MKUTANO wa Wadau wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), unaanza kesho katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) mjini Arusha na unatarajiwa kufunguliwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Mkuu wa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa NSSF, Eunice Chiume (pichani), ameiambia Chachandu Daily leo kwamba mkutano huo ambao ni wa kwanza na unaotarajiwa kuwa utakuwa ukifanyika kila mwaka, unatarajiwa kuhudhuriwa na wajumbe wasiopungua 700 na hadi leo asubuhi 570 walikuwa wamejisajili katika daftari la mahudhurio ya mkutano huo.
Alisema, katika ufunguzi Waziri Mkuu atawakabidhi zawadi na vyeti wadau hasa waajiri waliong'aa katika nyanja mbalimbali ikiwemo uwasiliashaji mapema na kwa usahihi michango ya wafanyakazi wao kwenye mfuko wa NSSF.
Eunice alisema, mkutano huo unafanyika katika ukumbi wa Simba , katika kituo hicho, na baada ya kufunguliwa na Waziri Mkuu utaendelea kwa siku tatu hadi Ijumaa, wiki hii.
Aliwataja wajumbe wa mkutano huo kuwa ni wadau wote wa NSSF wakiwemo waajiri, wanachama waajiriwa, wataalam mbalimbali wa masuala ya hifadhi ya jamii na wale wa kutoka mifuko mingine ya hifadhi ya ajamii na mashirika ya kifedha ya ndani na nje ya nchi.
Eunice alisema, katika siku tatu za mkutano huo, wajumbe watajadili hoja kadhaa zinazohusu NSSF na hifadhi ya ajamii kwa ujumla na changamoto zilizopo na zinazotarajiwa kuwepo.
"Mada zitakazojadiliwa ni pamoja na shughuli za uendeshaji na uwekezaji za NSSF, hifadhi ya jamii kwa sekta isiyo rasmi, kazi za mamlaka mpya inayosimamia mifuko ya hifadhi jamii na mada nyingine zitakazoelimisha washiriki juu ya masuala mbalimbali ya maisha", alisema Eunice.
Alisema NSSF inatajaria kutumia fursa ya mkutano huo, kutoa ufafanuzi wa kina kwa masuala yote ambayo yamekuwa yakiwatatiza wanachama wake na wananchi kwa jumla kutokana na kutoelewa vizuri sheria ya Shirika hilo na kanuni zake.
"Hii itasaidia kutoa mwelekeo thabiti kwa wanachama ili waajiri na waajiriwa waelewe wajibu wao na hata haki zao", Eunice alisema na kuongeza kwamba kutokana na kuona umuhimu huo ndiyo sababu NSSF haikuweka ada kwa wadau kushiriki mkutano huo.
Wafanyakazi wa NSSF wakiwa kando ya mabegi maalum yaliyoanadaliwa kwa ajili ya washiriki wa mkutano huo kutunzia makabrasha. Hapa ni katika ukumbi wa AICC leo
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269