaswa kupokea wastani wa sh. 10,000 kwa  kila mwanafunzi lakini ni wastani wa sh. 3580 tu kwa kila mwanafunzi  uliofika shuleni na wastani wa sh. 16, 384 tu ukifika shule za sekondari  badala ya sh. 25,000 uliopangwa.


Alisema mwenendo huo wa utoaji ruzuku siyo dalili tu za kuyofikiwa  malengo ya BRn bali pia ni ishara hasi ya kufikia lengo la kuboresha  elimu hapa nchini kwa sababu ruzuku ya wanafunzi ndicho chanzo kikuu  cha mapato kwa shule za umma ambapo hutumika kununua vifaa vya  kufundishia na kujifunzia na kukidhoi gharama ndogondogo za  uendeshaji wa shule hivyo shule zimapokosa ruzuku zinashindwa  kunoresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia na hivyo kuathiri  ubora wa elimu itolewayo shuleni.


Boniventura alisema BRN pia ilikuwa imeazimia kuwa hadi kufikia  Septemba 2014 serikali itakuwa imefanya ukarabati na ujenzi wa  miundombinu kwa shule 792 lakini hadi kufikia Machi 2014 ni shule 56  tu ndizo zilikuwa zimefanyiwa ukarabati.


Alisema licha ya BRN kujikita katika ujenzi na ukarabati miundombinu  lakini changamoto ya ubovu wa miundombinu bado ni kubwa kwa shule  nyingi, takwimu za BEST, 2014 zinaonyesha kuwa wa shule za  sekondari kuna upungufu mkubwa wa maabara 1355 sawa na asilimia  94.8, za kilimo, maabara 4416 za baiolojia sawa na asilimia 76.4,  maabara za kemia 4461 sawa na asilimia 72.6 na maabara za Fiizikia  1024 sawa na asilimia 75.


Pia kuna upungufu wa nyumba 51187 za walimu sawa na asilimia 72,  madarasa 13591 sawa na asilimia 22.6 na matundu ya vyoo 44926  sawa na asilimia 40, hali ikiwa mbaya zaisi kwa shule za msingi ambapo  kuna upingufu wa vyoo 27,736 sawa na asilimia 60.3 ambapo uwiamo  wa wanafunzi wa tundu la choo ni 1:53 badala ya 1:23 kwa wavulana  na 1:51 kwa wasichana badala ya 1:20.


Alisema, pia kuna upunguzu wa madarasa 82,788 sawa na asilimia 41  ambapo uwiano wa wanafunzi kwa darasa ni 1:72 na tatizo ni kubwa  zaidi kwa mikoa ya Rukwa uwiano 1:84, Geita 1:126 na Mwanza 1:110,  upungufu wa nyumba za walimu 16,007 sawa na asilimia 79 na  madawati milioni 1.2 sawa na asilimia 37.7.


Boniventura alisema, serikali pia ilikusufdia kutoa mafunzo kwa walimu  19, 350 kwa shule za msingi na sekondari hadi ifikapo Septemba 2013  lakini taarifa za utekelezaji zinaonyesha kuwa hadi kufikia Aprili 2014  serikali iliweza kuwapatia mafumzo ya uomgozi walimu 3469 tu ambao  ni wa shule za sekondari na hivyo kuwa imetekeleza lengo hilo kwa  asilimia 18 tu.


Alisema changamoto kubwa inaonyesha kuwa walimu wa shule za  msingi ambao hadi kufikia Septemba 2014 hakuna hata mwalimu  aliyepatiwa mafunzo ya uongozi kati ya walimu 15,524 waliotarajiwa  kupatiwa mafunzo hayo.

UTIAJI SAINI MKATABA WA KUJENGA UMOJA NA KUKIUNGANISHA UPYA CHAMA TAWALA CHA SPLM CHA SUDANI KUSINI

MKATABA wa kujenga tena umoja na kukiunganisha upya Chama Tawala cha Sudan Kusini cha Sudan People’s Liberation Movement (SPLM) ulitiwa saini usiku wa jana, Jumatano, Januari 21, 2015, katika sherehe ya kufana iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Ngurdoto, Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha.
Mkataba huo unaojulikana kama Agreement on the Re-unification of Sudan People’s Liberation Movement umepongezwa kuwa ni hatua muhimu katika kulitoa taifa changa la Sudan Kusini katika hali ya machafuko, vita vya wenyewe kwa wenyewe, kutoelewana na kutoaminiana, mambo ambayo yameligubika taifa hilo tokea mwishoni mwa 2013 wakati kutokuelewana kulipozuka ndani ya SPLM na hatimaye katika Serikali ya nchi hiyo.
Viongozi waliotia saini ni Mheshimiwa Salva Kiir Mayardit, Rais wa Sudan Kusini ambaye pia ni Mwenyekiti wa SPLM na anayeongoza kundi linalojulikana kama SPLM in Government (SPLM-IG), Mheshimiwa Dkt. Riek Machar ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa SPLM na pia aliyekuwa Makamu wa Rais wa Sudan Kusini anayeongoza kundi la SPLM in Opposition (SPLM-IO) na Dkt. Deng Alor Kuol ambaye anaongoza kundi la SPLM Leaders- Former Detainees (SPLM Leaders – FD).
Sherehe hiyo ilishuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho kimesimamia mazungumzo yaliyozaa Mkataba huo. Rais Kikwete pia ndiye mdhamini mkuu wa Mkataba huo.
Wengine walioshuhudia tukio hilo muhimu ni Rais wa Uganda, Mheshimiwa Jenerali Yoweri Kaguta Museveni; Rais Uhuru Muigai Kenyatta wa Kenya; Naibu wa Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mheshimiwa Cyril Ramaphosa, Makamu Mwenyekiti wa zamani wa CCM Mheshimiwa John Samwel Malecela ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa mazungumzo yaliyozaa Mkataba huo na Katibu Mkuu wa CCM Mheshimiwa Abdulrahman Kinana ambaye alikuwa mwezeshaji wa mazungumzo.
Mazungumzo yaliyozaa Mkataba huo yalianza mwishoni mwa mwaka jana baada ya Rais Kikwete na Chama cha CCM kuombwa na Rais Kiir Mayardit kukubali chama hicho tawala cha Tanzania kutumia uzoefu na ujuzi wake wa miaka mingi wa uongozi na siasa kujaribu kuleta suluhu ndani ya SPLM.
Mazungumzo hayo ya kutafuta suluhu ambayo yamefanyika kwa awamu mbili, ya kwanza yakiwa yamefanyika Oktoba mwaka jana na pili yakiwa yameanza mwanzoni mwa mwezi huu, Januari 2015,  yameongeza thamani kwenye mazungumzo mengine yanayofanyika Addis Ababa, Ethiopia chini ya usimamizi wa taasisi ya IGAD na yanayojadili jinsi ya kurejesha amani nchini humo.
Viongozi wa SPLM wanaamini kuwa kwa sababu mgogoro wa kisiasa nchini mwao ulianzia ndani ya chama hicho na kwa sababu SPLM ndicho chombo pekee ambacho kinawaunganisha wananchi wote wa Sudan Kusini, basi busara inaelekeza kuwa suluhu ianze kutafutwa ndani ya chama hicho.
Mkataba wa jana, kimsingi, unalenga kuweka mazingira ya kujenga utulivu, maelewano, amani na umoja wa kudumu ndani ya chama hicho na nchini humo kwa kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mambo ya msingi yaliyokubaliwa kuhusu shughuli za siasa, uongozi na oganisheni ya chama hicho yanafanyika bila kukawia.
Mkataba huo pia unalenga kuhakikisha kuwa chama cha SPLM kinabuni na kutekeleza sera za kuondokana na ukabila, makundi yenye mitazamo finyu na mwenendo wa kijeshi katika siasa za Sudan Kusini.
Aidha, Mkataba huo unalenga kuhakikisha kuwa chama cha SPLM kinafanya mageuzi ya kuanza kujenga utamaduni wa kuvumiliana na ujenzi wa misingi ya demokrasia.
Mkataba huo pia unataka watu wote ambao walishiriki katika mauaji na umwagaji damu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe wasiruhusiwe kugombea wala kushika nafasi ya uongozi wa umma ndani ya chama hicho.
Pia viongozi wote wa Sudan Kusini wanatakiwa, chini ya Mkataba huo, kuwaomba radhi wananchi wa nchi hiyo ya Sudan Kusini kwa kuruhusu nchi hiyo kuingia katika machafuko ya umwagaji damu mkubwa.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.

VIDEO MPYA: Y-TONY FT BARNABA - MAMA

NYALANDU AZIDI KUFANYA MAKUBWA MALIASILI NA UTALII, MAREKANI NA UJERUMANI WAIPA TANZANIA VIFAA VYA KISASA KUKABILIANA NA UJANGILI MBUGA YA SELOUS LEO

Jan 21, 2015

Meneja wa Mbuga ya wanyama ya Selous, Benson Kibonde akimpatia maelezo kuhusu masalia ya injini ya mvuke iliyoachwa na Wajerumani, kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Lazao Nyalandu (kushoto), waziri huyo alipofika katika mbuga hiyo, kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kupokeavifaa vya kukabiliana na ujangili vilivyotolewa na serikali za Marekani na Ujerumani kwa ajili ya Mbuga ya Selous leo
Maelezo kuhusu masalia hayo ya  injini hiyo ya moshi iliyoachwa na wajerumani Benson Kibonge
Waziri Nyalandu akitembela maeneo mbalimbali ya mbuga hiyo ya Selous kabla ya kukabidhiwa vifaa hivyo ya kukabiliana na ujangili katika mbuga ya wanyama ya Selous leo. anayemuongoza na Meneja wa mbuga hiyo
Waziri Nyalandu akisalimiana na Ofisa Mawasiliano na Umma wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania,  David Feloemann, alipowasili kwenye mbuga ya Selous leo
Mkurugenzi wa theNkoromo Blog, Bashir Nkoromo, ambaye alialikwa kwenye hafla hiyo, akitazama mto Ruaha unaopita katika mbuga ya Selous


Waandishi wa habari wakiwa kwenye hafla hiyo
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akizungumza maneno ya Utangulizi kabla ya kukabidhiwa vifaa vya kukabiliana na ujangili kutoka na serikali za Marekani na Ujerumani katika hafla hiyo. Kulia ni Balozi wa Mrekani Mark Childress na waili kulia ni Balozi wa Ujerumani Egon Kochanke
Balozi wa Marekani nchini, Mark Childress akizungumza kabla ya kutiliana saini na Nyalandu mkataba ya kukabidhiana vifaa hivyo. Kushoto ni Balozi wa Ujerumani  Egon Kochanke
Balozi wa Marekani Mark Childress na Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania, Lazaro Nyalandu wakitiliana saini mkataba wa Marekani kuipa Tanzania msaada wa mafunzo yakiwemo ya kikomandoo kwa askari wa wanyamapori na vifaa vya kisasa vya kukabiliana na ujangili katika mbuga ya wanyamapori ya Selous leo.
 Waziri Nyalandu akibadilishana hati na Balozi wa Marekani, Mark Childress baada ya kusaini mkataba huo. Kushoto ni Balozi wa Ujerumani Egon Kochanke
 Waziri Nyalandu akibalidilishana hati na Balozi wa Ujerumani Tanzania  Egon Kochanke, baada ya kutiliana saini mkataba wa ujerumani kuipa Tanzania msaada wa vifaa vya kisasa vya kukabiliana na majangili katika mbuga ya wanyama ya Selous leo
 Waziri Nyalandu akimshukuru balozi huyo wa Ujerumani baada ya kubadilishana hati walizosaini. kulia ni Balozi wa Marekani Tanzania Mark Childress

 Waziri Nyalandu akitoa maelezo baada ya kutiliana saini na mabalozi wa Marekani na Ujerumani
 Vifaa mbalimbali vya kisasa vilivyotolewa na serikali za Marekani na Ujerumani kwa ajili ya kukabiliana na majangili katika mbuga ya wanyamapori ya Selous
 Askari wa Wanyamapori Anita Albert akijaribu kionambali ambacho ni miongoni vya vifaa vilivyotolewa kwa Tanzania na Seriali za Marekani na Ujerumani kwa ajili ya kukabiliana na ujangili
Askari wa wanyamapori wakikagua mahema ambayo ni miongoni mwa vifaa vya kisasa vilivyotolewa na serikali za Marekani na Ujerumani kwa ajili ya kukabiliana na ujangili katika mbuga ya wanyamapori ya Selous. Picha zote na Bashir Nkoromo wa theNkoromo Blog

MKOA WA MBEYA WAIOMBA IDARA YA MAMBO YA KALE KUWAKABIDHI MAKUMBUSHO YA MAMBO YA KALE YA KIMONDO

Wanahabari  wakitazama  Kimondo
Mwanahabari  wa Habari  leo  Iringa na mwenyekiti wa chama  cha waandishi wa habari  mkoa  wa Iringa Frank  Leonard  akitoka  kutazama  Kimondo
Mgeni  akisaini kitabu cha wageni katika  ofisi ya makumbusho ya mambo ya kale  ya  Kimondo Mbeya
Wanahabari wakitoka katika  Kimondo  kulia na Slvanus  Kigomba  (ITV) na kulia ni Iren Mwakalinga (TBC),nyuma yao ni ofisi ya makumbusho  hayo
Mhifadhi  akionyesha  jiko  ambalo  linatumika  eneo  hilo
Nyumba ya  wahifadhi  wa makumbusho ya mambo ya kale ya  Kimondo Mbeya
Mhifadhi  msaidizi  wa makumbusho ya  Kimondo  akiingia katika nyumba  yake
Hii  ndio  nyumba  ya  mhifadhi mkuu na mhifadhi msaidizi wa Kimondo  Mbeya

Mwanahabari  wa ITV Iringa  Slvanus Kigomba  akijipumzisha kando ya  Kimondo
Mwanahabari  wa Star Tv Iringa  Mawazo Marembeka  kushoto akiwa na mzee  wa matukiodaima katika Kimondo
Wanahabari  wakimhoji mhifadhi msaidizi  wa makumbusho ya mambo ya kale ya Kimondo Mbeya  Bw Mussa Nsojo
Hiki  ndicho  kimondo  kina tani 12
Afisa utalii kanda  ya  kusini Tanapa  Bi Risala kabongo akiwa katika kibao  cha Kimondo
Na MatukiodaimaBlog
MKOA  wa  mbeya   umepania  kuboresha miundo  ya  kituo cha mambo ya  kale  cha  Kimondo wilayani Mbozi mkoani hapa  iwapo Idara ya Mambo ya kale iliyopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii itakubali  ombi la mkoa   huo  kukabidhi  kivutio  Halmashauri  ya  Mbozi.

Hatua   hiyo   imekuja  kufuatilia ziara ya  wanahabari  mkoani Iringa wanaotembelea vivutio  vya  utalii  mikoa ya  Mbeya, Njombe na Iringa  kama  njia ya  kuhamasisha  utalii  mkoa ya nyanda  za  juu  kusini na pia  kubaini sababu  za  utalii kutokua kwa kasi katika  mikoa   hiyo  .

Mhifadhi  msaidizi  wa  kituo  cha makumbusho ya  mambo ya kale ya  Kimondo  wilayani  Mbozi Bw Mussa Nsojo alisema  kuwa  mbali  ya  watalii wengi  kupenda  kutembelea  eneo  hilo la Kimondo ila miundo  mbinu ya  eneo  hilo si rafiki kwa  watalii kuendelea  kutembelea  kutokana na  serikali  kushindwa  kuboresha  majengo na  eneo  hilo kwa  ujumla.

Alisema  kuwa  kimondo  hicho  ambacho mwaka kilipoanguka  eneo  hilo haufahamiki ila  utafiti wake ulianza kati ya  mwaka 1930 -1931 na kubainika  kuwa  si  jiwe la kawaida  bali ni sayari iliyoanguka  kutoka angani  toka  wakati   huo  kimendelea  kupata  umaarufu  wa  watalii kufika  kutembelea  eneo hilo japo katika  eneo  hilo mazingira  yake ni mabovu  zaidi.

Mhifadhi   huyo  akielezea  historia  ya  kimondo  hicho  alisema  kabla  ya  watafiti  kubaini  kuwa ni  kimondo miaka  ya  nyuma kulikuwa na wenyeji  ambao walikuwa  wakiishi  eneo  hilo na  mkazi  mmoja aliyefahamika  kwa jina la Harele  ambae  alikuwa akifanya kazi  ya uhunzi kuweza kubaini jiwe  hilo la ajabu wakati akitafuta  udongo chuma kabla  ya  kumega kipande  kidogo na kutengenezea shoka .

Alisema  kutokana na wakati   huo chuma kuwa na dhamani  kubwa alipeleka taarifa  kwa chifu  wa  eneo  hilo na  kulifanya  eneo hilo  kuwa  la tambiko kabla utawala  wa Waingereza  kuchukua eneo  hilo na  kulihifadhi kabla  ya  serikali ya  Tanzania  kupitia idara ya mambo ya  kale  kuhifadhi  eneo  hilo.

Kuhusu  changamoto  kubwa  zilizopo eneo  hilo alisema ni pamoja na kukosekana kwa  nyumba  bora  za watumishi ,jengo la ofisi  ya makumbusho  kutokana na kibanda  kilichopo  kutokuwa na sifa ya utalii ,pia miundo mbinu  ya barabara  kufika  kituoni hapo.

Afisa  utalii ofisi ya utalii kanda  ya kusini Bi Risala Kabongo akielezea  kivutio   hicho  alisema  kuwa  ni  moja kati ya  vivutio  visivyo  vya kawaida  hapa  nchini na kuwa  iwapo  serikali itaboresha  zaidi  eneo hilo upo uwezekano  wa uchumi  wa  mkoa  wa Mbeya kukua  zaidi  kupitia kivutio  hicho .

" Kivutio   hiki kinavutia   zaidi ila ushauri  wangu  kwa serikali ni kuboresha  miundo  mbinu ikiwa ni pamoja na kutenga eneo la banda la  wageni na eneo la kujenga mahema kwa  wageni.....Kimondo  hiki  kimetoka katika  sayari ya Mars na  hivyo ni  kivutio  cha ajabu  zaidi"

Katibu  tawala msaidizi (miundombinu)  mkoa  wa  Mbeya  Kastory Msigala  alisema  kuwa mkoa  huo  kupitia  kikao  chake  cha kamati ya ushauri ya  mkoa  kimeiandikia  barua  idara ya mambo ya kale  ili kuipa eneo hilo  la Kimondo Halmashauri ya  Mbozi  ili  kusimamia kwa lengo la  kuiboresha  zaidi.

Kwani  alisema  shida  kubwa ya  Halmashauri  hiyo na mkoa  kushindwa  kuboresha  majengo na miundo  mbinu  inayozunguka  makumbusho hayo ni  kutokana na kutokuwa na mamlaka ya  kufanya  hivyo kutokana na usimamizi wa eneo  hilo  kuwa  chini ya idara ya mambo ya kale ila pale  idara  hiyo  itakapokabidhi katika serikali ya  wilaya  upo uwezekano wa  wilaya  kusimamia  vizuri  zaidi.

Alisema katika mkoa   huo kuna  jumla  ya  vivutio 13  vilivyotambuliwa kikiwemo  kivutio   hicho  cha Kimondo  na  kuwa mbali ya  vivutio   hivyo  bado  mkoa  umejipanga zaidi  kutangaza  utalii  kufuatia ushirikiano mkubwa  uliopo kati ya  mkoa huo na ofisi ya SPANEST  , bodi ya utlii ,wizara  ya utalii na wadau mbali mbali  kukuza  utalii mkoani  humo .

NAPE: CCM HAITARUHUSU WANUNUA URAIS KUPENYA UCHAGUZI MKUU WA MWAKA HUU

Jan 20, 2015

> . Asema wanapoteza muda na pesa zao
>. Awataka wakumbuke salaam za mwaka mpya 2015 za CCM.
>. Ajivunia uzoefu wa CCM kudhibiti wasio waadilifu
>. Atamba CCM kufanya vizuri uchaguzi mkuu 2015.
>. Awataka Watanzania kuiombea nchi ipate kiongozi mwadilifu.
Na Mwandishi Wetu, Kibaha
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM Ndg. Nape Nnauye amewaibukia tena wasaka urais ndani ya CCM na kudai kuwa Chama hicho hakitatoa mwanya kwa wanaosaka uteuzi huo kwa kununua wajumbe mbalimbali wa vikao husika.

Nape ameyasema hayo jana kwenye  mafunzo kwa wachungaji wote wa huduma ya Efatha nchini yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani. Nape alikuwa akitoa mada inayohusu nafasi ya CCM na uhusiano wa CCM katika jamii.


Pamoja na Nape ambaye aliwakilisha CCM kwenye mafunzo hayo walikuwepo watoa mada wengine kutoka vyama vingine vya upinzani nchini.


Akizungumzia mada ya nafasi na uhusiano wa CCM ndani ya jamii, Nape alisema historia ya Chama hicho ambayo haiwezi kwa vyovyote kufanana na ya chama chochote kilichopo au kijacho nchini ni moja ya sababu kubwa ya Watanzania kuendelea kukiamini Chama hicho. Aliongeza kuwa sababu kubwa ya pili ni misingi ambayo Chama hicho kinaiamini ambayo ndio imelifanya taifa la Tanzania kuwa taifa.


Nape alisema CCM ipo kila kona ya nchi na hivyo inamtandao mkubwa kuliko taasisi yeyote nchini, na hiyo ndio moja ya siri za uimara wa CCM.


Akizungumzia swala la maadili Nape alidai kuwa CCM ndio chama duniani chenye nyaraka nyingi na bora zinazozungumzia maadili ya viongozi. Pamoja na nyaraka hizo alisema mfumo wa uchujaji majina hasa kwa nafasi ya urais kupitia CCM hautoi nafasi kwa mgombea yeyote wa nafasi hiyo kupita kwa kununua uteuzi huo.


Alisema Nape kuwa wasaka urais wanaohangaika kutoa pesa zao kujaribu kununua uteuzi wa CCM wanapoteza muda na pesa zao kwani Chama hicho hakitawateua kugombea nafasi hiyo.


Nape akatumia nafasi hiyo kuwaomba wachungaji hao kukiombea Chama hicho na viongozi wake wawe na ujasiri wa kulisimamia hilo kwani kupitisha wagombea walionunua uteuzi huo ni kukaribisha laana kwa nchi.


" Nawahakikishia kuwa hakuna mnunua urais atakayepenya mchujo ndani ya CCM. Kuruhusu mtu wa namna hiyo kupenya ni kuleta laana kwa nchi yetu,hivyo viongozi wa dini tuombeeni tuwe na ujasiri wa kutosha kukataa laana hii" alisisitiza Nape.


Nape alisema mwanzoni mwa mwaka huu wa 2015 Katibu Mkuu wa CCM  Ndg. Kinana akitoa salaam za mwaka mpya za CCM mjini Tanga, aliwaambia Watanzania kuwa CCM imekuwa ikisimamia maadili kwa miaka yote lakini mwaka huu itaongeza ukali ili kuhakikisha nchi inapata viongozi waadilifu watakaoisaidia nchi kupiga hatua zaidi.


Anasema Nape hakuna atakayeingia madarakani kwa rushwa atakayeunda serikali itakayokusanya kodi. Bila kukusanya kodi hakuna namna nchi itapiga hatua ya maendeleo na huduma za kijamii zitadumaa na hivyo kusababisha maisha magumu na hiyo itakuwa laana kwa nchi.


Semina hiyo inayofanyika Kibaha mkoani Pwani itahitimishwa tarehe 24/01/2015 na imehusisha wachungaji wa huduma ya Efatha nchi nzima, na baadhi ya wachungaji kutoka nchini Kenya.

HABARI KAIKA PICHA
 MTUME na Nabii wa Kanisa la EFATHA Josephat Mwingira akimlaki kwa furaha, Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alipowasili katika ukumbini, kutoa mada kuhusu nafasi ya CCM na uhusiano wa CCM katika jamii, kwnye semina ya wachungaji wa kanisa hilo wa ndani na nje ya Tanzania, inayoendelea Kibahaka mkoa wa Pwani. Watatu kulia ni Mama Eliakunda Mwingira.
 Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akitoa mada kwenye semina hiyo
 Nape akifafanua jambokuhusu CCM ilivyo imara licha ya kuwa na mapungufu kama Taasisi kubwa
 "Hili Chama ni kubwa sana, siyo rahisi kuling'oa madarakani, ukiona unakereka a mambo ingia humohumo ndai ya Chama ukisafishe... hiyo ndiyo dawa", akisema Nape kwenye Semina hiyo
 "Hatukatai kwamba CCM haina mapungufu, inayo lakini mifumo yake ni mizuri kuliko Chama chochote Afrika na pengine duniani kote", alisema Nape kweny Semina hiyo.
 Nabii Mwingira na Mkewe wakimsikiliza Nape kwa makini wakati akitiririka kwenye utoaji mada kwenye semina hiyo
 Washiriki katika semina wakifuatilia kwa makini wakati Nape akitoa mada kwenye semina hiyo
 "Katiba hii ya CCM imesheheni kila kitu.. tatizo ni baadhi ya watu kusuasua katika kuyatekeleza" anasema Nape.
 Nape akimaliza kutoa mada yake kwa kuwaomba watanzania kuhakikisha nchi inapata mgombea wa Urais aliye bora na siyo kwenye kuinunua nafasi hiyo muhimu
 Nape akirejea kuketi baada ya kutoa mada kwa zaidi ya saa moja na nusu kwenye semina hiyo
 Washiriki wakimshangilia Nape baada ya mada yake
 Nape akijibu maswali yaliyoulizwa na washiriki baada ya kutoa mada yake
 Mtume na Nabii Mwingira akitoa maelezo kusadifu maneno aliyotoa Nape katika mada yake.

 Waumini wakiombea Tanzania, CCM na Nape kudumu katika mwendendo ulio bora kwa manufaa ya Taifa la Tanzania
 Nape akiwa amesimama wakati wa maombi hayo
 Nape akienda kukutana na Mwingira kwa ajili ya kuagana baada ya semina
 "Kijana umetoa mada nzuri, Mungu amekuonyesha njia, umezungumza na kujibu maswali vema" Mwingira akimwambia Nape wakati akimsindikiza ktoka ukumbini
 Mtume na Nabii Mwingira akimsindikiza Nape huku wakionyesha kuwa wenye furaha kwa tukio lililotokea la CCM kushiriki kutoa mada kwenye semina hiyo
 Mwingira akimsindikiza Nape hadi nje ya ukumbi
 Mwingira na Nape wakiingia jengo la Utawala la EFATHA, kwa ajili ya kuagana rasmi. Picha zote na Bashir Nkoromo