Breaking News

Your Ad Spot

Oct 16, 2010

KILA NCHI INAYOHAKI KUTUMIA NISHATI YA NYUKLIA KWA MATUMIZI SALAMA

MKURUGENZI wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar, Katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mohammed Hamza, akichangia mjadala uliofanyika makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York,  Marekani, kuhusu silaha za nyuklia ambapo alisisitiza kuwa Tanzania inaunga mkono matumizi salama ya nishati hiyo  kwa maendeleo endelevu na si utengenezaji wa na umiliki silaha za maangamizi
================================
NA MWANDISHI MAALUM
NEW YORK
Tanzania imesisitiza haki ya msingi ya kila nchi kuendeleza na kunufaika na teknolojia ya nishati ya nyuklia kwa matumizi salama, lakini inapinga umiliki wa silaha za nyuklia kwa nchi yoyote na kwa sababu zozote zile.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi Mohamed Hamza, Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wakati alipokuwa akichangia mjadala wa siku tatu kuhusu silaha za nyuklia , mjadala huo unafanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Akasema kuwa Tanzania inasisitiza matumizi salama ya nishati hiyo na kupiga matumizi ya silaha kutokana na ukweli kwamba kuendelea kuwapo kwa silaha za nyuklia kunaifanya dunia iendelee kuwa si mahali salama.

Akaongeza kwamba jukumu la nchi wanachama libakie katika kutokomeza silaha hizo na kuchochoea matumizi ya kimaendeleo na salama ya nishati ya nyuklia bila ya ubaguzi wowote na kwa kuzingatia Mkataba wa NPT.

Hata hivyo akasema kuwa juhudi zinazofanywa hivi sasa na jumuia ya kimataifa za kupokonya ama kuzuia baadhi ya nchi zisitengeneze au kuwa na uwezo wa kinyuklia zinaibua maswali mengi miongoni mwa nchi wanachama na wakati mwingine kuonekana kama ni za unafiki.

Balozi Hamza , akabainisha kuwa licha ya ukweli kwamba silaha hizo zinaufanya usalama wa kimataifa kuwa wa mashaka, lakini cha kutisha zaidi nipale silaha hizo zinapoweza kuangukia kwenye mikono vya makundi ya kigaidi au vyombo visivyostahili.

“ kutokana na ukweli huu, Tanzania inapenda kusisitiza kwamba kila nchi inaowajibu wa hiari na wa kisheria wa kuzitokomeza silaha hizo, silaha ambazo mara mbili katika karne iliyopita dunia imeshuhudia madhara makubwa kwa wanadamu na mazingira” akasema Balozi Hamza.

Akaueleza mkutano huo ambao unahudhuriwa na nchi ambazo ni wanachama wa mkataba wa kimataifa dhidi ya usambazaji wa silaha za nyuklia, kwamba ni athari na matumizi ya zana hizo za kinyuklia ndizo zilizomfanya mwanadamu aape kutotumia tena silaha hizo.

“ Hiki ni kiapo kilicho katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa uliopitishwa miaka 65 iliyopita. Kutotekeleza kwa vitendo kiapo hicho ni sawa na kusaliti utu wetu” akasisitizia.

Na akataka kuwapo kwa ushirikiano baina ya nchi tajiri na maskini katika eneo hili, kwa kile alichosema kutachangia kuziba ama kupunguza pengo lililopo la maendeleo na teknolojia baina ya nchi hizo.

Tanzania ni mwanachama wa Mkataba wa Kimataifa dhidi ya Usambaji wa Silaha za Nyukllia (NPT) na Mkataba wa Pelindaba unaoanzisha Ukanda wa Afrika bila silaha za Nyuklia.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages