Breaking News

Your Ad Spot

Nov 9, 2010

TANZANIA YAPONGEZA JUHUDI ZA MAREKANI ZA KUANZISHA TENA MAZUNGUMZO YA AMANI KATI YA ISRAEL NA PALESTINA

BALOZI WA TANZANIA KATIKA UMOJA WA MATAIFA, OMBENI SEFUE AKIZUNGUMZA WAKATI WA MKUTANO WA BARAZA KUU  LA UMOJA WA MATAIFA ULIOKUWA UKIJADILI TAARIFA YA KAMATI MAALUM ILIYOCHUNGUZA VITENDO VYA UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU VINAVYOFANYWA NA ISRAEL DHIDI YA WANANCHI WA PALESTINA
==============
STORI


• YASISITIZA KUIUNGA MKONO PALESTINA KUWA TAIFA HURU

NA MWANDISHI MAALUM
NEW YORK-
Tanzania imepongeza juhudi zinazofanywa na serikali ya Marekani za kuanzisha tena mazungumzo ya kutafuta amani kati ya Israel na Palestina.

Pongezi hizo zimetolewa na Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Ombeni Sefue wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipokuwa likijadili taarifa ya Kamati Maalum iliyohusika na uchunguzaji wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wananchi wa Palestina unaofanywa na Israel.

“Tanzania tunaunga mkono hatua hii iliyochukuliwa na serikali ya Marekani ya kufufua mazungumzo haya. Tunaishukuru na tunaihimiza kuendelea na juhudi hizo na tunawatakiwa mafanikio mema ”.Anasema Balozi Sefue

Aidha mwakilishi huyo wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa ameeleza kwamba, Tanzania pia inapenda kutambua michakato mingine inayofanywa na Umoja wa Mataifa, Jumuia ya Ulaya, Urusi , Misri pamoja na wadau wengine katika kutafuta amani na muafaka wa kudumu kati ya Israel na Palestina.

Hata hivyo, pamoja na kuipongea Marekani na wadau wengine katika uendelezaji wa mchakato wa kutafuta amani ya kudumu kati ya mataifa hayo mawili. Balozi Sefue hakusita kuelezea msimamo wa Tanzania wa kuungana na nchi nyingine katika kuelezea masikitiko yake ya namna Israel inavyoendelea na harakati zake za ujenzi wa makazi katika eneo linalokaliwa isivyo kihalali na Israel, mipaka ya Palestine, eneo la Mashiriki ya Jerusalemu na maeneo mengine ya Kiarabu.

Akasema wazi kuwa Tanzania inasikitishwa sana na upanuzi wa makazi hayo, ubomoaji wa nyumba na kuondolewa kwa nguvu kwa watu kutoka Ukingo wa Magharibi likiwamo eneo la Mashariki ya Jerusalemu.

“Tanzania tunaona maendeleo haya na ujenzi kama kikwazo kikubwa katika mchakazo wa utafutaji wa amani ya kudumu. Ingawa tunatambua haki ya kiusalama ya watu wa Israel, lakini katika mtazamo huo huo tunasikitishwa na taarifa za utumiaji nguvu wa kupita kiasi dhidi ya wananchi na tunapinga matumizi hayo ya nguvu” anasisitiza Balozi Seufe.

Aidha Balozi Sefue ameueleza mkutano huo kwamba, Tanzania inaunga mkono juhudi za kumalizwa kwa mgogoro kati ya waarabu na waisrael kwa kuzingatia misingi ya sheria za kimataifa , maazimio mbalimbali ya Baraza Kuu la Usalama, hadidu za rejea za mkutano wa Madrid na mikakati mingine ya amani .

“ Tanzania pia inaunga mkono suala la kuwapo kwa mataifa mawili huru likiwamo la Palestine huru wakiishi sambamba katika mazingira ya amani na salama na taifa la Israel huku tukiunga mkono haki ya waisrael kuishi kwa amani”

Tanzania pia imesisitiza utekelezwaji wa azimio namba 1860 la mwaka 2009 la Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kuheshimu sheria za kimataifa na kufunguliwa bila ya mashariti njia za kupitishia misaada ya kibinadamu, biashara na watu.

Kwa kuzingatia misingi hiyo Tanzania, anasema Balozi Sefue, inakaribisha juhudi za hivi karibuni zilizotangazwa na serikali ya Israel za kulegeza vikwazo katika Ukanda wa Magharibi na uingizaji wa bidhaa huko Gaza, na kusisitiza kuchukuliwa kwa hatua zaidi.

Katika hatua nyingine Mwakilishi wa Tanzania Katika Umoja wa Mataifa, anatamka bayana kwamba Tanzania inapenda kusisitiza msimamo wake wa kuwaunga mkono wananchi wa Palestina katika jitihada zao za kuwa taifa huru ikiwa ni pamoja na kuufanya mji wa jerusalem kuwa makao makuu yake.

Akasema ni maoni ya Tanzania kuwa kwa kutambua na kuwapatia haki hii wapalestina ni njia muafaka na sahihi na yenye manufaa kwa pande zote yaani waisrael na wapaletina kwani wote watanufaika na kuwapo kwa amani ya kudumu.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages