Breaking News

Your Ad Spot

Aug 17, 2011

YANGA NA SIMBA KATIKA VITA VYA NGAO YA HISANI LEO TAIFA

NA MWANDISHI WETU
Miamba ya soka yenye mashabiki wengi hapa nchini, Yanga na Simba  leo wanaingia vitani  tena kusaka heshima zao zitakapovaana katika mchezo wa maalumu wa Ngao ya Jamii uliopangwa kuchezwa kuanzia saa 2 usiku kwenye Uwanja wa kisasa wa Taifa, Dar es Salaam.
       Mchezo huo ni maalumu kwa ajili ya ufunguzi wa pazia la michuano ya Ligi Kuu soka Tanzania lililopangwa kufunguliwa Agosti 20, ambapo timu 14 za Tanzania Bara zitachuana kuwania ubingwa unaoshikiliwa na Yanga iliyotwaa msimu uliopita.
       Pambano hilo la kukata na shoka, limepangwa kuanza saa 2.00 usiku ili kutoa fursa kwa waumini wa dini ya kiislamu waliopo katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan kupata muda mzuri wa kufuturu kabla ya kwenda uwanjani kushuhudia mtanange huo.
      Msimu uliopita Yanga ilitwaa Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Simba mabao 3-1 kwa mikwaju ya penalti mchezo uliopigwa Agosti 18, kwenye uwanja huo baada ya miamba hiyo kutoka suluhu katika muda wa kawaida.
      Mbali na kupata matokeo hayo mazuri, Yanga itashuka uwanjani ikiwa na morari kubwa ya kuendeleza ubabe kwa mahasimu wao baada ya kushinda mchezo uliozikutanisha mara ya mwisho katika mechi ya fainali ya Kombe la Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) Julai 10, walioshinda bao 1-0 lililofungwa na Kenneth Asamoah dakika 108.
     Mchezo wa Ngao ya Jamii utakuwa na changamoto kubwa, Yanga itashuka dimbani ikiwa na nia ya kuendeleza furaha kwa mashabiki wa klabu hiyo kutoka makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani na 'Wekundu wa Msimbazi' bila shaka hawawezi kukubali kulala mapema kwa kupoteza mchezo huo ambao kocha Moses Basena, ameapa vijana wake watafia uwanjani.
      Timu zitakazoshiriki Ligi hiyo  ni Yanga, Simba, Azam FC, African Lyon, Villa Squad, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Toto African, Polisi Dodoma, Coastal Union, Moro United na JKT Oljoro. Jumla ya sh. bilioni 1.2 zinazotolewa na wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom zinatarajiwa kutumika.
     Macho na masikio ya mashabiki wa klabu hizo zenye utani wa jadi, ni kushuhudia nyota wa kimataifa wakiwemo wapya watakavyoonyesha uhodari wa kucheza soka baada ya kusajiliwa kwa mamilioni ya fedha kutoka katika klabu zinazotamba katika medani ya soka barani Afrika.
     Yanga ilifanya kufuru baada ya kumng'oa kwa nguvu nahodha na 'injini' ya APR ya Rwanda, Haruna Niyonzima 'Fabregas' na mfungaji bora wa ligi ya Uganda, Hamis Kiiza kutoka URA na Asamoah ambao viwango vyao vya uchezaji vimekuwa gumzo nchini. 'Mapro' wengine ni kipa Yaw Berko na Davies Mwape.
       Kocha Mganda kama alivyo Basena, Sam Timbe anatambia vijana wengine waliopo kwenye viwango bora akiwemo kiungo aliyecheza vizuri msimu uliopita, Nurdin Bakari, Nadir Haroub 'Cannavaro', Chacha Marwa, Godfrey Taita, Julius Mrope, John Tegete na nahodha Shadrack Nsajigwa.
      Hata hivyo, Yanga huenda ikamkosa Kiiza aliyetimkia nyumbani kwao Uganda kwa madai kuwa ana matatizo ya kifamilia ingawa uongozi wa klabu hiyo umemkana na kudai mchezaji huyo anasumbuliwa na utoto.
     Kukosekana kwa Kiiza ni pigo kwa Yanga katika safu ya ushambuliaji kwani mchezaji huyo amekuwa kipenzi cha mashabiki kutokana na uhodari wake uwanjani kulinganisha na Mwape au Asamoah.
    Simba kwa upande wao walijibu mapigo kwa kumsajili mfungaji mabao wa kimataifa Mzambia, Felix Sunzu, Gervas Kago (Jamhuri ya Afrika ya Kati), Jerry Santo na Emmanuel Okwi ambao kimsingi wameonyesha uwezo mkubwa tangu walipojiunga na kigogo hicho.
     Timu hiyo imemrejesha beki wa kati hodari aliyekuwa akicheza soka ya kulipwa nchini Msumbiji Victor Costa 'Nyumba' na winga msumbufu uwanjani Ulimboka Mwakingwe na beki Said Nassoro 'Cholo'. Nyota wa zamani ni kipa Juma Kaseja, Kevin Yondan, Salum Kanoni na Juma Said 'Nyoso'. 
     Mchezo huo utakuwa wa kihistoria kwa Yanga na Simba ambazo muda mrefu zimekuwa zikitambiana kwa kila mmoja kuvutia upande wake akijinadi kuwa amefanya maandalizi ya kutosha ili kuhakikisha anawapa raha mashabiki wake kwa kutoka uwanjani kifua mbele dhidi ya mpinzani wake.
   Miamba hiyo inavaana ikiwa imetokea katika maumivu baada ya kuboronga katika mechi zao za mwisho za maandalizi. Yanga ilikuwa Khartoum, Sudan ambapo ilichapwa jumla ya mabao 6-2, ilifungwa mabao 3-1 kwa kila mchezo katika mechi mbili ilizocheza na El Hilal inayonolewa na kocha wa zamani wa timu hiyo, Sredojevic Milutin 'Micho'.
       Simba ilionja shubiri na kuliona tamasha la 'Simba Day' kuwa chungu baada ya kulazwa bao 1-0 na Victors ya Uganda katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha kabla ya kulazimishwa suluhu na AFC Leopards ya Kenya.
        Matokeo hayo yametia shaka kwa mashabiki wa klabu hizo, ingawa ukweli unabaki pale pake kwamba zinapocheza timu hizo, mtoto hatumwi dukani kwani kila mmoja anacheza kwa nguvu zote ili kuhakikisha anapata matokeo mazuri ili kulinda heshima.
       Tayari hofu imetanda kwa mashabiki wa klabu zote mbili kutokana na historia ya timu hizo zinapocheza ambapo bendera za rangi ya njano na kijani kwa upande wa Yanga, nyeupe na nyekundu kwa Simba zinatawala sehemu kubwa mitaani.
Kumbukumbu muhimu
Rekodi za Yanga na Simba kuanzia mwaka 2000. Agosti 5, Yanga ilishinda mabao 2-0 yote yakifungwa na Iddi Moshi, aliyekuwa anacheza kwa mara ya kwanza tangu ametoka kwenye fungate la ndoa yake.
Mechi iliyofuata Septemba 1, 2001, bao pekee la Joseph Kaniki ‘Golota’ alilofunga dakika 76 liliwalaza mapema Yanga.
Sekilojo Chambua, aliinusuru Yanga kulala tena mbele ya Simba Septemba 30, 2001 baada ya kufunga bao la kusawazisha dakika 86, Kaniki alifunga kwa upande wa Simba dakika 65 na timu hizo zilitoka sare bao 1-1.
Agosti 18, 2002, Chambua aliikoa Yanga baada ya mwamuzi Victor Mwandike kutoa penalti dakika 89 na miamba hiyo kutoka sare bao 1-1 baada ya Madaraka Selemani Mzee wa Kiminyio kutangulia kufunga dakika 65. Novemba 10, 2002 timu hizo hazikufungana. 
Septemba 28, 2003 mabao ya Kudra Omary na Herry Morris yaliinusuru Yanga kulala 2-0 mbele ya Simba, kufuatia Emmanuel Gabriel kufunga dakika za 27 na 36. Novemba 2, 2003 hazikufungana.
Agosti 7, 2004, Shaaban Kisiga alitangulia kuifungia Simba dakika 64, kabla ya Pitchou Kongo kusawazisha dakika 48 na Mwakingwe alifunga la ushindi 76. Simba ilishinda mabao 2-1.
Simba iliifunga Yanga bao 1-1 Septemba 18, 2004 kwa bao pekee la Athumani Machupa dakika 82.
Aprili 17, 2005 Aaron Nyanda alitangulia kuifungia Yanga dakika 39, kabla ya Nurdin Msiga kusawazisha dakika 44 na Machupa kufunga la pili dakika 64. Simba ilishinda mabao 2-1.
Agosti 21, 2005, Nicodemus Nyagawa alikuwa nyota wa mchezo kwa kufunga mabao yote mawili yaliyoipa Simba ushindi wa 2-0. Mwaka 2006, timu hizo hazikufungana katika mechi zote mbili za ligi.
Mwishoni mwa mwaka 2006 katika fainali ya Ligi Ndogo Tanzania Bara, Moses Odhiambo alitangulia kuifungia Simba kwa mkwaju wa penalti dakika ya pili ya mchezo kabla ya Said Maulid ‘SMG’ kusawazisha dakika 55. Simba ilishinda kwa penalti 5-4.
Oktoba 24, 2007 ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Mwakingwe dakika 23.
Aprili 27, 2008 zilitoka suluhu, lakini Oktoba 26, 2008, Ben Mwalala alifunga bao dakika 15. Yanga ilishinda bao 1-0. Aprili, 2009 zilitoka sare mabao 2-2. Katika mchezo wa ligi msimu 2009/2010 Simba ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Musa Hassan 'Mgosi' na ziliporudiana Aprili ilishinda 4-3.

1 comment:

  1. Visit us contemporary to obtain more knowledge and facts regarding Come to see us contemporary to buy more information and facts in the matter of [url=http://akwarystyka-morska.dogory.pl]Akwarystyka morska[/url]

    ReplyDelete

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages